Uhakiki wa mali wachelewesha makubaliano kesi ya Sh5.7 bilioni
Muktasari:
- Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa yao kati ya Agosti 30, 2024 na Juni 28, 2025, makao makuu ya benki ya Equity Tanzania Limited yaliyopo Ilala, ambapo waliiba jumla ya Sh5.7 bilioni mali ya benki hiyo.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha hadi Juni 22, 2026 kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili washtakiwa wanane wanaodaiwa kuisababishia Benki ya Equity Tanzania hasara ya zaidi ya Sh5.7 bilioni, baada ya Jamhuri kueleza kuwa bado inahakiki mali zilizowasilishwa na mmoja wa washtakiwa kwa ajili ya makubaliano ya kumaliza kesi.
Akizungumza leo Juni 9,2026 Wakili wa Serikali, Titus Aron, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga, amesema majadiliano ya kumaliza kesi kati ya Jamhuri na mshtakiwa Fredrick Ogenga yanaendelea, huku mali alizowasilisha zikiendelea kufanyiwa uhakiki kabla ya kukamilisha makubaliano hayo.
Aron ameiomba Mahakama ipange tarehe nyingine ili kukamilisha mchakato huo, huku wakili wa utetezi, Meshack Dede, anayemtetea Fredrick, akiomba tarehe ya karibu zaidi kwa masilahi ya mteja wake. Hakimu Kiswaga ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 22, 2026 na washtakiwa wakaendelea kubaki rumande kutokana na shtaka la utakatishaji fedha kutokuwa na dhamana.
Mbali na Fredrick, washtakiwa wengine ni Jasmine Elphas, aliyekuwa ofisa wa Benki ya Equity, pamoja na Halifa Maina, Kaizilege Mohamed, Daudi Fata, Mrisho Mrisho, Neema Paul na Jefferson Ogenga, wote wafanyabiashara.
Kwa mujibu wa mashtaka, washtakiwa hao wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu na kujipatia zaidi ya Sh5.7 bilioni kwa udanganyifu dhidi ya Benki ya Equity Tanzania Limited kati ya Agosti 2024 na Juni 2025.
Jasmine na Fredrick wanadaiwa kuiba Sh3.6 bilioni kutoka akaunti ya clearing and settlement ya benki hiyo iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Washtakiwa wengine wanadaiwa kuhusika katika wizi wa fedha mbalimbali za benki hiyo zikiwemo Sh728 milioni, Sh758 milioni, Sh211 milioni, Sh101 milioni, Sh57 milioni, Sh32 milioni na Sh26 milioni.
Mbali na mashtaka ya wizi na kuongoza genge la uhalifu, washtakiwa wote pia wanakabiliwa na mashtaka 10 ya utakatishaji fedha yanayohusiana na fedha hizo zinazodaiwa kuibwa.