Tujadili Katiba tunayoitaka

Tujadili Katiba tunayoitaka

Muktasari:

  • Kaandika mwanaharakati wa kujitegemea Mange Kimambi, katika ukurasa wake wa Instagram na katika hili yupo sahihi sana: “Unajua mi nawashangaa sana wanaokausha makoo sababu ya Katiba Mpya. … Jamani Katiba Mpya itakuja hata bila wapinzani kukausha makoo.”

Kaandika mwanaharakati wa kujitegemea Mange Kimambi, katika ukurasa wake wa Instagram na katika hili yupo sahihi sana: “Unajua mi nawashangaa sana wanaokausha makoo sababu ya Katiba Mpya. … Jamani Katiba Mpya itakuja hata bila wapinzani kukausha makoo.”

Mange Kimambi anasema miaka mitano ya Hayati Rais John Magufuli imetoa somo kubwa kwa kila Mtanzania. “Sio CCM, sio Chadema, sio Rais Samia Suluhu Hassan wala sio Rais mstaafu Jakaya Kikwete. Sidhani kama kuna mtu anataka kujiweka katika hatari tena tulichokipitia kwa Magufuli. Yaani CCM wenyewe wataileta katiba mpya bila kushikwa shati na mtu maana kama chamoto na wao walikiona kwa Magu (Magufuli).”

Yuko sahihi, ingawa alinogesha alipodai hakuna Mtanzania asiyetaka Katiba Mpya. Kiukweli, wapo wasioitaka; na wapo wengine hawajali.

Ije, isije kwao sawa tu. Lakini wale wanaounda kundi ambalo lina ushawishi katika kujenga maoni ya umma ‘elites’ wengi wanataka katiba mpya.

Hitimisho la Kimambi kuwa katiba ni suala la muda tu na kwamba haiepukiki, ni sahihi kwa sababu nyingi zaidi, sio tu kwa sababu ya somo la mwendazake. Kadhalika, ni muhimu sana watu waukubali ukweli huu mapema ili wajiandae kwa masuala na ajenda zake.

Kwanza, Katiba Mpya si mradi mpya. Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete alitangaza kuanzisha mchakato huu katika hotuba ya mwaka ya kuupokea mpya wa 2011 na wakati Tanganyika ikiadhimisha miaka 50 ya uhai wake.

Kikwete alisema walikubaliana serikalini kuwa katika kuadhimisha miaka 50 ya uhai wa taifa wafanye mambo manne, ikiwemo kuanza mchakato wa kuandikwa katiba mpya inayoendana na taifa lenye umri wa nusu karne na ambayo italipeleka taifa 50 ijayo.

Hata hivyo, mchakato uliishia njiani kwa sababu ya mabishano ya wanasiasa. Hii maana yake ni kwamba walau tulivuka hatua ya kukubaliana umuhimu wa katiba mpya. Aliyeanzisha mchakato ule ni rais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) bila shaka kwa makubaliano ya chama chake. Kwa sababu hizo sioni ni vipi CCM wanaweza kuua mchakato huo baada ya kutumia rasilimali fedha nyingi.

Kadhalika, ukichambua maelezo ya Rais Samia mara zote alipozungumzia Katiba mpya alionesha kuitaka, isipokuwa tu anadhani kwa sasa sio muda sahihi kwa sababu nchi inapitia kipindi cha mpito cha kurejesha imani ya wafanyabiashara, jumuya ya kimataifa na wananchi kwa ujumla kwa utawala sheria.

Kampeni hizi za mitadaoni na katika makongamano zitawalazimisha CCM walipe jambo hili kipaumbele. Pia, wafadhili wanasikia na wanaweza kuweka mbinyo kwa Serikali ili mchakato wa Katiba ufufuliwe haraka.

Muhimu zaidi, kama alivyodokeza Kimambi, Rais Magufuli ametusaidia sana kutuhakikishia umuhimu wa Katiba nzuri. Katika utawala wake, Rais Magufuli alitutoa kwenye nadharia na kutuonesha kiuhalisia nguvu ya rais chini ya Katiba iliyopo.

Kama kuna cha kujifunza basi ni kwamba, Rais anaweza kufanya maisha ya watu asiowapenda yawe magumu sana. Kwa mkono mmoja, Rais anaweza kufifisha upinzani wa kisiasa, kulinda viongozi wanaofanya uhalifu wa kutisha, kutoheshimu sheria.

Utawala uliopita haukuwa rafiki kwa watu wenye mawazo tofauti. Taasisi za udhibiti wa Serikali zilifanya maamuzi kwa maslahi ya kisiasa zaidi. Harakati za vyama vya kiraia zilipata pigo kubwa.

Baada ya tuliyopitia, nani haoni umuhimu wa kuwa na vyombo vyenye nguvu vya udhibiti wa Serikali? Baada ya uchaguzi wa 2020, nani haoni haja ya kuwa na tume huru ya uchaguzi itakayotuhakikishia matakwa ya watu yanaheshimiwa?

Muda sahihi

Katiba haiepukiki, bali ni suala la muda tu. Rais Samia ana sababu nyingi za kuahirisha mchakato wa Katiba hadi hapo baadaye aidha kwa maslahi ya umma au yake binafsi na pengine chama chake, lakini hatimaye Katiba Mpya itapatikana.

Tusukume ajenda

Pale mchakato utakapoanza, nina wasiwasi baadhi ya makundi ya watu wataona wameshtukizwa kwa kuwa hawakujiandaa kusukuma ajenda zao. Huu ni muda muafaka wa kusukuma ajenda ili kutafuta uungwaji mkono.

Nikiwasoma wanachama wa makundi ya wanaodai Katiba Mpya, wengi wanajua nini wanataka kwenye hiyo Katiba. Tatizo lipo kwa wale wanaodhani namna bora ya kumuunga mkono Rais Samia ni kupambana na wanaoitaka Katiba Mpya.

Katiba Mpya yaja, tena yaja katika kipindi cha Rais Samia akijaaliwa uhai kutawala hadi 2025.

Uandishi wa Katiba ni suala la mashauriano. Si sawa kutegemea kila jambo lako unalolitaka likubalike. Mkwamo katika mchakato wa kwanza ulitokana na misimamo mikali.

Si sawa kutegemea kuwa rasimu itawasilishwa kwenye Bunge la Katiba, halafu itoke bila mabadiliko yoyote, na kama ni hivyo basi hilo Bunge liliundwa kwa nini?

mchakato wa uandishi wa katiba ni kura, hivyo kama unadhani Katiba iliyopendekezwa haifai kajengeni hoja kwa wananchi waikatae.

Imeandikwa na Na Njonjo Mfaume