Twitter, WhatsApp zilivyokuwa na mijadala

Twitter, WhatsApp zilivyokuwa na mijadala

Muktasari:

  • Mitandao wa Twitter na WhatsApp jana ilikuwa na mijadala kuhusiana na hotuba aliyoitoa Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu Dar es Salaam, huku kwa asilimia kubwa wakimpongeza.

Moshi. Mitandao wa Twitter na WhatsApp jana ilikuwa na mijadala kuhusiana na hotuba aliyoitoa Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu Dar es Salaam, huku kwa asilimia kubwa wakimpongeza.

Hata hivyo, baadhi ya wachangiaji wameonyesha wanaona kauli ya Rais katika mfumo wa ukusanyaji kodi, unaweza usiwe na matokeo chanya kama serikali haitaanza kurekebisha sheria ili kuwepo kwa taasisi imara.

Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa, kwa hotuba aliyoitoa Rais akigusa mambo makuu matatu, hana haja ya kuongea tena mwaka mzima.

Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye aliandika: “Salamu bora kabisa isiyotugawa Watanzania kwa imani zetu,” huku akirejea salamu mpya ya Rais: “Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” na kujibiwa “Kazi iendelee.”

Mwanaharakati Fatma Karume maarufu kwa jina la Shangazi akaandika: “Following her speech today, the woman of the moment on Twitter republic is”, na kuweka picha ya Rais akimaanisha ndiye mwanamke wa nyakati hizi.

Mwanasiasa Godbless Lema anayeishi uhamishoni aliandika: “Kauli zako leo zina matumaini tena kwa uhuru wa habari na biashara. Ikiwa huu ndio mwelekeo wako sina shaka kuwa nchi itapona.”

Katika makundi ya WhatsApp, wachangiaji wengi waliona hotuba imebeba majibu ya manung’uniko ya muda mrefu hasa wateule kuendekeza kauli na vitendo vya ubabe.

Baadhi waliandika: “Hawa wakuu wa mikoa waliokuwa wanachapa watu viboko ngoja nao mama awanyooshe.”