Tembo na nyati waleta taharuki Namtumbo

Tembo na nyati waleta taharuki Namtumbo

Muktasari:

  • Mbunge wa Namtumbo Nchini Tanzania (CCM) Vita Kawawa amelalamikia tembo na nyati kuvamia mashamba na makazi na kuleta tahariki

Dodoma. Mbunge wa Namtumbo nchini Tanzania (CCM) Vita Kawawa amesema ongezeko la wanyamapori katika hifadhi ya Taifa ya Selous limesababisha tembo na nyati kuvamia mashamba pamoja na makazi ya wanavijiji na kuleta taharuki.
Akiuliza swali bungeni leo Jumatatu Februari 8 2021, Kawawa amehoji Serikali inaweza kuwarudisha wanyama hao porini mbali zaidi na wananchi.
Akijibu Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema Wizara yake imeandaa na inatekeleza Mkakati wa Kitaifa wa kusimamia utatuzi wa migongano baina ya binadamu na wanyamapori.
Pia, amesema wizara hiyo inaendelea kukamilisha utaratibu wa kuweka alama katika shoroba na mapito ya wanyamapori ili kuimarisha uhifadhi wake na kuendelea kufanya utafiti na kueneza matumizi ya mbinu mbadala za kujikinga na wanyamapori waharibifu hasa tembo.
“Baadhi ya mbinu hizo ni matumizi ya pilipili, mafuta machafu (oil), mizinga ya nyuki na kutoa mafunzo kwa askari wa wanyamapori wa vijiji,”amesema.
Amesema wizara imekuwa ikiendelea kufanya doria za msako kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu.
Amesema katika kipindi cha Julai hadi Disemba, 2020 zilifanyika doria za msako zenye jumla ya watu 133 katika vijiji vya wilaya ya Namtumbo, kutoa elimu kwa wananchi juu ya mbinu za kujikinga na wanyamapori wakali na waharibifu ambapo jumla ya wananchi 2,303 walipata elimu katika vijiji 42 vya Wilaya za Namtumbo na Tunduru.
Nyingine ni kuimarisha vituo maalum vya doria za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu katika Kanda za Kalulu na Likuyu-Sekamaganga.