TEC watoa neno kuelekea siku ya uhuru
Muktasari:
- Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limewataka wananchi kujiandaa kwa ajili ya chaguzi zijazo, ukiwamo wa mwakani wa Serikali za mitaa na mkuu wa mwaka 2025.
Mbeya. Wakati Watanzania wakielekea kuadhimisha siku ya uhuru, Desemba 9, 2023 Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), limewataka kuendelea kudumisha amani, upendo na mshikamano.
Akizungumza leo Desemba 6, 2023 jijini hapa, Rais wa TEC na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya, Gervas Nyaisonga amesema hayo ni tunu iliyoachwa na waasisi wa Taifa hili, hayati Julius Nyerere na Abeid Amani Karume.
Amesema viongozi na waasisi waliweka mfumo imara ikiwa ni pamoja na kupokezana nafasi za uongozi, lakini walikataa na kupinga matabaka ya udini na ukabila.
"Waasisi wa Taifa letu waliacha misingi imara, walikataa matabaka kama udini na ukabila, wakaweka kupishana nafasi za uongozi. Tulijipambanua kushirikiana na mataifa mengine lakini kulinda rasilimali za nchi," amesema.
Askofu Nyaisonga amesema, "Nchi yetu imepitia kipindi kigumu kiuchumi, hivyo tuendeleze umoja na kupigania masilahi ya Taifa, kwani tunayo lugha inayotuunganisha ya Kiswahili iliyowekwa na waasisi hao.
Mbali ya hilo, amewaomba wananchi kujiandaa na uchaguzi ujao kuanzia wa Serikali za mitaa mwakani na uchaguzi mkuu wa 2025.
Amewaomba kutuliza akili ili kumpata kiongozi bora mwenye uelekeo.