TCRA: Leteni mapendekezo kuboresha kanuni za maudhui mtandaoni

Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Dk Philip Filikunjombe akiwasilisha mada ya kuhusu sheria ya maudhui mitandaoni kwenye semina iliyoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) mjini Morogoro leo. Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

  • Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka wadau wenye mapendekezo yatakayosaidia kuboresha mabadiliko ya kanuni za maudhui mtandaoni mwaka 2018 kuyawasilisha ili yafanyiwe kazi.

 Morogoro. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka wadau wenye mapendekezo yatakayosaidia kuboresha mabadiliko ya kanuni za maudhui mtandaoni mwaka 2018 kuyawasilisha ili yafanyiwe kazi.

Mkuu wa Kitengo cha Sheria cha TCRA, Dk Philip Filikunjombe amesema hayo leo Jumanne Mei 11, 2021 katika semina ya waandishi wa habari za mitandaoni kwa ajili ya kuwajengea uwezo.

“Mitandao ya kijamii imekua na nguvu sana duniani kwa sababu inapasha habari kwa haraka zaidi na popote ulipo ukiwa na kifaa sahihi cha kielektroniki, mnakumbuka miaka ya nyuma watu walikuwa wakiwahi nyumbani kuangalia na kusikiliza taarifa za habari, sasa hivi mambo yamebadilika ni muhimu kuwepo na usumamizi,” amesema Dk Filikunjombe

Amesema kupitia marejeo yatakayofanywa na Serikali kuhusu kanuni za maudhui mtandaoni, wadau wanakaribishwa kutoa mapendekezo ya vifungu wanavyodhani sio rafiki katika utekelezaji wa majukumu yao.

Dk Filikunjombe amesema msingi wa kuwepo kanuni hizo ni kuhakikisha kunakuwa na uwajibikaji ili kudhibiti maudhui yasiyofaa na mhusika achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria na kuwalinda watu wengine.