Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uhaba wa sukari waanza kupatiwa ufumbuzi


Muktasari:

Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi chaanza uzalishaji, tani 1,851 zaingizwa sokoni.

Dodoma. Tatizo la uhaba wa sukari limeanza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu, baada ya mradi wa kiwanda cha Sukari cha Mkulazi kuanza uzalishaji wa jumla ya tani 1,851 ambazo ziko sokoni.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hayo bungeni leo Jumatano Aprili 3, 2024 alipowasilisha taarifa ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge na taasisi zilizo chini yake.

Amesema uzalishaji wa tani 1,851 za sukari ni hadi kufikia Machi, 2024.

Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi kilichopo mkoani Morogoro kinamilikiwa kwa ubia kati ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Jeshi la Magereza.

“Serikali imeendelea na ujenzi wa kiwanda cha sukari Mkulazi, ambao umefikia asilimia 99 kwa gharama ya Sh320.05 bilioni. Kiwanda hicho kimeanza uzalishaji Desemba 2023 na hadi kufikia Machi 2024, jumla ya tani 1,851 za sukari zimezalishwa na kupelekwa sokoni,” amesema.

Waziri Mkuu amesema, “Kuanza kwa uzalishaji kumeongeza kiwango cha upatikanaji wa sukari nchini na kuchangia kuongeza ajira, hadi sasa kiwanda kimetoa fursa za ajira 1,996. Matarajio ya kiwanda ni kuzalisha tani 50,000 kwa mwaka ifikapo mwaka 2026/2027.”

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Kilimo, mahitaji ya sukari nchini kwa matumizi ya kawaida na viwandani ni tani 655,000 kwa mwaka.

Uzalishaji wa sukari kwa mwaka nchini ni wastani wa tani 300,000 ambapo katika msimu wa mwaka 2020/2021 jumla ya tani 377,527 zilizalishwa na viwanda vilivyopo vya Kilombero Sugar Company Ltd, Mtibwa Sugar Estate, Kagera Sugar Ltd, TPC Ltd na Manyara Sugar Ltd.

Taarifa ya Wizara ya Kilimo ilibainisha mahitaji ya sukari yataendelea kuongezeka kutokana na ongezeko la vipato na idadi ya watu, mkakati uliopo ni kuongeza uzalishaji.

Serikali inaendelea kufuatilia mipango ya upanuzi wa viwanda vya Kilombero, Kagera na Mtibwa vinavyotarajiwa kuzalisha jumla ya tani 519,000 ifikapo mwaka 2024/2025.

Hivyo ukamilishaji wa viwanda hivyo na mchango wa uzalishaji kutoka kwenye miradi mipya ya Bagamoyo na Mkulazi, kiasi cha sukari cha tani 704,000 kinatarajiwa kuzalishwa katika kipindi hicho.

Kwa kuwa mahitaji ya sukari yatakuwa yameongezeka hadi kufikia tani 568,371 katika kipindi hicho, kiasi cha tani 704,000 kitatosheleza mahitaji ya nchi na kuwa na ziada ya tani 135,629.

Takwimu za Wizara ya Kilimo zinaonyesha uzalishaji wa sukari una uhusiano mkubwa na kiasi cha miwa kinachozalishwa. Kwa kawaida tani 10 za miwa huzalisha tani moja ya sukari. 

Miwa hiyo huzalishwa katika mashamba ya kampuni na wakulima wadogo, kwa sasa iwapo eneo lote lenye miwa lingevunwa, hekta 57,640 (viwanda hekta 37,624 na wakulima wadogo hekta 20,016), jumla ya tani 4,010,720 za miwa zingepatikana na kuzalisha tani 401,072 za sukari kwa mwaka.

Pia, taarifa hiyo ilibainisha Serikali kupitia Bodi ya Sukari Tanzania na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) itaendelea kutangaza maeneo yaliyoainishwa kwa ajili ya kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari ili kupata wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kwenye sukari.

Maeneo hayo ni ya Kibondo (hekta 25,000), Kasulu (hekta 37,000), Rufiji (hekta 25,000), Songwe (hekta 22,000), Mara (hekta 12,000), Mpanda (hekta 27,462), na Rukwa (hekta 12,372).

Maeneo hayo yana uwezo  wa kuzalisha hadi kiasi cha wastani wa tani 976,000 kwa mwaka.