Tarura yaja na mkakati kupunguza gharama za ujenzi

Mtendaji Mkuu wa Tarura, Victor Seif

Muktasari:

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), imeanza mkakati wa kutengeneza barabara na madaraja kwa kutumia teknolojia ya mawe ambayo inaokoa gharama kwa asilimia 50.

Dodoma. Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), imeanza mkakati wa kutengeneza barabara na madaraja kwa kutumia teknolojia yam awe ambayo inaokoa gharama kwa asilimia 50.

 Hayo yamesemwa leo Alhamis Septemba 22, 2022 na Mtendaji Mkuu wa Tarura, Victor Seif wakati wa siku ya wahandisi nchini.

Amesema Tarura imeanza mkakati wa kutumia teknolojia ya ujenzi wa madaraja na barabara kwa kutumia mawe badala ya kutumia nondo na zege.

“Teknolojia ni mojawapo ya mkakati wetu wa Tarura kujenga madaraja na barabara na kutumia vifaa ambavyo viko katika eneo ambalo ujenzi huo,”amesema.

Seif amesema uzuri wa teknolojia hiyo ni bei inakuwa chini kwasababu vifaa vinavyopatikana katika maeneo ya kazi.

Amesema wameshajenga mawe katika madaraja zaidi ya 72 mkoani Kigoma kwa Sh1.4 na kwamba ujenzi huo unaendelea kwenye mikoa Mwanza, Iringa na Singida.

Amesema ujenzi huo ni nafuu kwasababu vifaa vinapatikana katika eneo la ujenzi na kwamba mkakati wao ni kuangalia maeneo yote yenye mawe.

Seif amesema kwa kushirikiana na Serikali ya Ubeligiji wanafanya mafunzo mkoani Kigoma kwa mafundi kutoka maeneo mengine ya Kilimanjaro, Iringa, Singida.

“Gharama ni zaidi ya 50 zinapungua, ukitumia zege na nondo utakuta ni gharama zaidi ya mara mbili kama utakijenga kwa kutumia zege na nondo. Teknolojia hii wanatumia saruji, mchanga na mawe,”amesema.

Hata hivyo, amesema mawe yanayotumika katika ujenzi wa barabara yanatakiwa yawe na ubora na yachongwe na kupangwa vizuri ili iweze kukamilika.

Mmoja wa wahandisi kutoka Tarura, Phares Ngeleja amesema wanampango wa kuendesha mafunzo kwa wahandisi ili waifahamu teknolojia hiyo maana ndio watakuwa wanasimamia.

“Kuanzia Februari mwaka huu, tutakuwa na mafunzo yatakayofanyiwa na wenzetu wabeligiji, tutaanzia mikoa kadhaa na baadaye tutasambaa nchini,”amesema.