Tozo za moto

Muktasari:

  • Wakati wananchi wakilalamika kuanzishwa kwa tozo ya miamala ya kielektroniki katika akaunti za benki, mbunge wa Babati Vijijini na mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge, Daniel Sillo amesema ingawa zinauma ni lazima tu wananchi wazilipe.

Wakati wananchi wakilalamika kuanzishwa kwa tozo ya miamala ya kielektroniki katika akaunti za benki, mbunge wa Babati Vijijini na mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge, Daniel Sillo amesema ingawa zinauma ni lazima tu wananchi wazilipe.

Sillo ametoa maoni hayo licha ya wasomi, wanasiasa na wananchi kutaka tozo hizo ama zipunguzwe au zifutwe kabisa, wakisema zinawaongezea wananchi ugumu wa maisha unaosababishwa na kupanda kwa bei huku zikitishia mzunguko wa fedha kwenye sekta rasmi.

Mwenyekiti huyo wa kamati ya Bunge, amesema walitambua kuwapo kwa tozo hiyo na walikubaliana nayo hivyo wananchi wailipe tu.

“Sisi tulipitisha ile sheria, si kwamba hatukuona, sheria inapitishwa bungeni. Kilichofanyika, Serikali ilipunguza tozo ya miamala ya simu kwa asilimia 60, baada ya hapo ikaongeza mawanda. Kwa sababu wanaofanya miamala siyo kwenye simu peke yake, hata benki wanafanya kwa kuweka na kutoa fedha,” amesema Sillo.

Anasema tozo iliyokuwa inakatwa kwenye miamala ya simu pia ililalamikiwa na ikapunguzwa, sasa hivi benki nazo zimewekewa tozo.

Alipoulizwa kuhusu malalamiko ya wananchi wanayoyatoa kutokana na utekelezaji wa sheria ya tozo hizo, Sillo amesema “hakuna kodi inayofurahiwa, kodi hiyo ni ngumu lakini ndiyo inajenga vituo vya afya na inaleta maendeleo. Malalamiko ni baada ya watu kukatwa lakini mara nyingi tozo haifurahiwi.”

Sillo amesema hayo licha ya kumbukumbu za Bunge kuonyesha kuwa hakukuwa na mchango wa mbunge yeyote kuhusu kipengele hicho katika Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2022 uliosomwa kwa mara ya pili Juni 27. Tozo hizo zilianza kutumika Julai mosi.

Miongoni mwa wabunge waliochangia muswada huo ni wa Sikonge, Joseph Kakunda aliyesifu akisema hakukuwa na misuguano katika kuujadili.

“Naunga mkono hoja, tupitishe mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Fedha ambayo ndio tunaitegemea itumiwe na vyombo vyetu ikiwamo TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) kuhakikisha Sh28.02 trilioni zinapatikana. Tukikwamisha baadhi ya vipengele basi itaathiri ukusanyaji wa Sh28.02 trilioni,” alisema Kakunda.

Mbunge mwingine aliyechangia mjadala huo ni wa Viti Maalumu (Pwani), Subira Mgalu aliyeipongeza Serikali kwa kufanya marekebisho katika mifumo ya malipo sura 437, kupunguza ukomo wa tozo ya miamala kutoka Sh10,000 hadi Sh4,000.

Baada ya Bunge kutekeleza wajibu wake wa Kikatiba, Serikali ilitoa Kanuni za Sheria ya Mifumo ya Kitaifa ya Malipo (Tozo za Miamala ya Kieletroniki) za mwaka 2022 zilizoanza kutumika Julai mosi.

Kuanza kutumika kwa kanuni hizi, kumezifuta Kanuni za Tozo ya Miamala ya Simu za mwaka 2021 ambazo kutokana na malalamiko ya wananchi zilirekebishwa na kushusha kiwango cha juu cha makato kutoka Sh10,000 mpaka Sh7,000 kwa anayefanya muamala unaozidi Sh3 milioni.

Kuanza kutumika kwa tozo hizi, kumefuta Kanuni za Tozo za Miamala ya Simu za mwaka 2021, jambo ambalo rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Rugemeleza Nshala anasema kuzibatilisha kwake kunaziondoa kwenye matumizi hata zile za mwaka jana.

“Kama kanuni za sasa zimezifuta zilizopita, ukizikataa na Serikali ikasikiliza maana yake na za mwaka jana hazitatumika,” anasema Nshala.

Wanasiasa wapinga

Licha ya wananchi wanaolalamika mtaani, wataalamu wa kodi na fedha wanaoeleza kukiukwa kwa misingi ya kodi kwenye tozo hizi, wanasiasa hasa wa vyama vya upinzani nao wanataka mwananchi apunguziwe gharama za maisha.

Wiki iliyopita, Chama cha ACT Wazalendo kiliitaka Serikali kusitisha matumizi ya tozo za miamala ya kielektroniki na kutafuta vyanzo vingine vya mapato ili kumpa ahueni mwananchi wa kipato cha chini.

Naibu Msemaji wa Sekta ya Fedha na Uchumi wa ACT Wazalendo, Juma Kombo alisema makato hayo yameongeza mzigo kwa watumiaji wa huduma za benki.

“Badala ya Serikali kutafuta namna ya kumpunguzia mwananchi mzigo imeenda kuanzisha kodi mpya kwa watumiaji wa huduma za benki. Zitashusha ari na hamasa ya wananchi kutumia mifumo rasmi ya fedha, zitapunguza mzunguko wa fedha katika mfumo wa benki. Tunaitaka Serikali isitishe utekelezaji wake ili kuwapa wananchi nafuu ya maisha,” alisema Kombo.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alisema badala ya mwananchi kulundikiwa mzigo mkubwa, Serikali iangalie vyanzo vingine vya mapato kuanzia ardhi, madini, bahari, misitu na shughuli za biashara za ndani na nje.

“Tunahitaji hizo tozo ziwekwe kando kwanza, tutumie teknolojia kukuza ujasiriamali. Serikali itafute njia ambazo haziathiri jitihada za wananchi kujikwamua kiuchumi,” alisema Profesa Lipumba.

Aliyekuwa mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche anasema ni haki ya wananchi duniani kote kupiga kelele kunapokuwa na sheria mbaya zinazowaumiza, kwani bila kufanya hivyo Serikali haitajali.

“Kodi ina kanuni zake. There is no taxation without representation (hakuna kodi bila uwakilishi). Ingawa imepita bungeni, malalamiko haya yanadhihirisha kwamba waliopo kule ama uwezo wao ni mdogo kung’amua vitu vitakavyowaumiza wananchi wanaowawakilisha au hawakuchaguliwa ndio maana hawajali masilahi ya wengi,” anasema Heche.

Mwanasiasa huyo anasema wabunge wasipokuwa na uwezo, huwa shida kwao kung’amua mitego iliyowekwa kwenye miswada inayowasilishwa na Serikali, hivyo kupitisha sheria zitakazowaumiza wananchi.

“Serikali ni dude lenye mabavu hivyo sheria hutungwa ili kuibana isiwaumize wananchi. Kwa jinsi Bunge letu lilivyo, Serikali inaweza hata kupitisha kifungu cha kuwanyonga Watanzania na wabunge wakapiga makofi,” anatahadharisha Heche.

Kisheria, Dk Nshala anasema kanuni za tozo hizi zinakiuka Ibara ya 24 ya Katiba ya Tanzania inayomruhusu kila raia kumiliki mali. Ibara hiyo yenye vifungu viwili inasema, “bila ya kuathiri masharti ya sheria za nchi zinazohusika, kila mtu anayo haki ya kumiliki mali, na haki ya hifadhi kwa mali yake aliyonayo kwa mujibu wa sheria.”

Na, “bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (1), ni marufuku kwa mtu yeyote kunyang’anywa mali yake kwa madhumuni ya kuitaifisha au madhumuni mengineyo bila ya idhini ya sheria ambayo inaweka masharti ya kutoa fidia inayostahili.”

Kwa mfanyakazi anayepitisha mshahara wake benki au mfanyabiashara anayepeleka mapato yake benki kutozwa tozo hii, mwanasheria huyo nguli anasema “ni kumpora mali yake. Mshahara umeshakatwa PAYE (kodi ya mshahara) sasa anapoenda kuutumia hatakiwi kukatwa tena.”


Kodi mpya

Mtafiti wa Fedha na Sheria za Kodi, John Aguta anasema kodi mpya inapopendekezwa huzingatia sera ya fedha iliyopo na kuna mambo ya msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele.

Kwanza, anasema ni usawa kwa walipaji kwamba wenye kipato kinacholingana wanatakiwa kutozwa sawa, na kodi hiyo inatakiwa itozwe sehemu yenye ongezeko la thamani.

Ili kuepuka malalamiko ya wananchi, anasema kodi inatakiwa kueleweka kwa walipaji na iwe rahisi kukusanywa na watendaji huku ikitabirika kwa wadau, gharama za kuikusanya zisiwe kubwa kuliko kiasi kinachokusanywa.

Aguta anasema kodi hutozwa kwa kuzingatia Ibara ya 138(1) inayosema hakuna kodi ya aina yoyote itakayotozwa isipokuwa kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge au kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa kisheria na uliotiliwa nguvu kisheria na sheria iliyotungwa na Bunge.

“Wananchi wasiporidhika na kodi iliyopitishwa kwa utaratibu uliowekwa, mchakato wa kuiboresha unatakiwa ufuatwe ila ni muhimu kufahamu kwamba kuifuta kodi yoyote maana yake unapunguza vyanzo vya mapato ya bajeti iliyoidhinishwa,” anasema Aguta.

Tatizo lililopo, wakili huyo wa kodi anasema ni watu wengi kulalamika baada ya kodi kuanza kutumika badala ya kutoa maoni yao pindi muswada unapojadiliwa.

“Bunge hukusanya maoni ya wadau kila mara, lakini watu hawaendi kupeleka mtizamo wao. Wengi huwa tunasubiri kufanya postmoterm (kujadili baada ya sheria kupitishwa),” anasema.

Kwa kutozingatia utaratibu huo wa kitaaluma, Afrah Sanga anasema Serikali inatengeneza mazingira ya kuwakatisha tamaa wananchi kuwa wazalendo watakaolipa kodi kwa hiari yao.

“Mimi natokea Makete. Kule watu wanaamka alfajiri yenye baridi kali kwenda shambani. Fikiria mtu kama huyo eti akiuza mazao yake na kupeleka fedha zake benki, atakutana na kodi akitaka kuitoa. Sasa atakuwa na sababu gani za kutumia huduma za fedha,” alihoji mfanyabiashara huyo wa mbao jijini Dar es Salaam.

Afrah anasema haieleweki Serikali inataka nini kwa muda mrefu ujao, kwani inahamasisha matumizi ya huduma za fedha, zikiwamo za bima na benki halafu wanaleta tozo zinazokatisha tamaa.

“Inakuwa ngumu kwa watu wa masoko wanaowahudumia wakulima wa korosho kwa mfano. Umwambie mtu malipo yako utaingiziwa benki ambako anajua kuna makato. Wengi watauza kangomba inayopingwa na halmashauri,” anasema Afrah.

Ili Serikali ipate fedha, Aguta anasema inaweza kuanzisha kodi, tozo au ada. Kodi, anasema huwa endelevu ingawa mara chache inaweza ikaanzishwa ya malengo mahsusi.

“Kuna wakati sababu za kisiasa au kiuchumi zinaweza kulazimisha kuanzishwa kwa kodi. Mfano, wakati wa Vita Vikuu ya Pili ya Dunia, nchi zilianzisha kodi ya vita iliyolenga kugharimia mapambano. Vita ilipoisha nayo ikakoma,” anasema.

Vinginevyo, Aguta anasema Serikali hukusanya mapato kutoka kwenye tozo au ada, akitolea mfano tozo ya Umeme Vijijini (REA), barabara au reli pamoja na bili ya maji au umeme.

“Kwenye huduma kuna utility fee (ada ya huduma) unayolipa pindi utumiapo huduma hiyo. Usipoitaka basi unaiepuka. Tozo hutolewa kwa malengo maalumu, mfano uboreshaji wa barabara, usambazaji umeme au ujenzi wa reli. Inaweza kukoma lengo likikamilika,” anasema.

Utungaji sheria

Iwapo sheria mpya iliyopitishwa na Bunge haitoridhiwa na wananchi, Mkurugenzi mstaafu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba anasema wanaweza kuipinga kwa kufuata utaratibu uliopo kisheria.

Mwanasheria huyo anasema sheria inaweza kupingwa kwa wananchi kutoa maoni ya malalamiko kwenye mamlaka husika iwe kwa maandishi au maneno.

“Wananchi wanaweza kuwasiliana na mbunge wao, kwenda wizara husika iliyopitisha sheria inayolalamikiwa au kwenda bungeni kuwasilisha maoni yao. Huko kote, wanaweza kwenda wenyewe kwa kuandamana au wakaandika barua,” anasema.

Dk Hellen anafafanua kwamba, katika kuunda sheria, wazo linaweza kuibuliwa na wananchi au mbunge akatoa hoja binafsi bungeni. Ikionekana kuna mshiko, wataalamu wa wizara husika huiandaa halafu hupelekwa kwenye Baraza la Mawaziri kabla muswada haujaenda bungeni kusomwa.

Muswada huo ukishasomwa kwa mara ya kwanza, anasema unatakiwa kupelekwa kwa wananchi kwa ujumla ili watoe maoni yao kwa kuboresha maeneo muhimu yanayowahusu.

“Ndio maana unaona asasi za kiraia kila siku zinafanya ushawishi kuhusu kubadilisha sheria zinazoonekana kutokuwa sawa. Wananchi wakiona sheria ni mbaya wanatakiwa kuikataa,” anasema.

Baada ya wadau kutoa maoni, zikiwamo asasi za kiraia, wananchi wa kawaida na mashirika mahsusi bila kuwasahau wasomi na watafiti, Dk Hellen anasema muswada hurudishwa bungeni unakosomwa kwa mara ya pili na kujadiliwa na wabunge wanaowawakilisha wananchi wa nchi nzima.

Hatua hizo zote zikikamilika, anasema muswada husainiwa kuwa sheria na ni mara chache itapingwa na wananchi kwa sababu wanakuwa wameshirikishwa kuanzia hatua ya wazo lake mpaka mwisho.

“Katika Bunge letu, kuna sheria zinazopitishwa kwa hati ya dharura ambazo hazifuati utaratibu huu wa kuwashirikisha wananchi ndio maana malalamiko hutokea. Sikufuatilia sana Bunge la bajeti ila inawezekana sheria ya hizi tozo haikupelekwa kwa wadau,” anasema.

Kauli ya Serikali

Juhudi za kumpata Waziri Mwigulu hazikuzaa matunda lakini alipoulizwa Msemaji wa Wizara, Benny Mwaipaja kama kuna hatua zozote zimechukuliwa kushughulikia kilio cha wananchi alisema zipo.

“Waziri wa Fedha na Mipango atalizungumzia suala hilo hivi karibuni. Naomba usubirie ufafanuzi wa wake,” alisema Mwaipaja.