Uamuzi waliotumia fedha za CWT kwenda mechi ya Taifa Stars kutolewa Mei 23

Muktasari:

  • Seif na Allawi wanakabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kutumia madaraka yao vibaya kwa kuchepusha Sh13.9 milioni ambacho ni mali ya CWT

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Mei 23, 2022 kutoa uamuzi kama aliyekuwa katibu mkuu wa Chama cha Walimu nchini Tanzania (CWT),  Deus Seif na mwekahazina wa chama hicho, Abubakari Allawi wanakesi ya kujibu au laa.

Seif na Allawi wanakabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kutumia madaraka yao vibaya kwa kuchepusha Sh13.9 milioni ambacho ni mali ya CWT.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutumia fedha hizo kwa ajili ya safari ya ndege kwenda Cape Verde, kuangalia mpira wa miguu kati ya Taifa Stars na timu ya Cape Verde kinyume cha sheria.

Uamuzi huo umetolewa leo Ijumaa Mei 13, 2022  na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Richard Kabate, baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao mashahidi tisa  na vielelezo 11 walivyotoa mahakamani hapo dhidi ya washtakiwa .

" Upande wa mashtaka wamefunga ushahidi wao hivyo nahitaji muda kidogo ili niweze kupitia na kuja kutoa uamuzi, hivyo Mei 23, kesi hii itakuja kwa ajili ya kutoa uamuzi, " amesema Kabate.

Kabla ya kuahirishwa kwa kesi hiyo upande wa mashtaka ukiongozwa na Iman Nitume akishirikiana na Veronica Chimwada walikuwa na shahidi mmoja, Faustine Mashauri ambaye ni mtaalamu wa maandishi kutoka Jeshi la Polisi.

" Mheshimiwa hakimu baada ya shahidi wetu huyu( Faustine) kumaliza kutoa ushahidi wake leo, naomba kuieleza mahakama kuwa upande wa mashtaka tumefunga ushahidi wetu," amedai wakili Nitume.

Baada ya kueleza hayo, hakimu Kabate aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 23, 2022 itakapoitwa kwa ajili ya mahakama kutoa uamuzi.

Katika kesi ya msingi, Seif na Allawi, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 39/2021.

Washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Oktoba 3, 2018 na Novemba 6, 2018 katika ofisi za CWT zilizopo Kinondoni wakiwa waajiriwa wa chama hicho walitumia mamlaka yao vibaya kwa kujipatia Sh13, 930,693.

Shtaka la pili, siku na maeneo hayo, Seif na Allawi kwa kutumia madaraka yao vibaya na kwa manufaa yao wenyewe wanadaiwa kuchepusha  Sh13.9 milioni ambacho ni mali ya CWT.

Viongozi hao wanadaiwa kutumia fedha hizo kwa ajili ya kulipia tiketi za ndege pamoja na kulipia gharama za malazi kwa ajili ya safari ya kwenda Cape Verde kuangalia mpira wa miguu.

Unadaiwa kuwa mwaka 2018, huko Cape Verde kulikuwa na mechi ya mpira wa miguu kati ya Timu ya Taifa ya Tanzania ( Taifa Stars), waliokuwa wanacheza na timu ya Taifa ya Cape Verde.

Washtakiwa kwa kufanya hivyo, wanadaiwa kwenda kinyume na vifungu vya 29 pamoja na 31 vya sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.