Temdo kutengeneza mashine za kuzalisha sukari

Temdo kutengeneza mashine za kuzalisha sukari

Muktasari:

  • Wakulima wadogo na binafsi wa miwa nchini Tanzania wataondokana na changamoto ya kukosa masoko ya bidhaa zao baada ya taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo nchini (Temdo) kutengeneza mitambo midogo yenye uwezo wa kuzalisha tani moja hadi 10 za sukari kwa saa moja.


Arusha. Wakulima wadogo na binafsi wa miwa nchini wataondokana na changamoto ya kukosa masoko ya bidhaa zao baada ya taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo nchini (Temdo) kutengeneza mitambo midogo yenye uwezo wa kuzalisha tani moja hadi 10 za sukari kwa saa moja.

Mkurugenzi Mkuu wa Temdo), Profesa Frederick Kahimba amesema hayo leo Jumanne Agosti 2021  alipokua akitoa taarifa ya taasisi  hiyo kwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo wakati akizindua bodi ya Wakurugenzi iliyoteuliwa mwezi Mei mwaka huu kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Profesa Kahimba amesema mara nyingi viwanda huwa vinavuna kwanza miwa yao kisha uangalia iwapo wanahitaji miwa zaidi kutoka kwa wakulima binafsi ambayo mara nyingi ni sehemu ndogo tu hivyo wakulima wengi wamekua wakikosa soko.

“Katika kipindi cha mwaka 2021/2022 tutakua tumetengeneza mashine mbili za mfano ambazo tutazipeleka kwa wakulima ambao watatupa mapendekezo ya mwisho ambayo tutayazingatia kwenye utengenezaji wa mashine zaidi,” amesema Profesa Kahimba

Amesema utengenezaji wa mashine hizo utakua mkombozi kwa wakulima wa miwa nchini ambao wataondokana na utegemezi wa kuuza miwa yao viwandani na kuanza kuchakata miwa yao kwaajili ya kuzalisha sukari ambayo kwa nyakati tofauti nchi imekua ikipata upungufu.

Profesa Mkumbo akizindua bodi hiyo ambayo Mwenyekiti wake ni Dk Richard Masika ameiagiza ijielekeze kufanya tafiti zinazolenga kuzalisha fedha kupitia utafiti na maendeleo ili kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka serikalini.

“Zipo taasisi za serikali ambazo tunapaswa kuzipa fedha za ruzuku lakini sio Temdo, mnao uwezo wa kuendelea na majukumu yenu ya msingi lakini kuingiza kipato kwa kujibadilisha na kuwa taasisi ya umma inayofanya biashara,” amesema Profesa Mkumbo