Jinsi mfumo wa ETS unavyotambua bidhaa bandia

Muktasari:

  • Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), inatarajia kuanzisha mfumo wa "mobile app” utakaotumia simu ya mkononi kumuwezesha mteja kutambua bidhaa kama ni bandia au halisi kabla hajaitumia.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), inatarajia kuanzisha mfumo wa "mobile app” utakaotumia simu ya mkononi kumuwezesha mteja kutambua bidhaa kama ni bandia au halisi kabla hajaitumia.


Mfumo huo utakaozinduliwa wakati wowote kuanzia sasa, unatokana na mafanikio ya matumizi ya stempu za kodi za Kieletroniki (ETS) ambao umewasaidia wazalishaji viwandani kudhibiti bidhaa bandia.


Meneja mradi wa stempu za ETS kutoka TRA, Innocent Minja alisema mfumo wa mobile app utamuwezesha mteja kujua uhalisia wa bidhaa kabla hajaitumia.


Alisema mobile app ni mojawapo ya malengo ya kuanzishwa kwa stempu za ETS, kumuwezesha mteja kutambua bidhaa yenye stempu halali kwa kutumia simu ya mkononi,
Minja alisema kuanzishwa matumizi ya stempu za ETS kwenye bidhaa baada ya kupiga marufuku utumiaji wa stampu za karatasi, ni mojawapo ya hatua ya Serikali inayolenga kuboresha usimamizi wa kodi nchini.


“Kwa kifupi, huwezi kusikia tena malalamiko kuwa maofisa wa TRA wamemuongezea mtu kodi kwa makusudi kwa bidhaa zinazotumia stempu za ETS,” alisema.


Minja alisema pia stempu za ETS zinasaidia kupata data za uzalishaji kwa wakati kutoka kwa wazalishaji.
Alisema tangu kuanzishwa kwa mfumo huo, wanufaika wamekuwa ni Serikali, wazalishaji, waagizaji na watumiaji.


Minja alizitaja faida hizo kuwa ni kulinda mapato ya Serikali kwa kuzuia bidhaa bandia, kuongeza uhiari wa ulipaji kodi kwa kutengeneza wigo sawa wa ushindani kwa wafanyabiashara wote wanaozalisha na kuingiza bidhaa nchini.


Faida zingine alisema ni kuwezesha ufuatiliaji wa bidhaa kutoka viwandani, mipakani, bohari zilizoruhusiwa, majengo ya kutunzia bidhaa, sokoni hadi kwa mlaji.


Pia, alisema faida nyingine ni kuwezesha usimamizi wa bidhaa zinazotengenezwa au zinazoingizwa kutoka nje ya nchi.
Alizitaja baadhi ya bidhaa zilizoorodheshwa kutumia stempu za ETS ni maji ya kunywa ya viwandani, sigara, juisi, vinywaji baridi, bia, mvinyo, pombe kali na vileo vingine.


Alisema tangu ETS ianze Januari 2019, mbali na kujua bidhaa feki na halisi, kumeongezeka idadi ya wazalishaji waliwekewa mfumo wa stempu za ETS.


“Idadi ya wazalishaji wa bia, pombe kali na mvinyo imeongezeka kutoka 57 hadi 272, Agosti mwaka huu... kwa ufupi hizi stempu zimesaidia kuongeza wigo wa kodi,” alisema Minja.


Serikali ilitangaza mpango wa kuanzisha mfumo wa stempu za ETS Juni 2018 na awamu ya kwanza ya mradi ilifanyika Januari 15, 2019 ambapo stempu ziliwekwa kwenye kampuni zinazozalisha bia, mvinyo na pombe.


Awamu ya pili ya mradi huo ilianza Agosti 1, 2019 wakati stempu za ETS zilibandikwa juu ya maji yenye ladha na vinywaji vingine visivyo vya pombe.


Awamu ya tatu, ambayo ilijumuisha kusajili stempu za elektroniki kwenye juisi za matunda, juisi za mboga na maji ya kunywa ya chupa, ilianza Novemba 1, 2020.