UCHAMBUZI WA KITABU: Mwinyi hatawasahau Maalim Seif, Mrema na Mtikila katika utawala wake

Mwinyi hatawasahau Maalim Seif, Mrema na Mtikila katika utawala wake

Muktasari:

Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi ametaja baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani waliompa shida katika utawala wake akiwamo Katibu mkuu wa zamani wa CUF na baadaye mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad.

Dar es Salaam. Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi ametaja baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani waliompa shida katika utawala wake akiwamo Katibu mkuu wa zamani wa CUF na baadaye mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad.

Wengine ni Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema na aliyekuwa Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila. Mwinyi amebainisha hayo katika kitabu chake cha Mzee Rukhsa; Safari ya Maisha yangu kilichozinduliwa mwishoni mwa wiki na Rais Samia Suluhu Hassan.

Maalim Seif

Kupitia kitabu chake, Mwinyi amesema alianza kumfahamu Maalim Seif tangu wakati wa utawala wa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Alhaj Aboud Jumbe, kiongozi aliyeingia baada ya kifo cha Rais Abeid Karume mwaka 1972 na kumwibua Maalim Seif.

Mwinyi ameandika kuwa, Maalim Seif pamoja na vijana wengine walioibuliwa na Rais Jumbe, walikuwa wakijiita ‘Frontliners.’ Vijana hao walimgeuka baadaye, hivyo kumsababishia Jumbe kujiuzulu urais mwaka 1984.

Mbali na vijana, kundi la wazee wakati huo liliitwa ‘Liberators.’ Ametaja kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kilichofanyika Januari 24-30, 1984 Dodoma kuwa kilihitimisha safari ya urais wa Jumbe baada ya kushtakiwa kuwa alitaka kubadili Katiba ya Zanzibar na kutaka Muungano wa Serikali tatu.

Mbali na kikao hicho, Mwinyi pia amezungumzia kikao kingine cha NEC cha mwaka 1982 alichosema kilikuwa kigumu sana, kwa kuwa licha ya kupangwakufanyika kwa siku mbili kilikaa kwa siku tano, huku wajumbe wengi kutoka Zanzibar wakidai kuwepo kwa uhaini unaofanywa kwa siri.

 “Pamoja na kina Khatibu Hassan, kiongozi hasa wa mashambulizi dhidi ya Jumbe alikuwa Seif Sharif Hamad wakati huo akiwa mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na mkuu wa idara ya Uchumi na Mipango. Upande mwingine walijaribu kutetea lakini utetezi ulionekana hafifu.

“Cha kushangaza ni kuwa, leo hii Maalim Seif huyu huyu ndiye amegeuka kuwa kinara wa kudai Muungano wenye mfumo wa Serikali tatu zilezile alizomshambulia nazo Alhaj Abdoud Jumbe Mwinyi,” anasema Mwinyi.

Hatimaye, Alhaji Jumbe alijiuzulu nafasi yake kwenye chama na Serikali Januari 29, 1984, kisha Mwinyi akateuliwa kushika nafasi yake kama Rais wa Zanzibar kabla ya kufanyika uchaguzi baadaye alipochaguliwa rasmi na Maalim Seif akateuliwa kuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar.

 Chokochoko za Maalim Seif

Akiendelea kumwelezea Maalim Seif katika kitabu hicho, Mzee Mwinyi ameandika kuwa mwaka 1985 wakati wa Uchaguzi Mkuu, Maalim Seif aliyekuwa Waziri Kiongozi alijitokeza kugombea urais wa Zanzibar sambamba na aliyekuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi, Idrissa Abdulwakil.

Mwinyi hatawasahau Maalim Seif, Mrema na Mtikila katika utawala wake

Hata hivyo, ilitarajiwa Maalim Seif ambaye wakati huo alikuwa na miaka 42 amwachie Abdul wakil aliyekuwa na miaka 60, lakini haikuwa hivyo.

“Maalim Seif akakataa kujitoa, ikabidi wapigiwe kura za uteuzi wa ndani ya chama, alipata asilimia 80 ya kura kutoka kwa wajumbe wa Pemba na Sheikh Idriss Abdulwakil akapata kiasi hicho cha kura upande wa Unguja ila akamzidi idadi ya kura, hivyo ndiyo akawa mgombea urais wa Zanzibar,” anasema Mwinyi.

Mwinyi hatawasahau Maalim Seif, Mrema na Mtikila katika utawala wake

Hata hivyo, baada ya uchaguzi kufanyika, anasema matokeo yalionyesha kuwa wajumbe wa Pemba hawakufurahishwa na ushindi wa Abdulwakil.

Hivyo ili kuwaunganisha Wazanzibari iliamuliwa kuwa Maalim Seif aendelee kuwa Waziri Kiongozi.

Katika hali hiyo, Maalim Seif aliendeleza chokochoko kwa Rais Abdulwakil.

“Chokochoko zilianza kusikika tangu Julai 1987. Kilele cha kutoelewana baina yao kikafikiwa Januari 1988 na ikabainika kulikuwa na mpango wa Maalim Seif na Wizara ya Mambo ya Ndani nikampeleka Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo, pamoja na kuondosha hicho cheo cha Naibu Waziri Mkuu.

“Jambo hilo lilimkera sana na akazua visa kimoja baada ya kingine. Ilipofika mwaka 1995 aliona wazi kuwa hakuna uwezekano wa kugombea urais kupitia CCM.

Akaamua kujiuzulu uwaziri na kisha baada ya mwezi mmoja akahamia mojawapo ya vyama vya upinzani, NCCR Mageuzi kilichokuwa kinaongozwa na Mabere Marando,” anaeleza Mwinyi.

Akikichambua chama hicho, Mwinyi anasema kilijaa wasomi hasa wa sheria, lakini hawakuwa na uzoefu wa siasa, hivyo walimwona Mrema ni kivutio cha siasa zao.

Amewataja baadhi ya waliokuwa makada wa chama hicho mbali na Marando kuwa ni pamoja na Makongoro Nyerere (sasa amehamia CCM), James Mbatia, Masumbuko Lamwai na Prince Bagenda.

“Kuhama kwa Mrema na kusimama akiwa mgombea urais kupitia chama cha upinzani kulitusumbua sana kwenye CCM,” anaeleza Mwinyi.

Anakumbusha mkutano wa kumtambulisha Mrema uliofanyika Machi 25, 1995 Uwanja wa Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

“Uwanja ulijaa watu wakiwamo baadhi ya wana CCM waliorudisha kadi zao za chama na kumjaza Mrema matumaini ya kushinda na kufikia ndoto yake ya kuwa Rais wa Tanzania,” ameandika.

Mchungaji Mtikila Miongoni mwa wanasiasa wanaotajwa kuwa mwiba kwa Mwinyi ni Mchungaji Christopher Mtikila aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha DP.

Mwinyi amemtaja Mtikila kuwa alimkera zaidi katika eneo la chuki za kidini. “Mmojawapo wa watu waliokuwa mwiba kwangu alikuwa Mchungaji Christopher Mtikila. Kati ya watu waliokuwa na chuki dhidi ya Waislamu alikuwa huyu bwana,” ameandika Mwinyi.

Ameeleza jinsi alipomteua aliyekuwa Waziri wa Elimu, Profesa Kigoma Malima, Mtikila alimshambulia. “Mchungaji Christopher Mtikila alinishambulia sana kwa lugha isiyostahili kabisa, mtu anayesema ni kiongozi wa dini.

Ni kweli walikuwepo pia baadhi ya maaskofu waliopata wasiwasi kuona nimemteua Muislamu kuwa Waziri wa Elimu, lakini Mtikila alikuwa katika ligi ya peke yake,” ameandika Mwinyi.

Pia, ameeleza kuwa Mtikila alimwandikia barua Mwalimu Nyerere (Julius) katika mkutano mkuu wa Taifa wa CCM wa mwaka 1987 akidai kuwa Serikali inanyanyasa Wakristo, jambo alilosema lilikuwa la uongo na uzandiki.