Tozo leseni za redio kupunguzwa

Monday July 26 2021
tozo pc
By Sharon Sauwa

Dodoma. Serikali ya Tanzania imeanza mchakato wa kupunguza tozo ya leseni za redio wilayani, za jamii na zilizoko pembezoni mwa nchi lengo likiwa ni kuimarisha usikivu wa mawasiliano hayo.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Julai 27 2021 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile wakati akifungua radio ya Jamii ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Amesema mchakato huo unafanywa na wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

“Tumekuwa tukiwatoza tozo za leseni za redio kwa mtu ambaye anaomba radio Dodoma, anaomba Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, tutakuwa hatuwatendei haki walioko pembezoni mwa nchi. Tumeamua kufanya mapitio ya tozo katika wilaya na maeneo yaliyoko pembezoni,”amesema.

Dk Ndugulile amesema lengo ni kuhakikisha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wanatimiza matakwa ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 kwa kuwa na usikivu wa kutosha nchi nzima inatimia.

Amewataka watu kuomba leseni hizo ambapo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza zabuni za masafa na leseni kwa mikoa 20 katika wilaya ambazo hakuna usikivu wa redio ikiwemo wilaya ambazo  ziko pembezoni.

Advertisement

Awali Mkurugenzi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, (USCAF), Justina Mashiba amesema ujenzi wa studio hiyo umegharimu Sh1.7 bilioni.

Advertisement