Uchunguzi wabaini mengi mabadiliko tabianchi - Mwananchi

Dar es Salaam. Uchunguzi maalum uliofanywa na Gazeti la Mwananchi, umebaini athari nyingi zilizotokana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame uliosababisha kupaa kwa bei ya chakula na kufa kwa mifugo wafugwao.

Ripoti hiyo inayotarajiwa kuchapishwa hivi karibuni na gazeti hilo linaloongoza nchini Tanzania, ililenga kuangalia mabadiliko ya tabianchi na athati za ukame zinazosababishwa na hali hiyo.

Hayo yamesemwa leo Jumatano, Novemba 23, 2022 na mhariri mshauri, ujengezi uwezo na ushirikishwaji wa miradi maalum kutoka Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Rashid Kejo wakati akichokoza mada katika mdahalo wa TwitterSpace isemayo Tanznaia ni miongoni mwa mataifa yanayoathirika na mabadiliko ya tabia nchi, nini kifanyike.
Mjadala huo umehusisha watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa Serikali kama Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndani.
“Lengo ni kutafuta mwafaka tunatokaje hapa tulipo, Mwananchi tulifanya utafiti mdogo katika baadhi ya mikoa hasa kanda za kaskazini Kilimanjaro pamoja na mikoa ya Dodoma, Iringa na maeneo mengine kuangalia athari za ukame.”

“Tumebaini mifugo mingi inaathirika, wanyamapori na wale wafugwao wamepoteza maisha, isitoshe pia baadhi ya kaya zinashindia mlo mmoja nayo ni moja ya mambo yaliyobainika hasa maeneo ya ufugaji tuliwauliza inakuwaje mnashindia uji ilhali mifugo inakufa…

“Walisema hailiki, nyama yake inateleza haifai. Kilichotushtua zaidi hata baadhi ya maeneo bei ya gunia la mahindi limezidi bei ya ng’ombe ambayo ni Sh 130,000 lakini ng’ombe unapata kwa Sh70,000 hiyo inaonyesha ukubwa wa tatizo,” amesema Kejo.

Amesema uchunguzi umebaini maeneo mengi yameathirika na mabadiliko ya tabianchi maeneo ambayo yalipata maji ya asili hakuna tena yamekauka.

Kejo amesema utafiti pia umebaini uwepo wa uhusiano baina ya wanyama na binadamu ambalo nalo limechangia kwa kiasi kikubwa kuleta madhara katika mabadiliko ya tabia nchi.

“Pia tulibaini baadhi ya maeneo wametengeneza sheria ndogo ambayo inamlazimu mtu yeyote anayetaka kujenga nyumba ya kisasa lazima awe na choo na mfumo wa maji ili utumike kwa kuvuna maji, sasa maji mengi yanapotea katika msimu wa mvua,” amesema.

Mwakilishi wa vijana Delicia Mwanyika ameshauri, “cijana lazima tuwe pamoja na Serikali tufanye kazi pamoja na mfano Nemc watuongoze kuangalia maeneo ambayo wao wanaona ni kipaumbele ili kutoa motisha na nafasi kwa vijana kutoa maoni yao na kufahamu me ngi zaidi hasa malengo ya kimataifa.”