Udom kusuka mitalaa, yatamba kuzalisha wahitimu bora

What you need to know:

Chuo Kikuu cha Dodoma kimeanza mkakati wa kufanya mageuzi makubwa ya kitaaluma kupitia Mradi wa Elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi (HEET).

Dodoma. Chuo Kikuu cha Dodoma kimeanza mkakati wa kufanya mageuzi makubwa ya kitaaluma kupitia Mradi wa Elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi (HEET).

Mkakati huo umekuja katika kipindi hiki ambacho Serikali kwa ujumla imeanza kufanya mageuzi makubwa ya kuboresha mitaala ya elimu kama sehemu ya mkakati wake wa kuzalisha wahitimiza watakaokuwa na uwezo wa kujitegemea.

Jana Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Profesa Lughano Kusiluka alieleza mkakati wa mpango huo kwenye uzinduzi wa kamati za kukisaidia chuo kufanya maboresho ya mitaala.

Mradi wa HEET unafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa ajili ya kupitia mitaala ya vyuo na kufanyia maboresho kwa ajili ya kupata wahitimu wa viwango.

Profesa Kusiluka anasema lengo lao chuo hicho ni kufanya mageuzi makubwa yatakayopelekea uzalishaji wa wasomi wenye kukidhi soko la ndani na nje ya nchi ambao hawatakuwa na hofu nao.

“Tunahitaji wahitimu walioiva, tumekuwa tukishinda kwa wahitimu wetu kwenye maeneo mengi, lakini dunia inazunguka lazima tujipange kwenye mitaala yetu, nami nasema Udom iko tayari kwa mageuzi hayo,” amesema Profesa Kusiluka.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda alisema Tanzania ya sasa inahitaji wasomi wenye uelewa siyo wasomi wanaomaliza bila ujuzi.

Profesa Mkenda amewaambia washiriki na wasomi kuwa Wizara ya Elimu kwa upande wao wameshakamilisha mitaala ya kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita na vyuo vya ualimu na sasa wanapitia masahihisho.

Mratibu wa HEET Udom, Profesa Razack Lokina anasema mitalaa watakayoifanya itakuwa ni ya kisasa yenye kuifanya elimu ya mhitimu kuwa bora katika soko la ajira.

Kwa mujibu wa Profesa Lokina, Udom wako katika hatua nzuri na wanatumia wasomi kutoka maeneo tofauti na taasisi zinazotoa ajira ambazo wanapokea maoni ya aina gani ya wasomi wanaowataka soko la ajira.