Tundu Lissu: Chadema haina mamlaka ya kufungua kesi ICC

Tundu Lissu: Chadema haina mamlaka ya kufungua kesi ICC

Muktasari:

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, Tundu Lissu amefafanua kwamba chama chake hakijafungua kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya The Hague (ICC), kwa sababu haina mamlaka ya kisheria ya kufanya hivyo.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, Tundu Lissu amefafanua kwamba chama chake hakijafungua kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya The Hague (ICC), kwa sababu haina mamlaka ya kisheria ya kufanya hivyo.

Amesema nchi wanachama ambao wametia saini mkataba wa Roma na mwendesha mashtaka mkuu wa ICC ndiyo pekee walio na mamlaka ya kisheria kufungua kesi katika Mahakama hiyo yenye makazi yake nchini Uholanzi.

Lissu ambaye alikuwa akizungumza wakati wa mjadala mtandaoni, alisema mchakato huo unaweza kukabiliwa na changamoto kubwa kutoka kwa wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambao wana nguvu ya kura ya Veto.

Katika ufafanuzi wake, Lissu alisema Chadema imewasilisha ushahidi juu ya matukio ambayo yanakidhi vigezo vya kuwa uhalifu dhidi ya ubinadamu ambao umefanywa ukilenga wanachama wa upinzani.

Tundu Lissu: Chadema haina mamlaka ya kufungua kesi ICC

Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Prof Adelardus Kilangi hivi karibuni alisema hakuwa anafahamu kama Chadema ilikuwa imeishitaki serikali katika Mahakama ya ICC kama alivyoeleza mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Lissu alisema ICC ambayo ilianzishwa mwaka 1999 inashughulika na aina nne za kesi ikiwa ni pamoja na zile zinazohusiana na mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu, uhalifu wa kivita na uchokozi baina ya mataifa.

“Ni jukumu la mwendesha mashtaka kuangalia kama ushahidi wetu unaendana na Kifungu cha 7 na 17 cha mkataba wa Roma ambao unabainisha aina za makosa ya uhalifu na kama yana uzito wa kutosha,” alisema.

Alisema uzitoo wa kutosha unapimwa na idadi ya waathirika, aina ya uhalifu na aina ya washtakiwa.

“Kwa hiyo, tumeorodhesha matukio ya mauaji, jaribio la mauaji ambalo lilinilenga huko Dodoma, kutoweka kwa watu, wengine kuwekwa rumande, kujeruhiwa pamoja na wahalifu kutoa taarifa zao kwa mwendesha mashtaka ili aamue,” alisema.

Aliongeza “lakini, hizi ni hatua za awali, kesi haitarajiwi kuanza leo au kesho kwa sababu kuna taratibu ambazo zinapaswa kufuatwa kwanza.

Akifafanua juu ya utaratibu, Rais huyo wa zamani wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS) alisema baada ya kuridhika na ushahidi, mwendesha mashtaka anaweza kwenda kwenye nchi husika kupata maelezo zaidi.

Alisema mwendesha mashtaka atatakiwa kupata idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lina wanachama 15, zikiwemo Uingereza, Marekani, Urusi, Ufaransa na China ambazo zina kura ya Veto.

“Changamoto ni kwamba wanachama wote wenye kura ya Veto wanatakiwa kukubali ili kesi hiyo ifunguliwe, jambo ambalo ni changamoto kubwa,” alikiri mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki.

Kwa mujibu wa Lissu, mbali na kuhitaji kuungwa mkono, makosa yaliyobainishwa yanapaswa kudhibitiwa kwa sababu siyo matukio yote ya mauaji ni uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Alisema uhalifu utambulike kama uhalifu dhidi ya ubinadamu, unapaswa kulenga kundi fulani la watu, unapaswa kuenea, unapaswa kurudia, unapaswa kuratibiwa na kutekelezwa na vikundi vinavyotambulika.

Akijibu swali kuhusu itakavyokuwa endapo nchi itaamua kujivua uanachama wa ICC kama ilivyotokea kwa Tanzania kujiondoka katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na (AfCHPR) iliyoko Arusha, LIssu alisema hiyo haitasaidia. “Nchi itashughulikiwa bila kujali hali yake ya uanachama kwa mujibu wa sheria za kitamaduni za kimataifa na mila ambazo zinakataza matukio ya uvamizi, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu,” alisema.

Alisema Tanzania imesaini mikataba mbalimbali ya kimataifa, jambo ambalo linaweza kuwa sababu nyingine ya kuendelea kukabiliwa na mashitaka hata kama itajitoa katika Mahakama hiyo.

Wakati wa hafla hiyo, wakili Jebra Kambole alisema mwendesha mashtaka wa ICC pia anaweza kuanzisha uchunguzi peke yake kama ilivyokuwa kwa Kenya, Burundi, Georgia n.k.

“Mwendesha mashtaka pia anaweza kuanzisha uchunguzi katika maeneo mengine ikiwa ni pamoja na kutoweka kwa watu, kuwekwa kizuizini pamoja na matukio ambayo hayakidhi viwango vya kimataifa na serikali haziko tayari au haziko tayari kuchunguza,” alisema.


Imeandikwa na Louis Columbia, Mwananchi