Mpangaji kuzuia 10% ya kodi yake na kuilipa TRA

Ofisa huduma na Elimu mkuu kutoka mamlaka ya mapato TRA Eugenia Mkumbo akifafanua jambo wakati wa mafunzo ya mabadiliko ya sheria ya kodi ya mwaka 2022. Picha na Samirah Yusuph

Muktasari:

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia mabadiliko ya Sheria ya Kodi ya Mwaka 2022, imeanza kusimamia sheria inayowapa mamlaka wapangaji wote kuzuia kodi ya pango katika nyumba binafsi na zile za biashara ili kurahisisha ulipaji na ukusanyaji wa kodi ya pango.

Bariadi. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesisitiza wapangaji katika nyumba za kapanga kuwa wazalendo na kulipia asilimia 10 ya kodi wanazokuwa wakilipa kwa wenyenyumba ili kulipia kodi ya pango.

 Hayo yamesemwa na Ofisa Huduma na Elimu Mkuu wa TRA, Eugenia Mkumbo katika mafuzo ya wafanyabiashara juu ya mabadiliko ya sheria ya kodi mwaka 2022, leo Alhamisi Agosti 25, 2022 wilayani Bariadi, Mkoa wa Simiyu.

Amesema kifungu cha 82(2) (a) cha sheria ya kodi kimefuta msamaha wa kodi kwa wapangaji binafsi, hivyo kuwapa mamlaka wapangaji wote kuzuia kodi ya pango katika nyumba binafsi na zile za biashara ili kurahisisha ulipaji na ukusanyaji wa kodi ya pango.

"Kama umepanga chumba kiwe cha biashara au makazi unajukumu la kukata asilimia 10 na kuilipa TRA na mwenye nyumba utampelekea nakala ambayo inaonyesha umelipia kodi, utaambatanisha na pesa iliyobaki unampa mwenye nyumba," amesema Eugenia 

Aidha, amesema Serikali imefuta kodi kwa wanafunzi wanaokwenda kupata mafunzo ya vitendo kwa lengo la kuwarahisishia waajiri kuwapa nafasi ya kupata uzoefu wa kazi kwa urahisi wanafunzi wanaohitimu masomo.


Akifafanua kuhusu kodi ya pango, Kissa Kyejo, Afisa Mkuu Usimamizi wa Kodi amesema mfanyabiashara ni mbia wa Serikali na anapaswa achangie kipato unachopata kwa kulipa kodi.

"Yule mwenye nyumba anapata kipato kwa sababu analipwa na wapangaji lakini TRA tunaweza tusimfikie mwenye nyumba kwa sababu hana namba ya utambulisho wa mlipa kodi.

“Pengine amejenga nyumba na sio mfanyabiashara sheria, ilichofanya ni kwamba mpangaji ambae ndie anamlipa mwenye nyumba kipato aweke zuio na kulipa kodi ya pango," amesema

Baadhi ya wapangaji katika mji wa Bariadi, wamesema kodi hiyo ni kama mgogoro kati ya wenye nyumba na wapangaji kwa sababu ni kazi ngumu kumlipia kodi mtu ambaye hajaamua kulipa kodi kwa hiari.

"Kabla ya kumpa mamlaka mpangaji kuzuia hela ya pango ili kulipa kodi, wangewaita wenye nyumba na kuwapa elimu ili wawe tayari kukatwa pesa zao lakini saizi itakuwa ni changamoto sana kwa sababu wengi hawajui hata hiyo kodi inahusu nini," amesema John Lucas mkazi wa Kidinda.