Uchaguzi serikali za mitaa, Profesa Lipumba awafunda viongozi CUF

Muktasari:

Chama cha Wananchi (Cuf) kimeandaa semina maalumu kwa makatibu wake wa wilaya ili kupanga mikakati ya ushindi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24,2019.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (Cuf), Profesa Ibrahim Lipumba amewataka makatibu wa wilaya wa chama hicho kuzielewa sheria na kanuni za uchaguzi ili kuepesha Chama cha Mapinduzi (CCM) kupita bila kupingwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 24,2019.

Profesa Lipumba ametoa wito huo leo Jumapili Septemba 15,2019 jijini Dar es Salaam wakati akifungua semina maalumu kwa makatibu wa wilaya wa chama hicho kwa lengo la kupeana mikakati ya kushinda uchaguzi wa serikali za mitaa.

Amesema makatibu hao wakizijua kanuni husika wataweza kujua mianya ambayo inatumiwa na wenzao kujipatia ushindi.

Amewataka wasikubali hali hiyo itokee kwenye wilaya zao bali wasimamishe wagombea na kufuata sheria na kanuni za uchaguzi.

"Kazi yenu kubwa ni kujipanga kuweza kushinda, mnapaswa kujua maeneo yenu, mnapaswa kuzijua sheria na kanuni za uchaguzi. CCM wana mfumo wa 4.4.2, mkilala tu wanatangazwa bila kupingwa," amesema Lipumba.

Mwenyekiti huyo amesema ni muhimu makatibu hao wa wilaya kuitambua Katiba ya chama hicho pamoja na itikadi yake ya "Haki Sawa kwa Wote" ili kutekeleza kwa vitendo pindi wanapochaguliwa kwenye vitongoji, vijiji na mitaa.

"Lazima tuweke wagombea kwenye kila kitongoji, kila kijiji na kila mtaa. Hatuna mpango wa kuruhusu wapite bila kupingwa, nyie (makatibu wa wilaya) ndiyo mtakaofanikisha hili kwa kuhamasisha watu kugombea," amesema Profesa Lipumba.

Baadhi ya makatibu hao wamesema wako tayari kwenda kufanya kazi na kukipatia chama hicho ushindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaitarajiwa kufanyika Novemba 24, 2019.

Katibu wa wilaya ya Tabora mjini, Rehema Kabata amesema mwaka 2019 lazima washinde vijiji na mitaa mingi kwa sababu chama chao kina mikakati mizuri ya kukiwezesha kuibuka na ushindi kwenye uchaguzi huo.