TTB, Azam waungana kutangaza utalii

Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Jaji mstaafu Thomas Mihayo (katikati) na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Tido Mhando kushoto baada ya kuingia makubaliano ya kutangaza utalii kupitia kipindi cha runinga leo Jumanne Januari 18, 2022.

Muktasari:

Kipindi hicho kitakafahamika kama Shangazwa kinalenga kuonyesha vivutio vya utalii vilivyopo nchini hasa vilivyopo kwenye ukanda wa kusini.

Dar es Salaam. Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imeingia makubaliano na Azam Media yanayolenga kutangaza utalii kupitia kipindi cha runinga.

Makubaliano hayo yameingiwa leo Jummane Januari 18, 2022 ambapo matangazo yatapatikana kwenye kipindi kitakafahamika kama Shangazwa kikilenga kuonyesha vivutio vya utalii vilivyopo nchini hasa vilivyopo kwenye ukanda wa kusini.

Mwenyekiti wa TTB, Jaji mstaafu Thomas Mihayo amesema ushirikiano huo unalenga kutangaza zaidi vivutio vya utalii ndani na nje ya Tanzania.

Amesema “Kazi yetu kubwa ni kutangaza utalii na hatuwezi kutimiza hilo bila kuhusisha wadau wakiwemo wa habari. Azam inafanya vizuri sana na tumeona tuna kila sababu ya kushirikiana nao.

“Wamefanya kazi kubwa kuonyesha upekee wa vitu tulivyonavyo kupitia vipindi vyao na sasa wamevuka mipaka wako katika nchi kadhaa za Afrika,” amesema Jaji Mihayo.

Amesema kupitia ushirikiano huo ni matumaini ya bodi kuwa utaongeza idadi ya watalii kutoka katika nchi zaidi ya saba za kusini mwa jangwa la sahara zinazofikiwa na matangazo ya Azam Tv.

Kwa upande Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Tido Mhando amesema mkataba wa mwaka mmoja ni mwanzo wa ushirikiano baina ya taasisi hizo ambao utadumu kwa muda mrefu.

“Kupitia kipindi hiki cha Shangazwa tuna imani wananchi wa Tanzania watapata fursa ya kuielewa vizuri nchi yao na hata wale wa nchi nyingine wataweza kufahamu vitu vya pekee vinavyopatikana hapa nchini.

“Tunataka watanzania waelewe kuwa vivutio hivi ni tunu kwa nchi yetu hivyo tuna kila sababu ya kujivunia na kuonyesha ulimwengu,” amesema Tido.