Tatizo la kichwa kujaa maji huwakumba watu wazima pia

Elizabeth Mwitakubi (31) akiwa na mtoto wake aliyezaliwa na kichwa kikubwa wakati wa mahojiano na Mwananchi. Picha na Saada Amir

Muktasari:

  • Kwa binadamu umuhimu wa maji unadhihirishwa na ukweli kwamba asilimia 75 ya mwili unaundwa na maji huku asilimia 25 inayosalia inaundwa na mifupa, nyama na mishipa.

Mwanza. Maji ni Uhai! Huo ni usemi maarufu uliyozoeleka kuelezea umuhimu wa maji kwa binadamu, mimea na wanyama.

Kwa binadamu umuhimu wa maji unadhihirishwa na ukweli kwamba asilimia 75 ya mwili unaundwa na maji huku asilimia 25 inayosalia inaundwa na mifupa, nyama na mishipa.

Pamoja na ukweli wa umuhimu wa maji mwilini, wataalamu wa afya wanaonya kuwa wingi wa maji kupitiliza kwenye mwili wa binadamu unaweza kusababisha madhara.

Kwa mujibu wa Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mgongo kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, Dk Gerald Mayaya anataja moja ya madhara yanayoweza kutokea kutokana na maji kupitiliza ni tatizo la kichwa kikubwa ( kujaa maji pasipo kawaida kichwani).

Dk Mayaya anasema tatizo la kichwa kujaa maji pasipo kawaida umkuta mwanadamu yeyote, awe mtoto ama mkubwa kwakuwa katika hali ya kawaida kila mtu ana maji kichwani (kwenye ubongo).

“Kila siku kuna kiasi kama mills 400 mpaka 500 (kipimo cha chupa ya soda) zinazalishwa kila siku kwenye ubongo wa mwanadamu, Pamoja na kwamba kiasi hicho kinazalishwa lakini kinachotakiwa kubaki ni  mills 100 mpaka 150 peke yake kila siku, kile kiasi kingine kinachobaki (milss 300 mpaka 350) kinakwenda kuingia kwenye ubongo kinafyonzwa kisha kinaingia kwenye mfumo wa damu. Hilo ni zoezi la kila siku,”anasema

Anasema tatizo hilo hata watu wazima hulipata ila wao vichwa vyao haviwi vikubwa tofauti na watoto ambao wakipata tatizo hilo vichwa vyao hutanuka na kuwa vikubwa. 

“Kwenye kichwa kuna mifupa nane ambayo inafunika ubongo, wakati mtoto anapozaliwa inakuwa haijafunga lakini mtoto anapofikisha miaka minne hadi mitano zinajifunga. Kwahiyo ikiisha funga maana yake kichwa hakiwezi kuwa kikubwa kwa sababu tayari ile mifupa ambayo ilikuwa haijafunga imeshafunga,ndio mana watu wazima wakipata tatizo hilo vichwa vyao haviwi vikubwa ila wanapata maumivu makali ambayo uweza kupona baada ya kupata matibabu,”anasema

Dk Mayaya anasema kwa mwezi hospitali ya Bugando hufanyia watu wazima watatu hadi wanne upasuaji kutokana na kichwaa kujaa maji pasipo kawaida na wakati mwingine hufanyia watu wenye umri hadi miaka 60 ama 70.

Kwanini mtu anapata tatizo la kichwa kujaa maji pasipo kawaida(Kichwa kikubwa)?

Dk Mayaya anasema sababu zimegawanyika mara mbili, akitaja sababu ya kuzaliwa na tatizo hilo na kulipata baada ya kuzaliwa.

“Ili uweze kupata tatizo la kichwa kujaa maji kuliko kawaida maana yake uzalishaji wa maji kwenye ubongo uwe mwingi badala ya kuzalisha mills 400 mpaka 500 kwa siku mtu azalishe mills hata 1,000 na kuendelea kwa siku, hivyo hata zikiingia kwenye mfumo wa kawaida bado utafeli kuyanyonya hayo maji,”anasema

Anasema uzalishaji wa maji ukiwa mwingi ndiyo sababu kichwa kinakuwa na maji kuliko kawaida ama uzalishaji unaweza kuwa ni ulele lakini ile sehemu inayotakiwa ifyonze yale maji unakuwa imeziba au njia ambazo maji yanatiririka  zinakuwa kuna sehemu zimeziba hivyo kusababisha maji yashindwe kutiririka. 

Sababu za mtoto kuzaliwa na kichwa kikubwa

kuziba kwa mrija wa kupitishia maji kwenye ubongo (Aqueduct Stenosis) ni moja ya sababu inayoweza kusababisha mtoto kuwa na kichwa kikubwa.

Sababu nyingine inayotajwa na Daktari huyo bingwa ni kuzaliwa bila njia ya kupitishia maji (Agenesis) hivyo kufanya maji yasifike mwisho pamoja na mtoto kuzaliwa na mgongo wazi.

“Kati ya watoto wanaozaliwa na mgongo wazi asilimia 70 mpaka 80 wanapata tatizo hilo,”anasema na kuongeza

“Sababu nyingine ni mama kuwa na maambukizi mbalimbali kama vile kaswende wakati wa ujauzito, nakupelekea kumuambukiza  mtoto akiwa tumboni mwake, mtoto akizaliwa na infection (maambukizi) maana yake kwenye ubongo kuna kuwa na makovu kwahiyo zile sehemu ambazo zinafyonza maji unakuta mara nyingi zina makovu kwahiyo maji yatazalishwa lakini hayawezi kutiririka,”anasema

Dk Mayaya anasema baadhi ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda pia wanaweza kupata tatizo hilo kwakuwa baadhi yao damu huvujia kwenye ubongo.

“Njia za maji kule ndani zipo nne maji yanazalishwa kulia na Kushoto alafu yanapita kwenye njia moja kisha kwenye njia nyingine nyembamba kwahiyo unakuta mtoto anazaliwa kameziba kale ka njia (Aqueduct Stenosisi),”anasema

Sababu zisizo zakuzaliwa na tatizo hilo

“watoto wote unaowaona wana vichwa vikubwa (vilivyojaa maji) sio wote wamezaliwa na tatizo hilo, wengi wanapata baada ya kuzaliwa na ndio kiasi kikubwa,”anasema Dk Mayaya

Ametaja sababu zinazopelekea watoto hao kupata tatizo hilo ni kuziba kwa mrija wa kupitisha maji, maambukizi kama vile kwenye uti wa mgongo au homa kali zinazoweza kupelekea kichwa kujaa maji, ajali na damu kuvujia kwenye mfumo wa njia ya maji, uvimbe kwenye ubongo ambao hupelekea kuziba kwa njia hizo.

Matibabu.

Dk Mayaya anasema,“Tunafanya upasuaji wa aina tatu lakini uwa tunafanya kulingana na sababu iliyosababisha maji kujaa, kama mgonjwa amejaa kwa sababu ya uvimbe asilimia 70 ya wagonjwa ambao tunawatolea uvimbe ile njia inaachia na maji yanarudi kwenye mzunguko wake wa kawaida,”

Anasema kwa wale wenye tatizo la maji kuzalishwa kuliko kawaida huwa wanayatengenezea njia“Wale ambao unakuta njia zote zipo sawa ila shida ni maji kuzalishwa mengi kuliko kawaida uwa tunawawekea mpira ambao unaenda kwenye njia za maji alafu yale maji tunayapeleka ndani ya tumbo (abdomen),”

Anasemaupasuaji mwingine ni wa wale ambao njia za maji zimeziba japo hawana uvimbe, huwa wanayatafutia njia nyingine kwa kutumia mtambo maalum ambao wenyewe hawawekewi mpira.

Sababu za upasuaji kufeli.

Ametaja sababu zinazoweza kusababisha upasuaji kutofanikiwa ni kucheleweshwa kwa wagonjwa kupata matibabu, baadhi ya watoto wanaowekewa mipira ya kufyonza maji kupata maambukizi yanayoweza kupelekea kutunga kwa usaha, kuziba kwa mpira hivyo kutofanya kazi ya kufyonza maji na wakati mwingine mpira kutoa maji kidogo kuliko yanayozalishwa na wakati mwingine mpira kuhama.

“Upasuaji ili ufanikiwe unategemea sana mgonjwa amewahi hospitali kwa kiasi gani, upasuaji ukifanikiwa mara nyingi inategemea amefanyiwa kwa wakati gani, na ubongo umeathirika kwa kiasi gani,”anasema

“Mtoto anapoonesha zile dalili mwanzoni kabla hajaathirika sana akifanyiwa upasuaji unafanikiwa lakini kuna wale unakuta tayari kichwa kimeshakuwa kikubwa sana kwahiyo kinachotokea ni ubongo unakuwa umeathirika maana njia za maji zinakuwa zimepanuka kupita kiasi na kuubana ubongo (kikawaida kuna sentimita tano mpaka sita kutoka kwenye njia za maji na ubongo) lakini unakuta mgonjwa mwingine amebaki na sentimita moja hivyo ubongo unakuwa umebanwa na kusinyaa na sehemu zingine inakuwa maji tu,”ameongeza Dk Mayaya

Anasema watu wazima wenye tatizo hilo mara nyingi wanawahi kupata tiba kwa sababu maumivu ya kichwa yanakuwa makali sana kutokana na  fuvu kutotanuka na wakifanyiwa upasuaji tu maumivu yanaisha na wanakuwa katika hali ya kawaida lakini watoto wengi wanachelewa kupata tiba kwa sababu ubongo hauna maumivu ili mradi ile mifupa yake inakubali kutanuka ubongo unakuwa unakandamizwa na kichwa kutanuka kuwa kikubwa.

Muathirika wa tatizo la kichwa kikubwa

Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, Elizabeth Mwitakubi (31) mama wa watoto watatu aliyejifungua mtoto mwenye tatizo la maji kuzalishwa kwenye ubongo kuliko kawaida (kichwa kikubwa) anasema mtoto wake wa tatu mwenye miezi minne sasa aligundulika na tatizo hilo wiki moja baada ya kuzaliwa.

“Baada ya wiki moja kupita tangu nimejifungua, muuguzi wa Afya Hospitali ya Katoro Geita akaniambia mtoto wangu ana tatizo la kichwa kikubwa inabidi niende hospitali ya Bugando kwa ajili ya matibabu,”anasema

Elizabeth anasema kutokana na hali ya mtoto wake anakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo fedha za matibabu ya mtoto wake baada ya mumewake kumkimbia.

“Mumewangu nilivyomwambia  mtoto kazaliwa na kichwa kikubwa na anatakiwa matibabu alinipa Sh100,000 kwa ajili ya matibabu ikabaki Sh100, 000, nilivyomuomba ela iliyobaki aliniambia amechoka kila siku matibabu ya mtoto hayaishi nakudai amefika mwisho nifanye ninavyovijua mwenyewe maana yeye amechoka,”

Anasema mtoto wake huyo ameshafanyiwa upasuaji mara mbili katika hospitali ya Bugando bila mafanikio huku upasuaji wa mara ya tatu ukitarajiwa kufanyika wakati wowote atakapo pata fedha ya kipimo cha CT Scan Sh200,000.

“Upasuaji wa pili baada ya kukimbiwa na mumewangu nilimwambia dada yangu mkubwa akanisaidia saidia, huu wa tatu kwakweli sina chochote naomba hatakayeguswa anisaidie pesa kwa ajili ya matibabu ya mtoto wangu pamoja na mtaji wa biashara ili nitakapomaliza matibabu nifanye biashara tuweze kujikimu,”

Mama huyo anasema awali alikuwa akifanya biashara ya makapi ya dhahabu (felo) migodini huko Geita aliyokuwa akiyachakata nakupata fedha ya kujikimu si chini ya Sh200,000 kulingana na dhahabu anayoipata baada ya kuchakata na kuosha makapi hayo.

“Nina changamoto za maisha hapa hata ela za matumizi zinanisumbua, kwakuwa nilikuwa nafanya biashara lakini sasa hivi sifanyi kutokana na hii changamoto ya mtoto wangu, hata chumba nilichokuwa naishi Katoro sina chochote cha kumlipa mwenye nyumba naye ananidai Sh180,000 kuanzia mwezi wa 11,”anasema

Elizabeth ambaye kwa sasa anaishi katika kituo cha nyumba ya matumaini (House of hope) kinachowasaidia watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi Jijini Mwanza.

Kituo cha malazi kwa watoto wenye tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi

Meneja wa kituo cha nyumba ya matumaini Kilichopo Nyegezi Jijini Mwanza, Getruda Butondo anasema kituo hicho kinapokea watoto wenye kichwa kikubwa na migongo wazi  kutoka sehemu mbalimbali nchini akitaja mkoa wa Mwanza, Tabora, Biharamulo, Kigoma na Musoma kuwa maeneo wanayopokea watoto wengi wenye shida hiyo.

“Changamoto tunayoipata nikupokea wazazi wengi wasio na uwezo wa kumuhudumia mtoto, wanawake kutelekezwa na wenza wao hivyo shirika linachukua majukumu ya kuwasaidia ili kupata matibabu, kwa kuwapatia malazi na upasuaji lakini mama atawajibika kununua dawa na vipimo”

Kwa atakayeguswa kumchangia Elizabeth awasiliane naye kupitia namba 0783089343.