Uhamisho wa Chalamila, Makalla gumzo

Dar es Salaam. Panga pangua ya wakuu wa mikoa iliyofanyika juzi imezua mjadala, huku gumzo zaidi likimhusu Albert Chalamila, aliyehamishiwa Dar es Salaam kutoka Kagera, ambaye wadau wamemtaka awe msikilizaji na ajenge uongozi shirikishi ili afanikiwe.

Wamebainisha hayo jana, ikiwa ni siku moja tangu Rais Samia Suluhu Hassan awabadilishe vituo vya kazi wakuu wa mikoa wanne, akiwemo Chalamila anayekwenda kuchukua nafasi ya Amos Makalla anayehamishiwa Mwanza.

Wengine waliobadilishwa vituo vya kazi ni Adam Malima aliyekuwa Mwanza sasa anakwenda Morogoro akichukua nafasi ya Fatma Mwassa, anayekwenda Kagera kushika mikoa ya Chalamila.

Macho ya wengi yalimulika uhamisho huo kwa Mkoa wa Dar es Salaam, kitovu cha biashara nchini kwa sababu mbili, moja kuhamishwa kwa Makalla katika mgomo wa wafanyabiashara na kupelekwa kwa Chalamila ambaye matukio na aina yake ya uongozi mara nyingi huibua mjadala.

Katika uongozi, Chalamila amekuwa akipanda na kushuka, lakini wakati wote akionekana mwenye nidhamu.

Juni 11, 2021, Rais Samia alitengua uteuzi wa Chalamila alipokuwa mkuu wa mkoa wa Mwanza kutokana na kauli aliyoitoa ya kuhamasisha wananchi kubeba mabango kwenye ziara ya Rais Samia katika mkoa wake.

Hata hivyo, Julai 28, mwaka jana, Rais Samia alimteua tena kuwa mkuu wa mkoa wa Kagera, ikiwa ni karibu mwaka mmoja tangu alipoondolewa kwenye kazi hiyo ambayo amekuwa akiifanya kikamilifu licha ya maneno yake ya mzaha.

Chalamila amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini na kumteua tena, huku akisema ana deni la kuimarisha imani hiyo kwake.

“Awali ya yote namshukuru Mungu kwa wema wake kwangu na familia. Namshukuru sana Rais kwa imani yake kwangu...Nina deni la kufanya kazi na kuimarisha imani ya Rais kwangu,” alisema Chalamila.

Mkuu wa mkoa wa zamani wa Dar es Salaam, Yusuf Makamba amefananisha mabadiliko hayo ya wakuu wa mikoa kama kocha wa mpira anapofanya mabadiliko ya wachezaji wakati mchezo ukiendelea.

“Hivi…kocha wa Simba akimtoa (Clatous) Chama na kumwingiza Kibu (Denis) unahoji? Yeye mwenyewe kocha, akimtoa huyu na kumwingiza mwingine ni siri yake. Ataulizwa wakati amefanya mabadiliko na magoli hayaingii,” alisema Mzee Makamba, ambaye ni shabiki wa Simba na kuongeza:

“Rais ni kocha, ili magoli yafungwe zaidi unafanya mabadiliko ukiona hayafungwi. Sasa ni wachezaji hawa waliofanyiwa mabadiliko wanapaswa kuhakikisha magoli yanafungwa.”

Hali ilivyo Dar

Chalamila amehamishiwa Dar es Salaam katika kipindi ambacho kuna mgomo wa wafanyabiashara wa Kariakoo wanaolalamikia kodi mbalimbali na utaratibu wa kuzikusanya.
Licha ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwasihi juzi wafanyabiashara hao kusitisha mgomo wao, baadhi waliendelea nao hadi jana.

Awali, katika mgomo huo, Makalla alifika na kuzungumza na wafanyabiashara hao, huku akiwataka wajumbe kusafiri naye kwenda Dodoma kwa ajili ya kikao na Waziri Mkuu, jambo ambalo walilikataa.

Msimamo huo wa wafanyabiashara unaonyesha kwamba Makalla alishindwa kutatua changamoto za wafanyabiashara hao mapema kabla hawajaamua kufunga maduka yao, uamuzi ulioathiri makusanyo ya mapato na siku hiyo Rais Samia akamtoa na kumteua Chalamila.

Wakizungumzia uteuzi huo, wadau mbalimbali walieleza matarajio yao kwa Chalamila, huku wakimtaka awe anawasikiliza anaowaongoza sambamba na kushirikiana na viongozi au taasisi nyingine badala ya kwenda mwenyewe.

Mtaalamu wa uchumi, Oscar Mkude alisema changamoto ya kwanza ambayo anakutana nayo Chalamila ni ya mgomo wa wafanyabiashara Kariakoo kwa sababu hakukuwa na kusikilizana kwenye madai yao.

“Nafikiri lazima aweke mechanism (mifumo) ambayo inafanya awe anasikiliza. Majiji kama haya ndiyo yana structures (miundo) za wafanyabiashara na wafanyakazi. Kiongozi lazima awe hodari wa kusikiliza na wakati anasikiliza awe tayari kuangalia hali halisi,” alisema.

Alisema viongozi wengi wamekuwa wakifeli kwa sababu wanafanya uamuzi wakijifunga kwenye sheria na kanuni bila kuangalia halisi halisi.

“Uongozi unataka mtu ambaye atakuwa tayari kutafsiri mazingira na kufanya uamuzi sahihi,” aliongeza.

Alisema siku hizi watu wanataka kuwa sehemu ya mchakato wa kufanya uamuzi, hasa katika masuala yanayowagusa moja kwa moja, hivyo wasipopata hiyo nafasi wataanzisha mgomo kama wa Kariakoo.

“Dar es Salaam ni jiji kubwa lenye mambo mengi na Chalamila anao wajibu mkubwa wa kuhakikisha anaweka balance (mizania), ni rahisi kusema lakini kwenye utekelezaji inahitaji teamwork (kufanya pamoja),” alisema.

Mwanahabari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Absalom Kibanda alisema Rais Samia aliwahi kumwambia Chalamila kwamba “akue”, sasa atakuwa ameona amekua, ndiyo maana amemhamishia Dar es Salaam ili aje apambane na changamoto zake.

Alisema amemteua Chalamila akiamini kwamba ataweza kuhimili mikikimikiki ya kisiasa katika mkoa huo uliojaa mambo mengi tofautitofauti.

“Chalamila anakuja kusimamia utekelezaji wa uamuzi ambao utafanywa na ama Waziri Mkuu au Rais. Watu wengi tunaamini kwamba Makalla alishindwa kuusimamia mgomo wa Kariakoo, hiyo kazi kapewa Chalamila,” alisema.

Alisema si mara ya kwanza kwa Chalamila kwenda kusahihisha mapito ya Makalla. Wakati wa awamu ya tano baada ya Makalla kuonekana ameshindwa Mbeya, Chalamila ndiyo alikwenda kupokea kijiti chake na akaleta mabadiliko makubwa mkoani humo.

“Kwa sababu huyu ni mzungumzaji mzuri, pengine ile kamati ya ulinzi na usalama itapata msukumo katika kuhakikisha mkoa unakuwa salama na shughuli zinafanyika,” alisema Kibamba, ambaye ni mwenyekiti wa zamani wa Jukwaa la Wahariri Tanzania.

Kwa upande wake, mhadhiri wa Chuo cha Serikali za Mitaa (Hombolo), Charles Matekele alisema Chalamila ana kazi kubwa ya kutumia diplomasia ya kijamii na kiuchumi na pia kuangalia masilahi ya Taifa na yale ya wafanyabiashara.

Alisema anaamini kwamba atakuwa amejifunza kutoka kwa mtangulizi wake (Makalla) pale alipoishia na namna ya kusonga mbele kwa kurekebisha yale ambayo hayakwenda vizuri na kufanikiwa.

“Mkuu wa mkoa anatakiwa afanye kazi kwa ukaribu sana na Taasisi mbalimbali kama vile TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) lakini pia wafanyabiashara, wakiwa na mtazamo wa kukaa pamoja kujadiliana changamoto zilizopo,” alisema.

Kuhusu changamoto ya usalama na kuwepo kwa panyarodi, Matekele alisema mkuu wa mkoa ashirikiane kwa karibu na Jeshi la Polisi, ulinzi shirikishi pamoja na vyombo vingine vya usalama ili kumaliza tatizo hilo.

Kuhusu suala la kuwapanga wamachinga, alisema ni jambo ambalo likifanyika kikamilifu lina tija kubwa kwa sababu wataweza kutambulika kirahisi na kuchangia uchumi wa Taifa na kuongeza mvuto wa fedha kwenye masoko.
 

Atua Dar, aanza kazi

Jana jioni zilisambaa picha na sauti kwenye mitandao zikimwonyesha Chalamika akiwa katika eneo la Mwenge akipita kupita kwenye maduka mbalimbali kuangalia athari iliyosababishwa na mgomo wa wafanyabiashara wa Kariakoo.

Chalamika anasikika akisema ingawa hajaingia ofisini, ametamani kujua mtaani watu wanasema nini na maeneo mengi aliyopita kinacholalamikiwa ni kodi kubwa isiyowezekana kulipwa wakati Kodi ya Ongezeko la thamani (VAT) ni asilimia 18.

Amesema eneo lingine ni idara ya forodha imeweka viwango vikubwa vya kodi hasa kwa vitenge pamoja na ufuatiliaji kuwa mgumu jambo linalokwamisha biashara zao.
 

Malima na Mwanza

Siku 267 za Adam Malima mkoani Mwanza zimejaa kumbukumbu chanya na hasi kulingana na mitazamo, hisia na maoni ya watu tofauti, wakiwemo watumishi wa umma, viongozi wenzake na wananchi wa kawaida.

Pia, wadau hao wamebainisha changamoto zitakazomkabili Makalla mkoani humo, ikiwemo kuhakikisha wafanyabiashara wamachinga wanafanya biashara zao katika maeneo yaliyotengwa.

Malima ni miongoni mwa wakuu wa mikoa waliohamishwa vituo vya kazi juzi kutoka Mwanza kwenda Morogoro kujaza nafasi ya Mwassa, ambaye amekwenda Kagera.
Katika utumishi wake wa siku 267 ndani ya Mkoa wa Mwanza, uongozi wa Malima ametawaliwa na mambo mengi chanya na hasi ambayo wadau wanasema yanampambanua kama kiongozi anayefanya uamuzi.

Udhibiti wa fedha za Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU 1984) zinazohifadhiwa kwenye akaunti maalumu na kusimamiwa na Serikali (Escrow) ni miongoni mwa mambo yatakayoendelea kusalia kwenye kumbukumbu ya wana ushirika huo.

Katika eneo hilo, Malima alisimama kidete kudhibiti zaidi ya Sh2 bilioni zilizohifadhiwa kwenye akaunti hiyo kwa kumwagiza Mrajisi Msaidizi wa Ushirika Mkoa wa Mwanza, Lucas Kiondere kusimamia uandaaji wa taarifa za fedha za NCU kabla ya kuziruhusu zianze kutumika.

Akizungumza katika moja ya mikutano ya wana NCU, Malima hakupepesa macho baada ya shinikizo la kutaka fedha hizo zianze kutumika, bila kumung’unya maneno alisimamia uamuzi wa Serikali wa kuendelea kuzuia fedha hizo hadi taarifa za fedha za ushirika zitakaporidhisha.

Licha ya kuwahakikishia wanaushirika kuwa fedha hizo ni mali yao na hazitachukuliwa na yeyote, mkuu huyo wa mkoa anayeondoka alisisitiza maboresho kiutendaji na mipango thabiti ya matumizi ya fedha hizo kwa maendeleo ya wana NCU.

Uuzaji wa viwanja viwili vilivyoko katikati ya Jiji la Mwanza kwa Sh1 bilioni uliofanywa na uongozi wa Jiji la Mwanza kinyume cha maelekezo yake na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Nyamagana uliowang’oa viongozi na watendaji wa jiji ni kumbukumbu nyingine chanya ambayo Malima ameiacha Mwanza.

Ingawa sababu za kutenguliwa kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Yahaya Selemani hazikutajwa, lakini wengi wanaamini huenda sakata la viwanja hivyo ambalo vilisababisha watumishi wanne wa jiji kusimamishwa kazi lilichangia.

Hata hivyo, kwa baadhi ya viongozi wa wilaya na halmashauri za Mwanza, kuondoka kwa Malima huenda ni faraja kwao, hasa katika eneo la kutunza na kuheshimu muda kutokana na kiongozi huyo kuwa na kawaida ya kuchelewa kwenye matukio kuanzia vikao vya ndani na mikutano ya nje.

Mmoja wa mtumishi mkoani Mwanza aliyeomba jina lihifadhiwe alisema kuna wakati walilazimika kukaa kwenye vikao hadi saa 8 usiku, jambo ambalo watumishi wengi liliwakwaza.

“Tulishazoea kufanya vikao hadi usiku wa manane kwa sababu mkuu alikuwa anafika saa 10:00 jioni kwa shughuli ambayo ratiba yake ilipaswa kuanza saa 3:00 asubuhi.
“Kuna siku tulikaa ukumbini hadi saa 8:00 usiku baada ya RC kufika saa 12:00 jioni, wakati kikao kilitakiwa kianze saa 4:00 asubuhi,” alisema mmoja wa watumishi wa halmashauri ya Buchosa kwa sharti la kutotajwa jina lake, suala ambalo liliungwa mkono na mtumishi mwingine.

Suala la uchafu mitaani na watoto wanaoishi katika mazingira magumu, baadhi wakiombaomba hadi kwenye mzunguko wa barabara ya Nyerere na Kenyatta, hatua zisizozidi 100 kutoka ofisini kwake na hatua chini ya 50 kutoka Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ni eneo lingine linalotajwa kumshinda Malima akiwa Mwanza.

Jitihada za kumfikia Malima kupata maoni yake jana hazikufanikiwa baada ya simu yake ya kiganjani kutokuwa hewa. Ujumbe aliotumiwa kupitia mtandao wa WhatsAPP pia haukujibiwa, licha ya kuonekana umepokelewa.

Hata hivyo, suala la kuwapanga na kuhakikisha wafanyabiashara wamachinga wanasalia katika maeneo waliyotengewa limetamkwa kama kiporo kinachomsubiri Makalla kuendelea nacho.

Hii ni baada ya wafanyabiashara hao kuanza kurejea katikati ya jiji kutokana na miundombinu ya maeneo waliyotengewa kutokuwa rafiki.

“Ukifika pale Mchafukuoga (moja ya soko ya wamachinga jijini Mwanza) utakuta meza nyingi ni tupu, wafanyabiashara wameondoka na kurejea katika maeneo walikoondolewa.

“Changamoto kubwa inayotajwa ni miundombinu duni; hakuna mifereji ya kupitishia maji. Mvua ikinyesha maji hutuama kwenye vibanda vyetu na kutusababishia hasara,” alisema Wilson Mtakulu, mmoja wa wamachinga eneo la Mchafukuoga.

Marietha John, mkazi wa Mtaa wa Igogo jijini Mwanza alitaja uchafu kurundikana mitaani licha ya wananchi kutozwa Sh2,000 za kuzoa taka kila kaya kwa mwezi.

“Mifereji ya maji barabarani imejaa takataka kwa sababu magari ya taka hayapiti mitaani kukusanya taka. Hii ni kero tunayomtarajia Mkuu mpya wa mkoa ashughulikie,” alisema Marietha.

Imeandikwa na Peter Elias na Fortune Francis (Dar), Saada Amir (Mwanza) na Alodia Dominick (Bukoba)