Tasac yawatoa hofu wananchi usalama wa MV Chato

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Wakazi wa Manispaa ya Musoma na mji wa Kinesi wilayani Rorya wametakiwa kuondoa hofu kuhusu kivuko cha MV Chato kwa sababu ni salama.

Musoma. Shirika la Uwakali wa Meli Tanzania (Tasac) imewatoa hofu wananchi kuhusu usalama wa wa kivuko cha MV Chato kinachosafirisha abiria na mizigo kati ya Manispaa ya Musoma na mji wa Kinesi wilayani Rorya.

Akizungumza mjini Musoma leo Jumatano Machi 8, 2023, wakati wa mafunzo ya wadau wa serikali kuhusu sheria ya usafiri majini, Ofisa Mfawidhi wa Tasac Mkoa wa Mara, Abeid Mwanga amesema Tasac imefanya ukaguzi wa chombo hicho na kujiridhisha na usalama wake baada ya kupokea malalamiko na taarifa za wananchi kuhofia usalama wake.

"Tumefanya ukaguzi kwanza kwa sababu ni moja ya wajibu na majukumu yetu; lakini pia kutokana na malalamiko ya wananchi kuhusu usalama wa chombo. Kiujumla, tumebaini MV Chato iko salama licha ya mapufungu madogo ambayo tayari tumetoa melekezo ya namna ya kuyarekebisha kwa Temesa," amesema Abeid

Kivuto cha MV Chato kinatoa huduma ya kusafirisha abiria kati ya Mji wa Musoma na Kinesi baada ya kivuko cha awali cha MV Musoma kilichokuwa kikitoa huduma eneo hilo kupelekwa kwenye matengenezo makubwa tangu mwaka jana.

Mwanasheria mwandamizi wa Tasac, Asma Mohamed amewaomba wananchi kutoa taarifa kwa ama viongozi na watendaji Tasac au viongozi wa Serikali katika maeneo yao pindi wanapobaini kasoro za kiusalama na ubora kwenye vyombo vya usafirishaji majini.

“Kwa ajili ya usalama na tahadhari wakati wa majanga, ni vema kila abiria ahakikishe anavaa jaketi okozi kila apoingia kwenye vyombo vya usafirishaji majini kabla ya kuanza safari,” amesema Asma

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Halfan Haule amesema Serikali itaendelea kusimamia sheria na kanuni za usafirishaji salama mjini huku akiwasihi wananchi kuzingatia sheria na kutoa taarifa pindi wanapobaini ukiukwaji wa sheria.