Uganda ni mpambano wa rais wa ghetto na rais maisha

Uganda ni mpambano wa rais wa ghetto na rais maisha

Muktasari:

Jambo moja kubwa halijafanyika Uganda. Ni mabadilishano ya madaraka kwa njia ya amani.

Jambo moja kubwa halijafanyika Uganda. Ni mabadilishano ya madaraka kwa njia ya amani.

Kesho, Januari 14, Waganda wanatarajiwa kufanya uchaguzi ili kuchagua rais na wawakilishi wa wananchi watakaohudumia taifa hilo kwa miaka mitano ijayo.

Kama ambavyo ilitokea kwa Benedicto Kiwanuka, Mganda aliyerahisha mengi kuelekea uhuru wa Uganda, kuondolewa kwenye nafasi ya Waziri Kiongozi miezi sita kabla ya taifa hilo kupata uhuru kamili kutoka kwa Uingereza, hali imebaki kuwa tete.

Milton Obote na Kabaka Yeka Edward Muteesa II, walimuweka pembeni Kiwanuka, kisha wao wawili wakaongoza ushirikiano uliofanikisha uhuru kamili wa Uganda, Oktoba 9, 1962.

Baada ya hapo Uganda ikawa dola ya shirikisho. Dola ya Kifalme ya Buganda nayo ikashiriki katika muundo wa serikali.

Muteesa II akawa Rais (mkuu wa nchi asiye na mamlaka ya serikali), Obote akaukwaa uwaziri mkuu (mkuu wa serikali).

Obote akamtumia aliyekuwa Mnadhimu wa Jeshi la Uganda, Idi Amin Dada, kumuweka kando Muteesa. Baada ya hapo Obote akajitangaza kuwa Rais wa Uganda, akampandisha cheo Amin hadi Mkuu wa Majeshi.

Amin akampindua Obote, kisha uchokozi wa Amin Kagera ukasababisha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere amuondoe. Yusuf Lule, akaingia madarakani.

Lule akaondolewa madarakani baada ya kuiongoza Uganda kwa siku 68, halafu Godfrey Binaisa akashika mpini. Jeshi lilimpindua Banaisa, nafasi ikachukuliwa na Paulo Muwanga. Alidumu madarakani kwa siku 10, Obote akarejea madarakani.

Kwa mara nyingine Obote alipinduliwa, safari hiyo aliyempindua ni Bazilio Olara-Okello. Halafu, Yoweri Museveni akampindua Olara-Okelo.

Tangu Museveni alipoingia madarakani Januari 26, 1986, hajawahi kuachia ngazi. Inakwenda miaka 35 sasa. Hivi sasa, Museveni anaongoza taifa ambalo robo tatu ya raia wake hawakuwa wamezaliwa kipindi anachukua hatamu ya uongozi.

Uganda yenye watu wanaokisiwa kuwa milioni 45.7 kwa sasa, kati ya hao, watu milioni 34.3 hawakuwepo duniani kipindi ambacho Museveni anampokonya madaraka Olara-Okelo.

Na inawezekana karibia nusu ya watu waliokuwa wamezaliwa kipindi Museveni anashika mamlaka, na ambao bado wapo hai, walikuwa watoto wakiwa hawawezi kufanya uamuzi wowote.

Mfano halisi ni Robert Kyagulanyi ‘Bobi Wine’, mgombea urais Uganda kupitia chama cha NUP, kwa sasa ana umri wa miaka 38.

Kipindi Museveni anashika madaraka, Bobi alikuwa na umri wa miaka mitatu na miezi 11.

Uganda ni mpambano wa rais wa ghetto na rais maisha

Hivyo, hakuwa na uamuzi wala utambuzi wa kilichokuwa kinatokea kwenye taifa lake. Sasa hivi, Bobi ambaye umri wake si rika la walio wengi Uganda, ndiye mpinzani mkuu wa Museveni.

Kwa maana kwamba Bobi alipopata ufahamu wa kutosha kuhusu maisha na dunia, alikuta Museveni ni Rais. Leo hii Bobi ni baba wa familia, kiongozi na mwanamuziki maarufu, hajawahi kuonja ladha ya uongozi tofauti na Museveni.

Hivyo ndivyo walivyo Waganda zaidi ya milioni 40 kwa sasa. Ama hawakuwa wamezaliwa wakati Museveni anachukua madaraka au walishazaliwa lakini walikuwa watoto, kwa hiyo hawajawahi kushuhudia mtindo wowote wa uongozi tofauti na wa Museveni. Kwa kutazama hilo la Museveni kuwepo madarakani kwa muda mrefu, pili taifa la Uganda kutokuwa na historia ya mabadilishano ya uongozi kwa njia ya amani, Waganda wanayo nafasi ya kuamua, ingawa haidhaniwi kuwa uchaguzi utakuwa huru na haki kwa sababu ya historia za uchaguzi katika nchi za Afrika. Pamoja na kukaa madarakani kwa muda mrefu lakini Waganda wengi wanampenda Museveni kwa sababu uongozi wake uliwezesha mabadiliko makubwa. Aliifanya nchi hiyo kuwa ya amani baada ya nyakati nyingi za machafuko. Anasifika kwa kuijenga Uganda kiuchumi na kimiundombinu. Upande wa pili kuna vuguvugu la la kutaka mabadiliko. Vuguvugu hilo linambeba zaidi ya Bobi ambaye ni kijana, ambaye tangu alipochaguliwa kuwa mbunge mwaka 2017, alitokea kuwa alama ya siasa za harakati zenye kulazimisha mabadiliko makubwa ya kimfumo.

Museveni anachuana na wagombea 10 wa upinzani, lakini jina linatajwa sana ni Bobi ambaye anajiita Rais wa Ghetto. Hivyo, ni mpambano wa nguvu kati ya Rais wa Ghetto anayetaka urais halisi wan chi dhidi ya rais wa maisha.

Ndio, kwa mitazamo ya wengi, Museveni haonekani kuwa na mpango wa kuachia madaraka hivi karibuni. Endapo Museveni atashinda urais kesho na kukaa madarakani kwa muhula mzima, maana yake atafikisha miaka 40 madarakani.

Nyakati zimebadilika, alishindana mno na rafiki yake wa zamani, Kiza Besigye ambaye mwaka huu kaamua kujiweka kando na kuruhusu damu mpya kupeana changamoto na Museveni. Mwenyewe (Museveni) haonyeshi kuchoka.


Imeandikwa na Luqman Maloto, Mwananchi