Tisa kortini kwa kumchafua Ruto

Thursday August 04 2022
KENYA PIC

Mgombea urais wa United Democratic Alliance (UDA), William Ruto

By Mwandishi Wetu

Wanafunzi tisa wa Chuo Kikuu cha Moi wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuhusika na usambazaji wa ujumbe wa chuki dhidi ya mgombea urais wa Kenya Kwanza ambaye ni Naibu Rais, William Ruto kupitia makundi sogozi (WhatsApp).

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Eldoret, Onkoba Mogire ameamuru wanafunzi hao washikiliwe katika Kituo cha Polisi cha Langas kwa siku tatu, huku uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili ukiendelea.

Kesi ya wanafunzi hao itatajwa tena Agosti 5, mwaka huu.


Ruto akasirishwa

Wakati uchunguzi wa shauri hilo ukiendelea, Ruto amejitokeza hadharani kulaani uwepo wa vipeperushi vyenye ujumbe wa kumchafua kwenye eneo la Eldoreti.

Advertisement

Ruto amemshutumu Rais Uhuru Kenyatta kwa kumuongelea vibaya kwenye kampeni za Azimio la Umoja.

Ruto amewashukia maofisa wa Serikali kuhusika na usambazaji wa vipeperushi hivyo kwa lengo la kusababisha vurugu kwenye ukanda wa Rift Valley ambao ni mtaji mzuri wa kura kwa wagombea wa urais, ukiwa ni mji wa tano kwa kuwa na idadi kubwa ya watu nchini Kenya.

Akionyesha kuchukizwa na vitendo hivyo, Ruto amemuomba Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa (NIS) kuhakikisha anakomesha mapema vitendo hivyo ili ya kuwa na uchaguzi wa amani.

“Kama mwenye mamlaka ya intelijensia zote nchini unawafahamu hawa watu ni akina nani (wahusika wanaosambaza vipeperushi), ni watu wako au watu wako wanawafahamu, naomba ukomeshe hili kwa sababu tunataka uchaguzi wa amani,” aliongeza.

Hii si mara ya kwanza kwa mgombea huyo kulalamika kuchafuliwa, huku siku chache nyuma akimtuhumu Rais Uhuru Kenyatta kumchafua na akimtaka kumnadi mgombea wake (Raila Odinga) na sio kumuongelea vibaya yeye.

Ruto ambaye pia ni kiongozi wa chama cha UDA amehudumu kama Naibu Rais wa Kenya kwa awamu mbili (2013 hadi 2017 na 2017 hadi 2022) chini ya Rais Uhuru Kenyatta, japokuwa kumekuwa na misuguano ya kimtazamo na kiitikadi kati ya wanasiasa hao mashuhuri.

Advertisement