UDSM kuanza kutumia mtalaa mpya 2024/25

Muktasari:

  • UDSM inatarajia kuanza kutumia mtalaa ulioboroshwa ifikapo mwaka wa masomo 2024-2025.

Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kinatarajia kuanza kutumia mtalaa ulioboroshwa ifikapo mwaka wa masomo 2024-2025.

 Hayo yamebainishwa leo Machi 13, 2023 jijini Dar es Salaam na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salam (UDSM), Profesa Bernadetha Killian katika warsha kwa watumishi wa chuo hicho  kuhusiana na mradi wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).

Alisema kwa sasa tayari wameshapokea maoni juu ya marekebisho ya mtalaa kutoka kwa wadau mbalimbali elimu, waajiri na wahitimu kutoka mikoa mbalimbali nchini ili kupata maoni juu ya mapungufu katika mtalaa unaotumika sasa.

"Warsha hii inalenga kuwapa watumishi wa idara mbalimbali zilizopo chuoni uelewa kuhusiana na maboresho ya mtalaa na wao kutoa maoni yao kisha maoni yote yaliyokusanywa yatafanyiwa upembuzi wa kina,"alisema.

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Heet katika upande wa uboreshaji mitaala, Profesa Joel Mtebe alisema mradi wa Heet unatarajia kupelekea maboresho katika maeneo makuu matatu.

Mtebe alibainisha maeneo hayo kuwa ni uboreshaji wa mitaala ili kusaidia kuzalisha wahitimu wanaoendana na soko la ajira lililopo sasa kitaifa na kimataifa, kuboresha mifumo ya kiteknolojia na utoaji wa elimu kwa njia ya mtandao.

"Kupitia mradi huo pia kunatarajiwa kufanyika kwa maboresho ya miundombinu na ujenzi wa kampasi mpya katika mikoa ya Lindi na Kagera," alisema.

Anasema anasema mradi huo unalenga kuifanya elimu ya juu iweze kuchangia katika mageuzi ya uchumi wa nchi kwa kuwajengea wahitimu.

HEET ni miongoni mwa miradi ya elimu inayotekelezwa nchini na kusimamiwa na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ukilenga kuleta mapinduzi katika elimu ya juu nchini  pamoja na kutolewa kwa elimu inayoendana na soko la ajira.