Uganda yatangaza mlipuko wa Ebola

Muktasari:

  • Janga hilo linalotisha limesababisha vifo vya watu 11,000 na wengine 28,000 kuambukizwa katika eneo la Afrika magharibi kati ya mwaka 2014 na 2016.

Dar es Salaam. Serikali nchini Uganda imetangaza mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini humo baada ya mgonjwa wa kwanza kugundulika katika Wilaya ya Mubende iliyopo katikati ya nchi hiyo.

 Ebola ni ugonjwa wa hatari wenye uwezo wa kusababisha kifo kwa asilimia 90. Shirika la afya duniani, (WHO) linasema kwa mara ya kwanza ugonjwa huo ulibainika mwaka 1976 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na nchini Sudan.

Taasisi ya Utafiti wa Virusi nchini humo leo Jumanne, Septemba 20, 2022 imethibitisha mgonjwa huyo baada ya kupima sampuli iliyochukuliwa kutoka kwa mwanaume mwenye umri wa miaka 24.

Taarifa hiyo imetangazwa leo kufuatia uchunguzi wa timu ya taifa hilo ya kukabiliana na majanga kuhusu vifo sita vya kutiliwa shaka vilivyotokea wilayani humo mwezi huu, ambapo mpaka sasa watu wanane wanaendelea kupatiwa matibabu.

"Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja ambapo Uganda inarekodi mlipuko wa virusi vya ebola vya Sudan. Tunafanya kazi kwa karibu na mamlaka ya afya ya kitaifa kuchunguza chanzo cha mlipuko huu huku tukiunga mkono juhudi madhubuti za kudhibiti ugonjwa huu," Amesema Dk Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika na kuongeza;

"Uganda si mara ya kwanza kudhibiti Ebola, hatua zimechukuliwa kugundua virusi kwa haraka na tunaweza kutumia maarifa haya kukomesha kuenea kwa maambukizi."

WHO inazisaidia mamlaka za afya za Uganda katika uchunguzi huo na inatuma wafanyakazi katika eneo lililoathiriwa. Shirika limetuma vifaa kusaidia utunzaji wa wagonjwa na linatuma hema ambalo litatumika kuwatenga wagonjwa.

Chanzo cha kirusi hiki hadi sasa hakijulikani lakini popo aina ya (Pteropodidae) wanaonekana kuwa wabebaji wa kirusi hicho, kwa mujibu wa ushahidi uliopo sasa.

Mwaka 1976 katika milipuko miwili ambapo watu 151 walifariki katika eneo la Nzara na Sudan kusini huku watu 280 walifariki katika eneo la Yambuku karibu na mto Ebola uliopewa jina kutokana na ugonjwa huo.

Janga hilo linalotisha limesababisha vifo vya watu 11,000 na wengine 28,000 kuambukizwa katika eneo la Afrika magharibi kati ya mwaka 2014 na 2016.

Maswali bado ni mengi sababu za ugonjwa huo kurudi mara kwa mara na ni jitihada gani zinazochukuliwa kuzuiwa kurudi upya kwa janga lililoshuhudiwa Afrika magharibi ambapo sasa umerudi Afrika Mashariki.

Ugonjwa huo hauwezi kudhibitiwa, kwani unaweza kusambaa kwa kasi kupitia kugusa maji maji ya kutoka mwilini mwa muathiriwa.