TRA Kigoma yakiri kumtambua mtumishi anayedaiwa kudakwa na meno ya tembo
Muktasari:
- Taarifa za kukamatwa kwa Bagisheki zilianza kusambaa jana kwenye mitandao ya kijamii zikimtaja ni mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Kigoma.
Kigoma. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma, limethibitisha kuwa linamshikilia Arving Bagisheki (39) akidaiwa kukutwa na meno mawili ya tembo ndani ya gari.
Taarifa za kukamatwa kwa Bagisheki zilianza kusambaa jana kwenye mitandao ya kijamii zikitaja kuwa ni mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Kigoma.
Mwananchi imezungumza na Meneja wa TRA Mkoa wa Kigoma, Deogratius Shuma ambaye amekiri kumfahamu na kuwa akidai anakaimu nafasi ya meneja wa Wilaya ya Kibondo.
Hata hivyo, kuhus kukamatwa kwake, Shuma amesema na yeye amesikia na kuona taarifa za kukamatwa kwake mitandaoni, lakini taarifa rasmi hana.
“Sina taarifa zozote rasmi kuhusu kukamatwa kwake na mimi naona mitandaoni kama ninyi, kwa picha zinazosambaa mitandaoni ninafahamu alikuwa kaimu meneja wa TRA Wilaya ya Kibondo, lakini kwa taarifa zaidi wasiliana na Jeshi la Polisi linaweza kukupa taarifa kamili,”amesema Shuma.
Akizungumza leo, Julai 3, 2024 ofisini kwake mjini hapa, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Iddi Kiyogomo amesema tukio hilo lilitokea Julai mosi, 2024, Saa 4:00 usiku, katika eneo la Kihomoko kwenye kizuizi cha Polisi wa Usalama Barabara wilayani Kakonko.
Amesema meno hayo yamekutwa kwenye gari la Serikali aina ya Toyota Landcruiser.
Hata hivyo, kaimu kamanda huyo amesema wakati linakamatwa gari hilo, lilikuwa limebandikwa namba bandia ya usajili.
“Jeshi la Polisi kwa sasa linaendelea kumhoji mtu huyo na baada ya upelelezi kukamilika atafikishwa mahakamani. Niwaombe wananchi waendelee kushirikiana na Jeshi la Polisi kuzuia na kubaini uhalifu ili kuimarisha usalama wa raia na mali zake,” amesema Kiyogomo.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana usiku, Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Evance Mallasa alisema mtumishi huyo alikamatwa Julai mosi, 2024 kwenye geti la ukaguzi akiwa anatokea wilayani Kibondo kwenda mkoani Kagera.
“Kwa sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi,” alisema Kanali Mallasa.
Taarifa za Mutegeki zilizoambatana na picha yake akiwa na meno hayo ya tembo zimesambaa katika mitandao ya kijamii, zilimhusisha na biashara ya nyara hizo kwenye mikoa mbalimbali na nje ya nchi.