Uchaguzi Afrika Kusini funzo kwa vyama vilivyopigania uhuru

Muktasari:

  • Wanasiasa waeleza wapigakura wa sasa hawaangalii historia ya ukombozi, vyama vya upinzani vikijipanga, vina nafasi ya kushika dola.

Dar es Salaam. Vyama vya siasa vilivyopigania uhuru vimetakiwa kubadilika ili kuendana na hali ya sasa kuviwezesha kuendelea kushika dola, ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Hayo yameelezwa leo Juni 5, 2024 na wanasiasa na wachambuzi wa masuala ya siasa za kimataifa waliochangia mada katika mjadala wa Mwananchi Space ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ukijadili mada isemayo: Uchaguzi Afrika Kusini unatoa funzo gani kwa Afrika.

Mei 29, 2024 wananchi wa Afrika Kusini walifanya uchaguzi ambao ANC ilipata asilimia 40.18, ikifuatiwa na Democtaric Alliance (DA), asilimia 21.81, UMkhoto we Sizwe (MK), asilimia 14.58. Economic Freedom Fighters (EFF) asilimia 9.52, huku vyama vingine vidogo vikukusanya jumla ya asilimia 13.91.

Matokeo rasmi yanaonyesha ANC imeshinda viti 159 katika Bunge la Taifa lenye viti 400, ikishuka kutoka 230 vya awali kutokana na hali hiyo ANC italazimika kugawana madaraka na wapinzani.

Mwanasiasa Zitto Kabwe, amesema kwa wapigakura wa Afrika baada ya wimbi la kujikomboa, hoja ya kuleta ukombozi siyo hoja tena.

Zitto, mbunge wa zamani na aliyekuwa Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo amesema mtu aliyezaliwa mwaka 1994 baada ya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia Afrika Kusini, kwa sasa ana miaka 30  na katika kumbukumbu ya maisha yake hajaona utawala wa kikaburu bali anahadithiwa.

Amesema mtu huyo kwa sasa badala ya kufikiri kuhusu ukombozi, anaangalia kama baada ya kumaliza chuo amepata ajira.

“Chama cha ANC walikutana na kizazi ambacho hakikuona ubaguzi wa rangi, hili ni jambo ambalo chama hiki kilishindwa kujinyumbulisha kuendana na hali halisi ya Afrika Kusini ya sasa,” amesema.

Amesema wapigakura wa sasa hawapigii kura yaliyopita bali ya sasa na yajayo. ANC mbali na kukutana na watu wanaotazama mbele, amesema pia kilikosa ajenda.


Funzo kwa Tanzania

Zitto amesema uchaguzi wa Afrika Kusini unatoa funzo kwa nchi nyingine, Tanzania ikiwamo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kutambua Watanzania hawaiangalii kama mtoto wa TANU iliyoleta uhuru.

Zitto amesema kwa sasa uhuru si hadithi ambayo watu wanataka kuisikia,  bali namna ambavyo changamoto zinazowakabili zinatatuliwa.

Ni kutokana na hilo, amesema vyama vya upinzani vikisimama katika ajenda ambayo watu wataiamini, inawezekana kuviondoa vyama vikongwe madarakani.

“Wenzetu Zambia wamefanya hivi mara kadhaa,” amesema.

Hoja hiyo imeungwa mkono na Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Filbert Komu aliyesema awali Afrika Kusini, Waafrika wengi walikuwa wamebaki nyuma, kielimu, kimaarifa na maendeleo tofauti na sasa mambo yamebadilika.

Hali hiyo amesema imefanya vyama vinavyokuja na dhana ya kuwa wao ndio waleta ukombozi kuwa haina mashiko.

Mbali na hilo amesema: “Pengo ni kubwa kati ya walionacho na wasionacho nchini Afrika Kusini, ukienda katika maeneo kama Cape Town utaona walioshikilia uchumi ni wachache.”

Ezekiel Maige, aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, amesema ANC kimeshindwa kubadili ajenda kama vile hali ngumu ya maisha, ukosefu wa ajira na kuzishughulikia changamoto hizo.

Badala yake, amesema waliendelea kusimamia hoja ya kuwaondoa makaburu ambayo haiwezi kuwa na mashiko kwa sasa.

Amesema vyama vya ukombozi vinapaswa kujigeuza kuwa vyama vya uongozi.

“Kikubwa kinachopaswa kufanyika ni kubadili mtazamo kutoka chama kinachotawala hadi chama kinachoongoza watu,” amesema.

Vyama hivyo amesema vinatakiwa kuangalia shida zilizopo kwa wakati husika na kuzitafutia ufumbuzi.


Hoja ya kujiamini kupita kiasi, uchawa

Maige amesema kumekuwa na uzito kwa baadhi ya vyama kuchukua hatua stahiki kutokana na kujiamini kupita kiasi.

Amesema chama kikiwa na mfumo unaotengeneza mazingira ya watu kutokuwa wawazi au wa ‘machawa’ husababisha sauti za mawazo tofauti kutosikika.

“Hilo linatokana na watu wenye maoni tofauti kuzomewa na ‘machawa’ waliondaliwa, huku waliosema au kutoa hoja tofauti wakifikia hatua ya kutishwa,” amesema Maige na kuongeza:

“Unatengeneza mfumo wa kutojiamini kwa baadhi ya watu na wakati mwingine inafanya chama kushindwa kuchukua ajenda ambayo imezungumzwa kwa wakati huo.’’

Amesema hali hiyo inaweza kukifanya chama kupoteza mvuto kwa watu na kupunguza kura kwenye uchaguzi.

Mchangiaji katika mjadala huo, Begga Richard amesema vyama vingi vikongwe  badala ya kutumikia watu kwa muda waliokaa madarakani,  vimebaki kuelezea historia ya kupigania uhuru.

“Vijana wengi sasa hivi wanahitaji mabadiliko na si kuelezewa tulitawaliwa na watu fulani wakati wanaona kuna tatizo la umeme, ajira hakuna, inakuwa tatizo kwa vyama vikongwe kushindana katika uchaguzi.

“ANC katika chaguzi zijazo wataenda kupotea zaidi kwa sababu wananchi wengi wa kizazi cha sasa wanataka kuona mabadiliko si kusikiliza historia zinazotolewa na watu,” amesema.

Mchambuzi wa siasa za kimataifa, Ibrahim Rahby amesema kilichoiangusha ANC ni watu kutaka kuona mabadiliko, changamoto ya ukosefu wa ajira na hali ya usalama.

Mwanachama wa Chadema, Gervas Lyenda amedai kuwa jahazi la ANC linakwenda ukingoni, akisema kilichoathiri chama hicho ni Rais wa zamani wa Taifa hilo, Jacob Zuma kupunguza kura nyingi za ANC baada ya kuanzisha chama chake.


Kutotekeleza ahadi

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Hezron Kangarawe amesema wananchi wanaamua kuviadhibu vyama vikongwe kwa kwenda katika vyama vingine, kutokana na kushindwa kutekeleza kile ambacho wameahidi.

“Unaahidi watu utawapa hiki, utawapelekea kile umewapelekea? wananchi wanakuwa na matarajio kutoka kwako mwishowe inabaki kuwa hewa,” amesema.

Amesema vyama vya Afrika, hususani vikongwe vijiandae kwa kuwa ipo siku kama havitekelezi ahadi wananchi wataviondoa madarakani.

Dk Kangarawe amesema lingine la kujifunza ni kuwa, Afrika Kusini tangu mwanzo, ANC haikuwa na nguvu sana kama vile ilivyo kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) au Chama cha Wananchi (CUF).