TCRA yapiga marufuku maudhui tata yanayogusa imani za kidini

Moshi. Uamuzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupiga marufuku urushaji wa maudhui ya kufikirika yanayoleta utata kuhusu imani za kidini kwenye jamii, umewaibua wasomi na wanahabari wakisema hatua

Katika taarifa yake, TCRA imesema mambo yanayohusu imani za dini ni masuala binafsi ya mtu hivyo mahali sahihi ni kwenye nyumba za ibada na si kwenye vyombo vya habari na utangazaji kama televisheni, redio na mitandao ya kijamii.

Ingawa TCRA haikutaja maudhui hayo yalirushwa kwenye radio au televisheni za kawaida au zile za mtandaoni, lakini siku za karibuni baadhi ya viongozi wa kiroho wamesikika wakitoa kauli zenye utata kwa jamii.

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo ni miongoni mwa walipaza sauti kupinga maudhui hayo kuwa baadhi yanalenga kuwavuruga waumini ili kupata umaarufu, mali na fedha.

Hata hivyo, maudhui mengi ya aina hiyo yamekuwa yakirushwa kupitia redio na televisheni za mtandaoni na makundi ya kijamii hivyo kuumiza imani za waumini hususan Wakristo kutokana na kupingana na Biblia.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa juzi na mkurugenzi wake mkuu, Dk Jabir Bakari mamlaka hiyo imesema vyombo vya habari na utangazaji vinawajibika kufuata misingi na maadili ya taaluma zao kwa kutoa taarifa zilizofanyiwa uchambuzi za kuaminika na za kweli.

Mamlaka hiyo imesema Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta za mwaka 2018 na zile za mwaka 2022 zinaelekeza watoa huduma ya utangazaji kujiepusha na maudhui ya upotoshaji na yanayogusa imani za watu.

Lakini katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na mfululizo wa taarifa fupi zilizo kwenye mfumo wa video zinazozungumzia mawazo fikirika yanayogusa imani hizo jambo ambalo si sahihi kufanywa na vyombo hivyo.

Mbali na kukemea habari zenye maudhui hayo, TCRA pia imeonya kuwa itachukua hatua kali za kisheria kwa chombo chochote cha utangazaji kitakachobainika kuendelea kurusha taarifa zenye maudhui hayo ya kidini.

Wakati TCRA ikikunjua makucha yake, kumekuwa na kilio cha muda mrefu kuwa baadhi ya wahubiri wamekuwa wakitumia televisheni, redio na mitandao ya kijamii kurusha mahuburi yanayofanya mzaha na kuumiza imani za wengine.


Walichokisema wanataaluma

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St Augustine (SAUT) cha Mwanza, Dk Kanael Kaale alisema uamuzi huo wa TCRA ni sahihi lakini umechelewa kwa kuwa matangazo yenye maudhui hayo yako katika vyombo hivyo kwa karibu miaka mitano sasa.

“Kutoandika habari za kufikirika hiyo ni sawa kwa sababu inasababisha watu wengi kushindwa kujikita kwenye vitu vya maendeleo na vingine vinaweza kuchukuliwa na watu wasio na uwezo wa kutafakari kuwa ndio ukweli. Ni lazima sheria isikae upande mmoja tu, kama ni kuzuia izuie kweli na kuchukua hatua,” alisema Dk Kaale na kuongeza kwamba:

“Maudhui yaliyoko kule ni ya hatari na yanaharibu saikolojia za watu, yanaleta chuki na yanapandikiza mambo ambayo hayana maadili mema. Hayo maudhui ya kufikirika na yanayogusa imani za watu yasirushwe. Serikali ijipange upya kwa sababu hao wenye hiyo mitandao ya dini wana subscribers (wafuasi) wengi kuliko mainstream media (vyombo vya habari vya kitaifa) na kukua kwa teknolojia ya habari wajipange vizuri kweli kweli.”

Kwa upande wake, Mhadhiri Msaidizi wa Idara ya Habari na Ukutubi ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Vincent Mpepo alisema masuala ya weledi yana changamoto katika vyombo vya mitandaoni.

“Kuna shida ya kuingiliwa kwa tasnia ya habari hususan vyombo vya habari vya mitandaoni. Serikali imefanya vyema kutoa tamko lakini imechelewa kwa kuwa kuna changamoto za kimaadili za muda mrefu hazijafanyiwa kazi,” alisema Mpepo.

Mhadhiri huyo alisema ni jukumu la wanahabari kupima na kuchagua aina ya watu wanaowatumia kama vyanzo vya habari katika vipindi vyao kwani baadhi ya vituo vina maudhui yaliyo kinyume na maadili.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa-Tan), Salome Kitomari alisema TCRA imefanya vyema kuzuia aina hiyo ya maudhui kwa kuwa yanaibua sintofahamu kwa wananchi.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo aliitaka TCRA kufuatilia watu binafsi ambao si waandishi wa habari wanaotengeneza maudhui na kuyasambaza hivyo kuikwaza jamii.

“Ni muhimu Serikali ije na mkakati wa kukabili maudhui na itoe elimu kwa umma ili kupunguza maudhui ya uongo ambayo hayatengenezwi na wanahabari bali kila mwenye mtandao wake. Hii ni hatari,” alisema Salome.

Neville Meena, mhariri mtendaji wa gazeti la Sama na mjumbe wa kamati tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), alisema tangazo la TCRA lina shida kwa kutoeleza ni chombo gani kilirusha maudhui hayo.

“Kama wameona jambo kwenye chombo fulani na wana mandate (mamlaka) ya kisheria walitakiwa wakionye ili iwe fundisho kwa wengine lakini hivi walivyofanya kitajishuku pasipo kuwa na uhakika,” alisema Meena.

Katibu Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa Kilimanjaro (Mecki), Nakajumo James alisema ni uamuzi sahihi kwani eneo waliloligusa ni kama vile halina mwenyewe kiasi cha kuruhusu maudhui ya upotoshaji.