TPHPA kuongeza nguvu mikoa inayovamiwa na visumbufu mimea

Uongozi wa TPHPA ukipokea tuzo ya mshindi wa kwanza wa Mamlaka zilizotoa gawio kubwa serikalini kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan

Muktasari:

  • Changamoto kubwa kwa sasa kwa wakulima ni ndege aina ya kweleakwelea ambapo wamefanikiwa kuwadhibiti na kuokoa tani 5,675 za nafaka hasa mpunga, mtama na alizeti.

Arusha. Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) inatarajia kuongeza nguvu katika mikoa inayoonekana kuvamiwa zaidi na visumbufu mimea hasa wadudu na ndege waharibifu, ili kukabiliana na hasara wanayoipata kutokana na uharibifu wa mazao unaofanywa na wadudu pamoja na ndege hao.

Hayo yamebainishwa leo Juni 17, 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru alipozungumza na watafiti wa taasisi hiyo kuhusu kuimarisha utendaji kazi, sambamba na kutambulisha tuzo waliyopewa na Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kuibuka mshindi wa kwanza wa mamlaka iliyotoa gawio kubwa serikalini.

Amesema changamoto kubwa kwa sasa kwa wakulima ni ndege aina ya kweleakwelea na kwamba wamefanikiwa kuwadhibiti zaidi ya milioni 40 na kuokoa zaidi ya tani 5,675 za nafaka hasa mpunga, mtama na alizeti.

“Ndege hao tumewadhibiti katika mikoa ya Morogoro, Tabora na Manyara kwa kutumia viuatilifu kwa njia ya ndege nyuki, lakini bado kuna mikoa wanasumbuliwa, hivyo mamlaka iko nyuma yao, watoe taarifa na sisi tutaweka kambi huko,” amesema Profesa Ndunguru.

Akizungumzia tuzo hiyo, Professa Ndunguru amewataka wafanyakazi kuendelea kufanya kazi itakayosaidia nchi kutimiza malengo yake ya kujitosheleza kwa chakula, kuongeza mchango wa sekta ya kilimo kiuchumi.

“Tusiridhike na tuzo hii bali tuongeze nguvu ya kufanya kazi na sisi kama mamlaka tutahakikisha tunaboresha miundombinu ya kazi, ikiwemo ununuzi wa magari zaidi ya tisa yatakayokuja hapa Agosti na kusambazwa kwenye idara zenu.

“Mkaongeze nguvu kwenye kufikia maeneo yote, ili kupambana na visumbufu vya mimea, lakini pia kurahisisha ukaguzi wa viuatilifu visivyo na ubora mikoani,” amesema Profesa Ndunguru.

Amesema katika ukusanyaji wa maduhuri ya mwaka 2023/2024, mamlaka imekusanya Sh19.7 bilioni kama mapato ya ndani na kufanikiwa kutoa Sh3.7 bilioni kama gawio serikalini na fedha zilizobaki zitakwenda kuimarisha utendaji kazi katika idara zote.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa wafanyakazi kutoka TPHPA, John Elia ameupongeza uongozi wa mamlaka kwa kupewa tuzo hiyo na kuitaka Serikali kuboresha mazingira na maslahi ya wafanyakazi, ili kuongeza ufanisi zaidi kazini.

“Ni kongole kwetu wote maana utendaji na kujitoa kwetu ndio umeleta mafanikio ya upatikanaji wa fedha hiyo iliyotolewa gawio, hivyo Serikali ione ni wakati mwafaka sasa wa kuongeza maslahi ya wafanyakazi, ili mafanikio haya yaonekane zaidi,” amesema.