Tumuenzi Nyerere kwa vitendo si maneno matupu

Muktasari:

  • Leo ni siku ya kumbukumbu ya kifo cha mwasisi wa Taifa la Tanzania Julius Nyerere aliyefariki dunia miaka 22 iliyopita, mimi ningetamani tumuenzi kwa kuyafuata yale aliyoyaamini na kubwa ni la kutaka kuwa na taifa la watu wenye uthubutu wa kuhoji.

Leo ni siku ya kumbukumbu ya kifo cha mwasisi wa Taifa la Tanzania Julius Nyerere aliyefariki dunia miaka 22 iliyopita, mimi ningetamani tumuenzi kwa kuyafuata yale aliyoyaamini na kubwa ni la kutaka kuwa na taifa la watu wenye uthubutu wa kuhoji.

Wala si dhambi kama anayekosoa anafanya hivyo kwa dhamira njema ya kujenga na ndio maana katika kipindi cha uhai wake alitoa hotuba ambazo mimi, wewe na atakayekuja kuzisikiliza vizazi na vizazi atadhani ndio ameongea leo.

Nyerere si tu kwamba alitaka tuwe na taifa la watu wenye uthubutu wa kuhoji, lakini katika hotuba zake alihubiri haki haki haki na hakika aliliacha Taifa la Tanzania likiwa na umoja, upendo na mshikamano ambao sasa umetikiswa.

Baba wa Taifa alikataa ubaguzi wa aina yoyote ile uwe wa rangi au kabila lakini tunapomkumbuka hebu tujitafakari kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2020 kama kweli tulimuenzi Nyerere au linapokuja suala la maslahi tunamweka pembeni?

Nasema hivyo kwa sababu licha ya Katiba ya Tanzania Ibara ya 13 kukataza ubaguzi wa aina yoyote, wakati wa uchaguzi huo watu walihubiriwa wachague mgombea wa chama fulani cha siasa vinginevyo hawatapata maendeleo.

Sasa ndio maana nimetangulia kusema kama kweli tunafuata nyayo za Baba wa Taifa na kuenzi falsafa zake basi tusitamke tu midomoni kuwa tunamuenzi Nyerere wakati mioyoni mwetu tunamng’ong’a na kuharibu misingi aliyotuachia.

Katika makala yangu leo nitaweka nukuu chache za Baba wa Taifa ili kesho tunapoadhimisha Nyerere Day tukikumba Oktoba 14, 1999 ambayo ndiyo siku aliyofariki dunia, basi tutafakari tulipotoka, tulipo na tunapotaka kwenda.

Moja ya nukuu inasema “Itakuwa yote ni makosa na si jambo la muhimu kuhisi kuwa lazima tusubiri hadi viongozi wafe ndipo tuanze kuwakosoa,” lakini leo hii hakuna Watanzania walishitakiwa kortini kwa kuwakosoa viongozi?

“Tunataka kuona vijana wenye ujasiri wa kuhoji na kupiga vita mifumo ya kidhalimu isiyoshabihiana na matakwa na matarajio ya Watanzania. Tunataka vijana waasi mifumo kandamizi, ubwana na ufisadi,” ananukuliwa Nyerere.

“Udikteta ni serikali ya mtu mmoja au kikundi cha watu wachache ambao wao ndio huwa sheria, anayepinga watakayo ataonyeshwa cha mtemakuni”

“Utii ukizidi sana unakuwa woga. Mara zote huzaaa unafiki na kujipendekeza. Sasa nyinyi watumishi wa umma kwa wingi wenu kama mmeshindwa kupiga kura kuondoa viongozi dhalimu bora mfe”, mwisho wa nukuu kwa makala leo.

“Mkianza mkiwa na woga, I promise you (nawaahidi), iko siku mtatawaliwa na dikteta. Mkiogopa-ogopa namna hii ninyi, wabunge, mkiogopa-ogopa, mkisema mzee wanakuwa wakali, then you are making absolutely fake, you will be under a dictator.

Kama nilivyotangulia kusema, Baba wa Taifa alitaka taifa la Tanzania liwe ni la watu wanaohoji, wanaochukia ubaguzi, wanaopenda haki na wanaoishi katika umoja na mshikamano, lakini tunapomkumbuka taifa liko katika hali gani?

Leo hii licha ya Katiba ya Tanzania na sheria ya vyama vya siasa kuruhusu shughuli za vyama vya siasa, tunazuia kwa kisingizio cha kujenga uchumi lakini mbaya zaidi zuio hilo linatekelezwa zaidi kwa vyama vya upinzani ambao ni ubaguzi wa wazi.

Nyerere alitaka watu wawe huru kutoa maoni yao ikiwamo kukosoa, lakini leo hii tuna sheria kama ya makosa ya mitandaoni ya 2015 ambayo inatumika kukandamiza uhuru wa maoni nab ado tunasema tunamuenzi baba wa taifa.

Tufike mahali tuhubiri uzalendo wa kweli ambao ni pamoja na kusema kweli na si uzalendo wa sasa ambao kupongeza na kusifu kiongozi ndio unachukuliwa kama uzalendo, hapana, baba wa taifa kana nukuu zilivyo alitaka viongozi wakosolewe.

Leo hii Taifa limegawanywa na likagawanyika kwa itikadi za kisiasa na bado kesho tutasema tunamuenzi baba wa taifa, mimi nafikiri huu ni wakati sasa wa kujitafakari na kutizama walipi tulipojikwaa na sio kutazama tulipoangukia.

Ni lazima watanzania wote bila kujali itikadi zetu tutambue kuwa amani tuliyonayo ni sawa na kubeba yai, ukiliacha likadondoka na kupasuka ndio basi huwezi kulirudisha lilivyokuwa, turudi katika misingi aliyotuachia Nyerere.

Turudi kwenye misingi yetu ya undugu, utu na kupendana kwa sababu ukitaka kujua taifa hili limegawanyika, nenda kwenye mitandao ya kijamii uone baadhi ya Watanzania wanavyofurahia na hata kuwaombea mabaya viongozi wetu au wenzao wenye itikadi tofauti.

Tunapoadhimisha Nyerere Day, hebu tuache unafiki katika kumuenzi Nyerere, kama kweli tunakubali ndio baba wa taifa la Tanzania basi tusione soni kuyaishi yale aliyoyahubiri kama amani, haki na kukataa ubaguzi wa aina yoyote.

0656600900