Tofauti ya wanandoa wa sasa, zamani

Muktasari:

  • Miaka ya karibuni yameshuhudiwa matukio ya ukatili baina ya wenza, huku taasisi ya ndoa ikionekana kuwa hatari kutokana na yanayoendelea ndani yake.

Miaka ya karibuni yameshuhudiwa matukio ya ukatili baina ya wenza, huku taasisi ya ndoa ikionekana kuwa hatari kutokana na yanayoendelea ndani yake.

Migogoro na mifarakano imekuwa kawaida kwa taasisi hiyo ambayo kuanzishwa kwake ililenga kukuza upendo na kuendeleza vizazi na vizazi, lakini sasa mambo yamekuwa tofauti.

Mengi yanatajwa kusababisha hali hii, kubwa ikiwa ni ndoa nyingi za sasa kufungwa kwa kukurupuka.

Wanandoa hawapati muda wa kuchunguzana na kujuana tabia kwa undani na matokeo yake inaleta shida katika safari hiyo ambayo kulingana na vitabu vya dini inapaswa kuwa ya kudumu.

Mwananchi imefanya mahojiano na wadau mbalimbali ambao wameeleza tofauti ya ndoa za sasa na zile za miaka ya zamani ambapo wazazi walihusika kwa kiasi kikubwa katika kushauri na kuwachagulia watoto wao wenza.

Wazazi wanasemaje?

Rukia Chacha (68) anasema changamoto kubwa iliyopo sasa ni vijana kuingia kwenye ndoa bila kufahamiana vyema kama ilivyokuwa zamani na ndiyo sababu ya ndoa nyingi kuwa na migogoro.

Anasema watu kuwa kwenye kipindi kifupi cha uchumba na uhusiano kuna uwezekano wa kuficha tabia zinazoweza kuleta shida katika siku za usoni.

“Sasa hivi kuna shida na binafsi naona haya maendeleo tuliyonayo ndiyo yanasababisha mambo haya, yaani watu wanakutana kwenye mitandao huko wanaanzisha uhusiano wanafunga ndoa,” anasema Rukia.

“Wengine wanakutana barabarani wanaingia kwenye uchumba kwa miezi mitatu, ndoa inafungwa, kwa utaratibu huu tutaendelea kusikia matukio ya ajabu kila kukicha, si wanawake wote au wanaume wote wanafaa kuingia kwenye ndoa.”

Rukia anaeleza kuwa ni muhimu kujuana tabia kabla ya kuingia kwenye ndoa na kila mmoja kuridhika na upungufu wa mwenzake kuliko kuyabaini baada ya ndoa kufungwa.

“Uchumba wa miezi mitatu ni rahisi mtu kuficha madhaifu yake ambayo baadaye mwenza wake akiyagundua inaweza kuwa chanzo cha migongano au hata ndoa kuvunjika, kuna watu ni wazuri mno kwa kuficha uhalisia wao ili wapate kitu wanachotaka, wakishafanikiwa sasa ndio utaona rangi zake halisi,” anasema Rukia.

Hata hivyo, Protas Lyimo (55) anasema upo uwezekano kuna vitu vingine vinavyochangia migongano na mifarakano katika ndoa za sasa tofauti na watu kushindwa kujuana tabia kabla ya kuingia.

“Binafsi naona kuna mengi zaidi ya kuchunguzana na kujuana tabia, hata hivyo maisha yamebadilika sasa vijana wanasoma wanakutana na wenza wao huko kwenye masomo au maeneo ya kazi wanapendana na kuamua kufunga ndoa, tena bahati mbaya huwa wakifikia kwenye hatua hiyo hawasikii ushauri hata wa wazazi,” anasema Lyimo.

“Utandawazi umetupeleka huko, mfumo wetu wa maisha umekuwa vigumu kwa mzazi kujua mtoto wa familia fulani anaweza kuwa bora kwa mwanao na hata hilo likitokea mtoto atakwambia mambo hayo yamepitwa na wakati anataka mtu atakayemchagua yeye kwa kuwa ndiye anaenda kuishi naye.”

Wanachosema wadau wengine

Akizungumzia hilo, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa anasema ni vyema ukarudishwa utaratibu wa zamani wa wazazi kuhusika kwenye uchaguzi wa wenza.

Sheikh Alhad anasema utaratibu huo uliokuwa ukiwashirikisha wazee ulisaidia kuwapata wenza baada ya kuwachunguza vijana na ndiyo sababu ndoa zilidumu.

“Zamani ilikuwa kijana akiamua kuoa, wazee wake ndiyo wanamshauri kaoe nyumba fulani hii kwa sababu wameshafanya uchunguzi wao na kuona huenda nyumba hiyo ina watu wenye maadili,” anasema Sheikh Alhad.

“Ni utaratibu ambao sasa unaonekana umepitwa na wakati, lakini ndio ulikuwa sahihi, vijana pia walifunzwa kuwa wavumilivu, hatukusikia masuala ya ukatili wala migogoro ya kila kukicha kama tunavyosikia sasa.”

Anasema kinachoendelea sasa, kwa kiasi fulani kinachangiwa na ndoa zinazofungwa na vijana bila kuwa na subira ya kupata muda wa kujuana tabia vyema kabla ya kuingia kwenye taasisi hiyo.

Sheikh Alhad pia amegusia suala la ukosefu wa maadili kuwa chanzo cha mifarakano kwenye ndoa na familia kwa jumla, huku watu wengine wakionekana kuachana na misingi ya dini.

Akizungumzia hilo, mtaalamu wa saikolojia, Deo Sukambi anasema hakuna uhusiano wa ndoa kudumu na wanandoa kuwa na muda mwingi wa kuchunguzana kabla ya kufikia kwenye hatua ya kuingia katika ndoa.

“Inaonekana kama ni sababu lakini kiuhalisia sio kweli. Hapa ni suala la tofauti tu ya kizazi na namna kinavyoitikia na kuchukulia mambo kutokana na masuala kadhaa, kubwa ikiwa ni kizazi cha sasa kukosa uvumilivu,” anasema Sukambi.

“Ni kizazi kilicholelewa kikiamini katika umimi, kupata wanachotaka, hawawezi kusubiri. Pia, kila mmoja anajiona anastahili na ni maalumu sana, hivyo dunia nzima imuelewe vile alivyo; hii haikuwepo kwa wazee wa zamani.

“Jambo lingine linalochangia hali hiyo ni shauku kubwa sana ya mafanikio kuliko shauku ya kuyafanyia kazi hayo mafanikio, ni kizazi kinachopenda raha kwa gharama za watu wengine,” anasema Sukambi.

Pia, anasema kizazi cha sasa pia kina tabia ya kulaumu, kusingizia na kuhisi mtu mwingine anawajibika kwa ajili ya furaha yake, jambo ambalo halikuwepo kwa wazazi wetu, wao walifundishwa kujitegemea.

Lingine ambalo limeelezwa kusababisha migogoro katika ndoa za sasa ni mitandao ya kijamii, ikielezwa kuwa imeleta mwingiliano mkubwa wa tamaduni, kuwafanya vijana waamini katika tamaduni za wengine.

“Sisi huku tunatafsiri tamaduni za wenzetu kuwa ni upendo. Mfano Wazungu wana tamaduni za zawadi, outing na mengineyo; sasa huku kwetu yanaonekana kama ni mapenzi; Hizi taswira tulizonazo zinaleta matarajio makubwa kuliko uhalisia, hivyo kiu ya kupendwa haikatiki kwa wengi na matokeo yake point ile ya kwanza hapo juu inaibuka na kuwatenganisha,” anasema Sukambi.

“Hilo linasababisha pia mtazamo mbaya kwa uhusiano, vijana wengi wanauchukulia uhusiano kama sehemu ya kutatua matatizo yao ambayo wameshindwa kuyatatua wenyewe.

“Hivyo, kijana anaingia ili mtu amsaidie shida zake za kiuchumi, kihisia, mpweke, kaumizwa ndio kinakuwa kichochezi cha kuingia huko; sasa anapojikuta uhusiano unamuongezea tatizo badala ya kulipunguza ndio mwanzo wa vita, hii fikra imezidi sana kukomaa katika kizazi cha vijana,” anasema mwanasaikolojia huyo.

“Kingine kinachosumbua ndoa nyingi za sasa ni shauku za kutaka kuwa huru. Ndoa maana yake kuuza uhuru wako. Kizazi cha sasa vijana wanataka uhuru na ndoa; hivyo viwili huwezi kuviweka pamoja, lazima ukipoteze kimoja na kwa wengi ni bora apoteze ndoa kuliko uhuru.”

Hata hivyo, anasema tatizo la afya ya akili, linachangia kwa kiasi kikubwa hivyo athari zake zinaonekana zaidi kwenye ndoa, ikielezwa kuwa tofauti na ilivyokuwa miaka ya zamani ndoa nyingi za sasa zinasumbua kwa sababu wanandoa hawako sawa na afya ya akili ndiyo chanzo kikubwa.