Tume ya Madini yakusanya Sh100 bilioni Mara

  • Afisa Madini mkazi mkoa wa Mara, Joseph Kumburu akizungumza na waandishi kuhusu mafunzo kwa wachimbaji wadogo na viongozi wa serikali za vijiji na kata wilayani Tarime.  Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Tume ya Madini Mkoa wa Mara imekusanya zaidi ya Sh100 bilioni sawa na asilimia 78.75 kati ya lengo la kukusanya Sh127 bilioni kwa mwaka huu wa fedha mapato yanayotokana na kodi mbalimvali za serikali kutoka sekta ya madini.

Tarime. Tume ya Madini Mkoa wa Mara imekusanya zaidi ya Sh100 bilioni sawa na asilimia 78.75 kati ya lengo la kukusanya Sh127 bilioni kwa mwaka huu wa fedha mapato yanayotokana na kodi mbalimvali za serikali kutoka sekta ya madini.

Akizungumza kwenye mafunzo kwa wachimbaji wadogo pamoja na viongozi wa serikali za vijiji na kata zilizopo wilayani humo, ofisa Madini Mkoa wa Mara, Joseph Kumburu amesema kuwa fedha hizo ni mapato kutoka kwa wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa.

Amesema ofisi yake inatarajia kufikia malengo ya makusanyo ifikapo mwisho wa mwaka wa fedha 2021/22.

Amesema kuwa miezi michache iliyopita makusanyo hayo yalishuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vitendo vya utorishaji wa madini vilivyoanza kuibuka mkoani Mara lakini tayari vitendo hivyo vimedhibitiwa na hali ya ukusanyaji wa mapato pia imeimarika.

"Hapa katikati tulirudi nyuma kidogo lakini baada ya kubaini tatizo ni nini tulianza kufanya oparesheni mbalimbali ikiwa pamoja nakuweka usimamizi imara kwenye migodi pamoja na mipakani na tayari matokeo yameanza kuonekana kwani mapato yameanza kupanda," amesema Kumburu

Akizungumzia mafunzo hayo, Kumburu amesema kuwa mbali na kuwa ni sehemu ya kuimarisha makusanyo ya serikali lakini pia mafunzo hayo yanalenga kuboresha mazingira ya wachimbaji kwa ujumla na hivyo kufanya kazi zao katika mazingira rafiki.

"Zipo changamoto nyingi zinazowakabili wachimbaji hasa wadogo ikiwemo migogoro na hata matumizi ya kemikali hatarishi hivyo mafunzo haya yanalenga kuwapa elimu juu ya uchimbaji wenye tija na kuleta mahusiano mazuri baina ya wachimbaji, wamiliki wa leseni pamoja na wenye mashamba," amesema Kumburu.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru ofisi ya madini kwa kuandaa mafunzo kwa maelezo kuwa mafunzo hayo yatasaidia utendaji wao wa kazi kwa ujumla.

"Kuna migogoro mingi sana kwenye machimbo yetu nadhani mkoa wetu unaweza kuwa unaongoza kwa migogoro ya wachimbaji, haya mafunzo yatasaidia kwenye utatuzi wa migogoro hii ambayo inachangia kudorora kwa shughuli zetu," amesema John Lyamela ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wadogo mkoani humo.