Tawa yachunguza nyara zilizokamatwa Australia

Dar es Salaam. Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), imekiri ‘mzigo’ wenye nyara za Serikali ambao umekamatwa nchini Australia, umetoka Tanzania na kwamba ulitumwa kama kifurushi, huku ikisema kibali kilichotumika ni kinyume na sheria.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Ijumaa 8, 2023; Vicky Kamata, Ofisa Mhifadhi Mkuu-Uhusiano kwa Umma wa mamlaka hiyo, amezitaja nyara hizo ni pamoja na ngozi ya chui na fuvu la simba, na kwamba Tawa imeaanza uchunguzi kuhusu tukio hilo.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa simba na chui ni wanyamapori wanaolindwa na Mkataba wa Kimataifa wa Biashara ya Wanyamapori na Mimea iliyo hatarini kutoweka (Cites), ambao Tanzania iliridhia tangu mwaka 1980.
“Hivyo, usafirishaji wa nyara hizo uhitaji kibali cha Cites..kwa kuzingatia mkataba huu ambao Tanzania ni mwanachama, idara ya wanyamapori ambao ndio wasimamizi wa mkataba wa cites nchini, tayari imeanza uchunguzi juu tukio hilo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza;
“Tayari idara hiyo imeshaiandikia barua mamlaka ya usimamizi wa mkataba wa Cites nchini Australia, ili kupata taarifa zaidi kuhusu nyara hizo, vibali vilivyotumika kuzisafirisha na hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Australia ili Tanzania iweze kuchukua hatua stahiki itakapobainika uwepo wa ukiukwaji wa sheria na kanuni.”
Awali, Tawa imeeleza kuwa hivi karibuni kwenye mtandao wa kijamii wa Tik Tok, kulionekana video fupi, ikiwaonyesha maofisa usalama wanaohusika na masuala ya baiolojia nchini Australia, wakichunguza picha za X-Ray ya mzigo wa mazulia unaodaiwa kutokea Tanzania.
Hata hivyo, baada ya kufunguliwa kwa mzigo huo, kulionekana kuwa na ngozi ya chui iliyotengenezwa kama zulia na fuvu la simba lililoungana na ngozi
Taarifa ya Kamata, imeeleza kuwa Tawa imechukulia video hiyo kwa uzito mkubwa kwa kuzingatia kuwa ndio taasisi iliyopewa dhamana ya utoaji wa vibali vya usafirishaji nyara nje ya nchi ikiwemo nyara zilizotengenezwa.
Kwa mujibu wa Tawa, nyara hizo zilitumwa kama kifurushi kwenda nchini Australia, na kwamba ziliambatanishwa nan a baadhi ya nyaraka kama kibali cha kusafirisha nyara nje ya nchi, ambacho kwa mujibu wa sheria kibali hicho hakiwezi kutumika kusafirisha nyara za wanyamapori hao.