TLS yajitosa sakata la uwekezaji bandari za Tanzania

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Harold Sungusia

Muktasari:

  • Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kimeunda kamati ya watalaamu ili kuuchambua mkataba kati ya Tanzania na Dubai, ambao pamoja na mambo mengine, unakijita katika ushirikiano wa kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuboresha utendakazi wa bandari nchini.


Dar es Salaam. Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kimeunda kamati ya watalaamu ili kuuchambua mkataba kati ya Tanzania na Dubai, ambao pamoja na mambo mengine, unakijita katika ushirikiano wa kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuboresha utendakazi wa bandari nchini.

Mkataba huo wenye ibara 31 ulisainiwa Oktoba 25, mwaka jana na serikali hizo mbili ili kuendeleza na kuboresha uendeshaji wa miundombinu ya kimkakati ya bandari za bahari na maziwa makuu, maeneo maalumu ya kiuchumi, maegesho ya utunzaji mizigo na maeneo ya kanda za kibiashara.

Mkataba huo uliofikia hatua ya kuridhiwa au kutoridhiwa na Bunge, umeibua mjadala kwa ya siku nne mfululizo kuhusu ibara zake 31 pamoja na uhalali wa Kampuni ya Kimataifa ya huduma za bandari Dubai Port World (DPW) itakayotekeleza uwekezaji kwa muda utakaojulikana kwenye mikataba ya utekelezaji

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Juni 8, 2023 na chama hicho, Makamu Mwenyekiti wa TLS Aisha Sinda ataongoza timu hiyo huku akisaidiwa Dk Hawa Sinare na wajumbe wajumbe wakiwa ni mawakili Mpale Mpoki, Stephen Mwakibolwa, na Mackphason Mshana.

“TLS inatambua uwepo wa mijadala inayoendelea nchini kuhusu makubaliano kati ya serikali hizo kuhusu uendeshaji wa bandari ya Tanzania na kampuni ya DP World ya Falme ya Dubai,” imenukuu sehemu ya taarifa hiyo iliyosiniwa na Rais wa TLS, Harold Sungusia.

“Kwa kuzingatia asili, uharaka na unyeti wa makubaliano hayo yanayopendekezwa, Baraza la Uongozi la TLS limeamua kuteua timu hiyo ya wataalam kutoka miongoni mwa wanachama wake ili kuchambua makubaliano yaliyopendekezwa,” imefafanua taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa TLS, kamati hiyo itajikita maeneo manne, ikianza kwa kuchambua mkataba huo, kushirikisha wadau wengine ili kuboresha, kufanya ulinganisho wa mikataba ya aina hiyo kabla ya kukabidhi ripoti hiyo Juni 12, mwaka huu mbele ya baraza ili TLS itoe yake maoni kwa hatua zaidi.