Uenyekiti wa CCM katikati ya siri nzito

Saturday May 01 2021
uenyekitipic

Rais Samia Suluhu Hassan

By Luqman Maloto

Wakati Taifa la Tanzania lilipotangaziwa kifo cha Rais John Magufuli, Chama cha Mapinduzi (CCM) kilitengeneza rekodi mpya. Kwanza, kuondokewa na Mwenyekiti wake, aliyekuwa bado akishika usukani.

Ikawa bahati mbaya kwamba wakati Mwenyekiti wake akifikwa na mauti, chama hicho hakikuwa na Katibu Mkuu. Rais Magufuli alimteua Dk Bashiru Ally kuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kabla ya uteuzi huo, Bashiru ndiye alikuwa Katibu Mkuu CCM.

uenyekitipic

Rais Samia Suluhu Hassan

Kwa muundo wa Katiba ya CCM, Katibu Mkuu kwa nafasi yake ya kuwa Mwenyekiti wa Sekretarieti ya chama, maana yake ndiye mtendaji mkuu, vilevile uhai wa chama. Hivyo, kwa vile chama kilimpoteza Mwenyekiti, ikawa bahati mbaya hata mtendaji mkuu hakuwepo.

Utamaduni wa CCM uko bayana kuwa Rais wa Tanzania anayetokana na chama hicho ndiye atakuwa mwenyekiti wa chama hicho. Na kwa vile Tanzania tangu kuzaliwa kwake hakuna chama kingine ambacho kimepata kushika nchi, imekuwa hivyo, Mwenyekiti wa CCM anakuwa na majukumu mengi ya nchi na Serikali kuliko ya chama.

Ingawa ibara ya 118 ya Katiba ya CCM inamtaka Mwenyekiti kuwa kiongozi mkuu wa chama na ndiye msemaji mkuu wa CCM, kwa majukumu, roho ya chama hicho huwa Katibu Mkuu, maana anakuwepo kila siku ofisini kuhakikisha chama kipo hai na shughuli zake zinaendelea. Siku chache kabla hajapotea kwenye uso wa jamii, Rais Magufuli alimteua Bashiru kuwa Katibu Mkuu Kiongozi. Akaacha wazi nafasi ya ukatibu mkuu CCM.

Advertisement

Ni kipindi ambacho, watu wakaanza kubashiri majina ya mtarajiwa wa ukatibu mkuu wa chama hicho, mithili ya wabashiri wa mechi za soka au mashindano mbalimbali.

Wengi ‘walibet’. Nani alishinda? Hakuna zaidi ya Mungu. Ni yeye aliye juu, aliamua kumchukua Magufuli kabla hajataja jina la Katibu Mkuu wa CCM aliyemtaka baada ya Bashiru.

Pengine aliyetarajiwa alishaambiwa. Je, akijisema leo kuwa aliambiwa na Magufuli kuwa ndiye angeteuliwa kuwa Katibu Mkuu nani atamuamini?

Bora kukaa kimya. Pengine Rais Samia alimtambua aliyetarajiwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM kwa matakwa ya Rais Magufuli. Inawezekana baada ya kumteua atatoboa siri hiyo. Kama hamjui basi itabaki kuwa siri. Inawezekana wote hawaijui lakini Mungu anaifahamu.

Mungu hana kawaida ya kutoa sauti ya moja kwa moja kuongea na waja. Hivyo, hata kama Samia anaweza kulala na kuota akizungumza na Magufuli, halafu katikati ya ndoto Magufuli akataja jina la mtu aliyemtaka awe Katibu Mkuu baada ya Bashiru, bado kwa sehemu kubwa Samia anaweza kupuuza na kuamini ni ndoto tu iliyomjia usingizini.

Magufuli aliiongoza Tanzania kwa zaidi ya miaka mitano, kadhalika CCM alikiongoza kwa takriban miaka minne na miezi nane, mtindo wake wa uongozi unafahamika. Hakuwa mtu wa kutoa siri zake haraka. Wengi aliowateua, walikiri kushitushwa, maana hawakuwa wametaarifiwa kabla.

Kwa kuchukua mtindo huo wa Rais Magufuli, inawezekana kwa asilimia kubwa hakuwahi kumwambia yeyote kuhusu aliyemkusudia kuwa Katibu Mkuu baada ya Bashiru.

Kwa maana hiyo, alipofariki dunia akaondoka nayo. Ni hapo utakiri kwamba binadamu hupanga lakini mwenye kuidhinisha mipango ni Mungu aliye juu.

uenyekitipicc

Kabla ya kumteua Bashiru kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, alimteua Humphrey Polepole, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM kuwa mbunge.

Uteuzi wa Polepole ulisababisha viulizo vingi kwenye vichwa vya Watanzania, hususan wachambuzi wa siasa. Wapo walioamini Polepole aliteuliwa kuwa mbunge kama hatua ya kuondolewa kwenye ukatibu wa Itikadi na Uenezi.

Hata hivyo, kuna waliootea kwamba Polepole aliteuliwa kuwa mbunge ili kuimarisha chama bungeni. Yaani, angeendelea kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, halafu kwa nafasi yake ya ubunge, angewezesha chama hicho kuwa imara bungeni, kwani Bunge la sasa kwa asilimia zaidi ya 90, ni la chama kimoja ambacho ni CCM.

Hiyo ya Polepole ni siri nyingine kama ambavyo ukatibu mkuu CCM baada ya Bashiru ulivyoacha maswali mengi kufuatia kifo cha Rais Magufuli. Utaona kwamba Samia anapokea uenyekiti wa CCM katikati ya siri nyingi. Ama Rais Magufuli alimwambia au kinyume chake, bado ni siri.

Uamuzi wa Rais Magufuli kumwondoa Bashiru kwenye ukatibu mkuu wa CCM, kwa vyovyote vile, ulitengeneza tafsiri kwamba alikuwa na kusudi la kuunda upya safu ya utendaji wa chama.

Si ajabu pia, hakumaanisha hivyo. Alitaka Bashiru aondoke, halafu ateue katibu mkuu mwingine, kisha timu ya sekretarieti iliyokuwepo wangeendelea kushika nafasi zao.

Je, Rais Magufuli alitaka kumpandisha cheo mmoja wa wajumbe wa sekretarieti ya sasa ya CCM kuwa Katibu Mkuu? Yote yanawezekana. Na kwa jumla, kila swali lisilo na majibu yaliyonyooka ndivyo inavyotimia tafsiri ya kwamba Rais Samia anachukua hatamu ya chama katikati ya siri nzito iliyoachwa na mtangulizi wake.

Utofauti wa Samia

Kama nilivyotangulia kueleza, Katiba ya CCM inaweka sharti kuwa Rais wa Tanzania atokanaye na chama hicho, ndiye anapaswa kuwa Mwenyekiti. Ni sharti hilo ndilo linalolazimisha Samia kuwa Mwenyekiti wa CCM.

Kama ambavyo Samia aliweka rekodi ya utofauti alipoapa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na CCM ni hivyohivyo. Kwanza, Samia anakuwa Mwenyekiti wa kwanza wa CCM mwanamke. Pili, anaweka alama ya kuwa Mwenyekiti aliyeshika nafasi hiyo baada ya kifo cha mtangulizi wake.

Tangu Tanzania ilipozaliwa, CCM kikarithi uongozi kutoka vyama vilivyokuwa vinaongoza dola; Tanu (Tanganyika) na ASP (Zanzibar), wenyeviti wake wote walistaafu, kisha mrithi akachukua kijiti.

Kwa hiyo, wakati CCM ikiandika rekodi, Samia anakuwa Mwenyekiti wa CCM wa kwanza kupokea kijiti cha mtangulizi wake aliyefariki dunia.

Pengine, nyakati zijazo akapatikana Mwenyekiti CCM atakayechukua nafasi baada ya mtangulizi wake kujiuzulu. Kwa sasa, Rais Samia anaandika ya kwake. Kuna wanaosema Rais Samia ni mwanamke mwenye bahati sana kwa kuangalia jinsi alivyopanda madaraka haraka hadi kuwa Rais. Wengine wanamtazama kama mwanamke wa rekodi zake.

Wanamwita mwanamke mwenye ‘namba moja nyingi’. Kwamba alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, halafu amekuwa Rais wa kwanza, kisha Mwenyekiti wa kwanza wa CCM ambaye maumbile yake ni mwanamke.

Swali kubwa ambalo wengi watakuwa wanajiuliza ni kwa namna gani atazielekea siasa za nchi? Wenyeviti wawili wa CCM waliomtangulia (Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete), kila mmoja kwa wakati wake walifanya maridhiano ya mara kwa mara na wapinzani wao wa kisiasa. Kipindi chao uhuru wa siasa za vyama ulikuwa mkubwa.

Magufuli, aliyeshika mpini baada ya Kikwete, mtindo wake wa uongozi ulisababisha ugumu mkubwa kwa vyama vya siasa kufanya shughuli zao, hasa mikutano ya hadhara. Magufuli hakufanya kikao cha maridhiano na wapinzani, licha ya kuandikiwa barua.

Swali ni je, Rais Samia baada ya kushika mamlaka ya chama, ataruhusu uwanja huru wa siasa kati ya CCM na wapinzani wake au atavibana vyama vingine ili kuruhusu chama chake kiwe na nguvu nyingi? Alishaahidi kukutana na wapinzani, lakini wakati huo alikuwa bado hajawa Mwenyekiti wa CCM.

Advertisement