Tanzania kuteta na Kenya kuhusu vibali vya malori

Muktasari:

  • Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba ameahidi kutatua kero ya madereva wa malori yanayopeleka bidhaa nchini Kenya ya kukaa muda mrefu mpakani.

Dar es Salaam. Waziri Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, amesema kuwa Serikali itawasiliana na Mamlaka za Kenya ili kutatua changamoto ya malori yanayopeleka bidhaa nchini humo kutumia muda mrefu kupata vibali vya kuvuka mpaka wa Horohoro-kuingia Kenya.

Dk Nchemba amesema hayo baada ya kuzungumza na madereva wa malori yanayobeba shehena ya mizigo kwenda  Kenya katika Mpaka wa Horohoro, akiwa njiani kwenda nchini humo kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Fedha wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Madereva hao walieleza kuwa wanapata usumbufu mkubwa kwa sababu wanatumia muda mrefu unaokadiriwa kufikia hadi siku 14 hadi 21 kuvuka mpaka wa Horohoro kwenda Kenya, wakati upande wa madereva wa Kenya wanaoingia Tanzania wanatumia siku zisizozidi 3 kuvuka mpaka huo.

Walimweleza Dk Nchemba kwamba, kuchelewa kuvuka mpaka kunawaletea matatizo makubwa ikiwemo kutumia gharama kubwa zisizolingana na posho za safari wanazopewa na waajiri wao, lakini pia kuna baadhi ya bidhaa zinaharibika kabla ya kuvuka mpaka.

Dk Nchemba amesema amebaini kuwa ucheleshwaji wa huduma ya forodha kwa Kenya unatokana na nchi hiyo kutoanza kutumia Mfumo wa Pamoja wa Huduma ya Forodha kama walivyokubaliana.

Amesema kuwa magari ya Kenya hayapati changamoto hiyo ya foleni kwa kuwa tayari Tanzania wanatumia mfumo huo ambapo mizigo yote ya Kenya hupata vibali ikiwa huko huko nchini Kenya, kabla ya kufika katika mpaka huo wa Horohoro na malori kupita bila tatizo.

Dk Nchemba amesema kuwa atawasiliana na Waziri mwenzake wa Fedha wa Kenya ili kuanza kutekeleza makubaliano ya kuweka Mfumo huo wa Pamoja na Forodha kwa kuwapeleka watumishi wa nchi hiyo upande wa Tanzania ili kuharakisha usafiri na usafirishaji wa mizigo kutoka Tanzania hivyo kuwaondolea adha wafanyabiashara na madereva wanaotumia mpaka huo kufanya biashara zao.