Tax miongoni mwa wanawake wa nguvu

Muktasari:

Mbunge wa Kuteuliwa, Dk Stergomena Tax ameweka rekodi ya kuwa mmoja kati ya wanawake saba wanaoongoza wizara nyeti katika Serikali ya awamu ya sita.

  





Dar es Salaam. Mbunge wa Kuteuliwa, Dk Stergomena Tax ameweka rekodi ya kuwa mmoja kati ya wanawake saba wanaoongoza wizara nyeti katika Serikali ya awamu ya sita.

Septemba 10, Dk Tax aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mbunge na siku mbili baadaye akateuliwa kuwa waziri wa Ulinzi na JKT akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Elias Kwandikwa aliyefariki Agosti 2.

Mawaziri wengine wanawake wanaoongoza wizara nyeti ni Profesa Joyce Ndalichako (Elimu), Dk Doroth Gwajima (Afya) na Jenista Mhagama (Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge).

Wengine ni Ummy Mwalimu (Ofisi ya Rais, Tamisemi), Balozi Liberata Mulamula (Mambo ya Nje) na Dk Ashatu Kijaji (Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari).

Dk Tax ambaye alizaliwa mwaka 1960, kabla hajaitumikia SADC kwa miaka minane kama mtendaji mkuu, alikuwa katibu mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Aliteuliwa kushika nafasi hiyo mwaka 2008 na Rais, Jakaya Kikwete.

Kabla ya hapo, alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji kuazia kwama 2006.

Mama huyo wa watoto wawili, aliwahikuwa ofisa mtendaji mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Ubora (BRU), katika Mpango wa Uimarishaji wa Maendeleo ya Biashara Tanzania (BEST), chini ya Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji.

Alishakuwa mratibu na mshauri katika Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamiii (ESRF) na aliwahi kuwa kuhudumu katika Wizara ya Fedha kwa nafasi mbalimbali, ikiwemo ofisa mkuu wa dawati la Benki ya Dunia na pia msimamizi wa dawati la Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Wa kwanza mwanamke

Kwa wadhifa huo mpya, Dk Tax ni mwanamke kwanza kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa tangu taifa lilipopata uhuru mwaka 1961.

Dk Tax ameteuliwa kushika nafasi hiyo zikiwa zimepita siku chache tangu alipomaliza muda wake kama Katibu Mtendaji SADC).

Jana, aliapishwa sambamba na mawaziri wengine ambao waliteuliwa na Rais Samia Ikulu jijini Dodoma na kuweka rekodi ya pili ya kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza wizara hiyo nyeti baada ya ile ya kuongoza SADC.

Tangu uhuru wake mwaka 1961, Wizara ya Ulinzi imepata kuongozwa na wanaume 15 kabla ya jana kuongozwa na mwanamke, jambo ambalo lilikuwa kama utamaduni ambao Rais Samia ameamua kuuvunja.

“Katika mabadiliko haya nimeamua kuvunja taboo (mwiko) ya muda mrefu ya kwamba wizara ya ulinzi lazima akae mwanaume mwenye misuli yake, lakini kazi ya waziri wa kwenye ile wizara siyo kupiga mzinga au kushika bunduki, ni mainly coordination, kusimamia sera na utawala wa wizara,” “Nimempeleka huyo siyo kwa sababu tu ya kuvunja hiyo taboo, lakini kwa sababu ya upeo wake mkubwa aliopata akiwa SADC. Kipindi chote tukienda SADC alikuwa anasimamia vema mambo yote ya usalama ndani ya region (kanda),” alisema Rais Samia.

Akizungumzia uteuzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema amefurahishwa na uteuzi huo kwa sababu unatoa ujumbe kwamba kazi yoyote inaweza kufanywa na yeyote.

“Tumefurahia uteuzi huo na ni matumaini yangu kwamba Rais ataendelea kuwapa imani wanawake wengi zaidi katika nafasi nyeti,” alisema.