Tulia ataka mpango maalum kukarabati shule kongwe
Muktasari:
Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameshauri Serikali kuwa na mpango maalum wa kukarabati shule za msingi na sekondari nchini.
Dodoma. Dk Tulia ameyasema hayo leo Jumatano Aprili 3, 2024 mara baada ya Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange kujibu swali la Mbunge wa Mbarali, Bahati Ndingo.
Bahati amehoji ni lini Serikali itakarabati shule kongwe za msingi zilizopo Mbarali ambazo zipo katika hali mbaya.
Akijibu swali hilo, Dk Dugange amesema Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya elimu ikiwemo ujenzi wa madarasa mapya na ukarabati wa madarasa chakavu.
Amesema katika mwaka wa fedha 2022/23 na 2023/24, Serikali imetumia Sh360 milioni kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa madarasa 18 mapya katika shule kongwe za Chimala, Igalako, Ujewa na Isitu.
“Mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imetenga Sh180 milioni kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe za Ipwani, Ibumila, Mbuyuni,”amesema.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe kote nchini.
Baada ya majibu hayo, Dk Tulia amesema tatizo hilo lipo kwenye maeneo mengi kwenye shule kongwe na madarasa yake sio makongwe sana.
Amesema hiyo inatokana na sababu madarasa wanayatumia watoto kwa hiyo yanaharibika haraka.
“Kwa sababu tuna Wizara ya Mipango na Uwekezaji kwa kweli tuwe na mpango wa kukarabati shule za msingi zote na sekondari zote kule yalikojengwa madarasa mapya. Kuna madarasa mapya yapo kwa sababu watoto wanasoma kule kuna yenye hali mbaya sana,”amesema.
Ameitaka Serikali kuainisha shule chakavu nchini kwa ajili ya ukarabati.
Dk Tulia amesema madarasa mapya yaliyojengwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika shule mbalimbali yafanane na yale yaliyokuwepo nchini.
Naye Mbunge wa Busanda, Tumaini Magesa amehoji ni lini Serikali itakarabati shule chakavu za Busanda.
Akijibu swali hilo la nyongeza, Dk Dugange amesema tayari Serikali imeanza kuanisha shule chakavu kote nchini na fedha zinatafutwa kwa ajili ya kuanza ukarabati kwa awamu.
Amesema na hivyo jimbo la Busanda pia litapewa kipaumbele.