Prime
TMA yataja hatua kudhibiti tishio mabadiliko tabianchi
Muktasari:
- Shughuli za kibinadamu zimeendelea kuiharibu asili ya dunia, huku ripoti zikionyesha dalili za ongezeko la magonjwa mbalimbali mapya, mafuriko, ukame, kupotea kwa viumbe hai kwa miaka ijayo kutokana na mwenendo wa ongezeko la gesijoto.
Dar es Salaam. Shughuli za kibinadamu zimeendelea kuiharibu asili ya dunia, huku ripoti zikionyesha dalili za ongezeko la magonjwa mapya, mafuriko, ukame, kupotea kwa viumbe hai kwa miaka ijayo kutokana na mwenendo wa ongezeko la gesijoto.
Pamoja na juhudi zinazoendelea kufanyika kitaifa na kimataifa, imeelezwa kuwa mabadiliko hayo yanasababisha pia ongezeko la kiwango cha joto duniani.
Hata hivyo, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeshauri hatua nne kwa Taifa zinazoweza kupunguza athari zaidi nchini ikiwamo kuiongeza TMA vifaa vya kisasa vitakavyosaidia utabiri wa haraka, wananchi kutunza mazingira, kufuatilia na kutumia taarifa za hali ya hewa na kila taasisi kutekeleza mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na mabadiliko hayo.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Mwananchi, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Ladislaus Chang'a amesema tathmini ya Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), kwa awamu ya sita, inaonyesha hali ni mbaya ya mwenendo wa ongezeko la gesijoto.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ushawishi wa kibinadamu umeongeza athari za hali ya hewa kwa kasi ambayo haijawahi kutokea katika angalau miaka 2000 iliyopita.
Mabadiliko yalianza kurekodiwa kwa hasi 0.5 nyuzijoto ambayo ilianza kupanda hadi kufikia wastani wa nyuzijoto 1.1 kwa mwaka kwa sasa.
Aidha, kwa sasa anasema dunia kupitia Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), imekubaliana kila nchi mwanachama kushiriki kupunguza joto hilo linalokadiriwa kufikia wastani wa nyuzijoto 1.5C ifikapo mwaka 2030 na wastani wa nyuzijoto tano ifikapo mwaka 2100.
Dk Chang’a aliyechaguliwa hivi karibuni kuwa Makamu Mwenyekiti wa IPCC, anasema siasa za kidunia pia zina changamoto katika kukabiliana na vita ya uzalishaji wa hewa ukaa duniani.
“Jopo hili hufanya tathmini ya kidunia kila baada ya miaka mitano hadi saba, tangu kuanzishwa kwake tayari tathmini sita zimefanyika kubwa, hii ya sita itaenda kuwasilishwa katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) huko Dubai Novemba mwaka huu,”alisema.
“Kama Jumuiya za kimataifa hazitachukua hatua za makusudi, basi ongezeko litafikia nyuzijoto 1.5 mwaka 2030 na nyuzijoto 5 ifikapo mwaka 2100.Athari zake ni kubwa sana.Kwa bahati mbaya sana Afrika ndio inaendelea kuathirika zaidi,”alisema Dk Chang’a.
Ripoti mpya kuhusu mwenendo wa mabadiliko ya tabianchi ‘State of the Climate in Africa 2022’ inaonyesha zaidi ya watu milioni 110 barani Afrika waliathiriwa moja kwa moja na mabadiliko hayo pamoja na uharibifu wa kiuchumi wenye thamani zaidi ya dola bilioni 8.5 (Sh20.4 trilioni).
Aidha, mabadiliko hayo yalisababisha vifo 5,000, asilimia 48 vilihusishwa na ukame na asilimia 43 vilihusishwa na mafuriko.
Matumaini nchini
Wakati joto likizidi kuongezeka Tanzania kwa wastani wa nyuzi joto 0.5 kila mwaka, Dk Chang’a alisema Serikali imeamua kuchukua hatua mbalimbali ikiwamo kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2021/24 unaohusisha sekta tisa zinazozalisha zaidi hewa ukaa.
“Hivyo wadau wanatakiwa kuupitia huo mkakati na kuutekeleza kadri ambavyo inaelekeza kila mmoja kwa nafasi yake iliyoainishwa kuhamasisha uelewa kwa vijana, kutunza mazingira na kuvuna maji ya mvua. TMA pia inafanya tathmini ya mwelekeo wa hali ya hewa kila mwaka.”
Pili, Dk Chang’a alisema uwekezaji wa Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), mradi wa mabasi yaendayo haraka (UDART) na Mradi wa bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere (JNHPP), itasaidia kupunguza athari za mabadiliko hayo kwa njia ya kufyonza kaboni ikiwa ni utekelezaji wa mchango wake kwa dunia.
Dk Chang’a alisema uamuzi wa Serikali kuwekeza mafunzo ya wanafunzi 13 kufanya shahada ya uzamili nchini China kuhusu teknolojia, utoaji wa shahada ya kwanza ya masuala ya hali ya hewa kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na Chuo cha Hali ya hewa huko Kigoma, ni matumaini mapya.
Alisema juhudi nyingine ni kusimamia tathmini ya masuala ya hali ya hewa ukanda wa Afrika Mashariki, kuimarisha utamaduni wa kubadilishana taarifa za msingi na nchi jirani, huku ikiwa imewezesha usahihi wa taarifa za hali ya hewa kwa asilimia 90 ikiwa ni juu ya asilimia 70 ya malengo ya kidunia.
Hata hivyo, alishauri hatua kadhaa zinahitajika ikiwamo kuendelea na uwekezaji hasa miundombinu kama vile vifaa vya kuangaza na kuwekeza katika teknolojia ili kuimarisha zaidi huduma.
Wito wake
Dk Chang’a alisema endapo hakutakuwa na utayari wa kudhibiti ongezeko la joto duniani, asilimia zaidi ya 70 mpaka 90 ya Matumbawe baharini yanaweza kutoweka, mvua kuongeza, mafuriko ikilinganishwa na ilivyo sasa.
“Kwa Tanzania ongezeko la joto limeendelea kukua kuwa wastani wa nyuzijoto 0.5 na linaendelea kuongezeka, matukio ya hali mbaya yanaendelea kuongezeka lakini tunaona Serikali imekuwa na juhudi za kukabiliana na changamoto hizi,”alisema Dk Chang’a.
Alisema TMA itahakikisha taarifa zinawafikia watu wa mwisho kwa wakati na mfumo rahisi kwa wananchi ili waweze kuzitumia.
“Kwa hiyo katika mfumo wa kuwasilisha hizi taarifa kwa mtu wa mwisho, bado ni suala ambalo halijapata ufumbuzi mkubwa katika ukanda mzima wa Afrika,” alisema akifafanua:
“Kwa sababu wapo wadau wa aina tofauti kwa wale ambao wanaweza kupata taarifa kupitia runinga na mitandao ya kijamii hawa wanaenda vizuri, lakini kwa upande wa wakulima wao njia ya kuwafikia ni changamoto hivyo TMA imejaribu kuwekeza ili kuwafikia kwa njia ya simu ya mkononi.”
“Suala hili linaendelea kufanyiwa kazi kuangalia namna gani linaweza kuwa tija na ufanisi bila ya kuongeza gharama ya kiutendaji,” alisema.
Pili, Dk Chang’a alisema TMA inaendelea kuwajengea uwezo wadau wa sekta zote kuhusu matumizi sahihi ya huduma za hali ya hewa nchini.
Alisema hali ya hewa ni sekta mtambuka na kila mtu anaathirika kwa namna moja au nyingine katika shughuli zake kutokana na hali ya hewa, hivyo sekta zote zina mchango katika kuimarisha huduma za hali ya hewa.
Kuhusu ajali
Alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu mazingira ya ajali za ndege na meli licha ya kuwa na mamlaka ya kutoa taarifa za hali ya hewa kabla ya safari, Dk Chang’a alisema:
“Tunafanya kazi kwa kuzingatia miongozo yetu ikiwemo kutoa huduma za hali ya hewa kwa ajili ya usafiri wa anga na majini.