TPSF yaiomba Serikali iboreshe mazingira ya biashara

Mwenyekiti wa TPSF Angelina Ngalula

Muktasari:

  • TPSF imesema hotuba ya Rais Samia imeleta matumaini kwa wananchi na kutaka Serikali iboreshe zaidi mazingira ya biashara nchini. 

Dar es Salaam. Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imeeleza kuridhishwa na hotuba iliyotolewa Aprili 6 mwaka huu na Rais Samia Suluhu Hassan, ikishauri Serikali kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wawekezaji. 


Rais Samia alitoa hotiba hiyo wakati akiwaapisha makatibu wakuu, manaibu makatibu wakuu na wakuu wa taasisi katika ikulu ya Dar es Salaam na kutoa miongozo na maelekezo yanayolenga kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza ushiriki mpana wa shughuli za kujenga uchumi nchini.


Kufuatia hilo bodi ya TPSF kupitia Mwenyekiti wake Angelina Ngalula imetoa mapendekezo kwa serikali ambayo yatasaidia nchi kupiga hatua kwa haraka kwenye nyanja ya uchumi.
Mapendekezo hayo ni pamoja na kubadilisha na kuboresha mifumo ya kodi ili kuondoa migongano kati ya taasisi zinazotoza kodi na walipa kodi.


Lingine ni kupanua wigo wa walipa kodi kwa kurasimisha biashara zilizo katika sekta isiyo rasmi, kutengeneza bidhaa na huduma mpya ili kuongeza wigo wa kukusanya mapato pamoja na kutengeneza sheria na kanuni zitakazowawezesha watanzania kushiriki katika uwekezaji na utekelezaji wa miradi mikubwa.


Pia Angelina amesisitiza umuhimu wa kuainisha maeneo ambayo yanaweza kutoa matokeo ya haraka bila kutumia gharama kubwa za uwekezaji wa muda mrefu.