Uhaba wa wahadhiri vyuo vikuu washtua

Thursday October 21 2021
uhabapic
By Jacob Mosenda

Dar es Salaam. Vyuo vikuu vya ndani vinakabiliwa na upungufu wa wahadhiri wenye sifa, kwa mujibu wa wakuu wa vyuo.

Siri hiyo imefichuliwa wakati wadau wa elimu wakieleza wasiwasi kuhusu ubora wa wahitimu hapa nchini.

Akizungumza katika mkutano ulioikutanisha Serikali, makamu wakuu wa vyuo na wadau muhimu wa elimu Dar es Salaam hivi karibuni, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Lughano Kusiluka alisema shida hiyo bado haijashughulikiwa.

“Tumeshuhudia katika maeneo mengine wafanyakazi wakiajiriwa mara kwa mara, lakini inaonekana vyuo vikuu vimesahaulika kidogo. Tunaomba eneo hili pia likumbukwe,” alisema Profesa Kusiluka.

Akijibu ombi hilo, Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako aliiambia Mwananchi kuwa, changamoto hiyo inajulikana na kuna mfuko utakaotoa ufadhili wa masomo kwa wahadhiri 1,000 ili kuwawezesha kupata sifa za kufundisha vyuo kikuu.

“Hii ni moja ya hatua tunazochukua kuhakikisha elimu inayotolewa na vyuo vyetu ni bora, hivyo lazima tupate suluhisho kwa changamoto hizi,” alisema Profesa Ndalichako.

Advertisement

Katika miaka miwili iliyopita, takwimu za Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) zinaonyesha kuwa wafanyakazi wa vyuo vikuu wameongezeka kutoka 6,238 mwaka 2019 hadi 7,187 mwaka 2020.

Wakati huohuo, uandikishaji wa wanafunzi umekuwa ukiongezeka kwa wastani wa asilimia 4.7 kwa mwaka kutoka wanafunzi 177,963 katika mwaka wa masomo 2017/18 hadi wanafunzi 206,305 mwaka 2020/21.

Hali ya sasa kwa mujibu wa takwimu za TCU, katika programu nne za Elimu, Sheria, Sayansi ya Tiba na Afya, Sanaa pamoja na Biashara, kumekuwa na tofauti ya idadi ya wanafunzi na wahadhiri inayoelezea upungufu uliobainishwa.

Mwaka 2019, Programu ya Elimu iliandikisha wanafunzi 54,156 (wahadhiri 524), Sayansi ya Tiba na Afya ilikuwa na wanafunzi 23,374 (wahadhiri 802). Programu za Sanaa zilikuwa na wanafunzi 6,345 (wahadhiri 616), Sheria wanafunzi 12, 424 (wahadhiri 205) na Biashara ikiandikisha wanafunzi 28,300 kwa wahadhiri 466.

Kufikia mwaka 2020 Programu ya Elimu ilikuwa na wanafunzi 51,489 na wahadhiri 708, wakati Sayansi ya Tiba na Afya ilikuwa na wanafunzi 24, 642 na wahadhiri 1,134. Programu ya Biashara ilikuwa na wanafunzi 107,913 kwa wahadhiri 729.

Kwa mujibu wa TCU, hadi kufikia 2020 kulikuwa na jumla ya wahadhiri 7,187 katika taasisi za vyuo vikuu.

Kati yao 4,863 walikuwa katika vyuo vikuu vya umma na 2,324 katika vyuo vikuu binafsi. Miongoni mwao, 5,088 ni wahadhiri wa kiume na 2,099 wanawake.

Wadau wa elimu walisema kama mambo hayo hayataangaliwa na kushughulikiwa ipasavyo, ubora wa elimu nchini utaporomoka kwa kasi.

Dk Thomas Jabir ambaye ni mshauri wa masuala ya elimu, alisema kumekuwa na ongezeko la vyuo vikuu lakini ongezeko hilo halilingani na ongezeko la rasilimali watu.

Kwa mujibu wa TCU, hadi Februari 2016, Tanzania ilikuwa na jumla ya vyuo vikuu 33 vya umma na vya binafsi, idadi ambayo imeongezeka hadi kufikia vyuo vikuu 47, vya umma 19 na 28 vya binafsi.

“Kuzalisha mwenye PhD huchukua muda mrefu na ni ghali pia. Inaweza kuchukua hadi miaka 10 au 12 kupata moja,” alisema Dk Jabir.

Ripoti ya 2017 ya Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU) ilikuwa imebainisha uhaba wa wafanyakazi wa masomo katika taasisi za elimu ya juu nchini kuwa asilimia 44.

Ripoti hiyo, ilibainisha kuwa, asilimia 53 ya wafanyakazi wa ngazi za juu waliokuwa wakifundisha katika vyuo vikuu walikuwa wamestaafu na walikuwa wakifanya kazi kama wafanyakazi waliopewa mikataba.

Advertisement