TMA yatoa tahadhari ya upepo mkali

TMA yatoa tahadhari ya upepo mkali

Muktasari:

  • Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetoa tahadhari ya kuwepo kwa vipindi vya upepo mkali unaofikia kilometa 50 kwa saa na mawimbi makubwa yanayozidi mita mbili.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetoa tahadhari ya kuwepo kwa vipindi vya upepo mkali unaofikia kilometa 50 kwa saa na mawimbi makubwa yanayozidi mita mbili.

Akizungumza leo Jumatatu Mei 3,2021 Ofisa Utabiri wa TMA, Rose Senyagwa amesema upepo huo unatarajiwa kuanza Mei 4 hadi Mei 7 mwaka huu katika maeneo ya Bahari ya Hindi ikiwemo mwambao wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Lindi, Mtwara,visiwa vya Unguja na Pemba.

Senyagwa amesema athari zinazoweza kujitokeza kuathirika kwa shughuli za usafiri na usafirishwaji,uvuvi katika maeneo ya Bahari ya Hindi.

Pia amesema vipindi vya mvua kubwa zinatarajiwa kunyesha kesho katika mikoa ya Dar es Salaam,Pwani,Tanga ,visiwa vya Ungija na Pemba.

"Hata hivyo hali hii ya mvua inatarajiwa kupungua ikilinganishwa na mvua iliyonyesha leo hivyo wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari na waendelee kufuatilia taarifa za TMA," amesema Senyagwa.