Ujenzi daraja Mto Wama, ahueni ya wana-Rombo
Mmoja wa wakimbiza mwenge Kitaifa akipima upana wa daraja la Mto Wama, Wilaya ya Rombo, ili kujiridhisha kama vipimo viko sawa. Picha na Florah Temba
Muktasari:
- Kukosekana kwa daraja katika Mto Wama, kulisababisha changamoto mbalimbali hususani kipindi cha Mvua ambapo wajawazito walibebwa kwa mikono kuvushwa upande wa pili huku wazazi wakihofia usalama wa watoto wao na kuwazuia kwenda shule.
Rombo. Adha ya kuwabeba wagonjwa na kuwavusha Mto Wama, Wilaya ya Rombo, Kilimanjaro imefikia tamati baada ya Serikali kukamilisha ujenzi wa daraja linalounganisha vijiji vya Wama, Msangai na Nanjara wilayani hapo, uliogharimu Sh131.5 milioni.
Kukosekana kwa daraja katika Mto Wama, kulisababisha changamoto mbalimbali hususani kipindi cha Mvua ambapo wajawazito walivushwa kwa kubebwa mikononi huku wazazi wakihofia usalama wa watoto wao na hivyo kuwazuia kwenda shule.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, leo Juni 22, 2023, wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru ulipofika kuzindua daraja hilo, baadhi ya wananchi wamesema hatua hiyo itawarahisishia huduma za usafiri kwa kuwa magari yataweza kupita bila shida.
Nicholaus Mushi mkazi wa Nanjara Kibaoni amesema katika mto huo palijengwa daraja la miti ambalo lilihatarisha usalama wa wananchi na wanafunzi hususani kipindi cha mvua.
"Eneo hili palikuwa pabaya sana, wakati mwingine watu waliangukia mtoni wakati wanapita na hata pikipiki, lakini kwa sasa baada ya matengenezo kufanyika, mambo yamekuwa mazuri na magari yanaweza kupita kwa urahisi kabisa," amesema Mushi.
Mkazi huyo wa Nanjara Kibaoni ameendelea kusema kuwa: “…wagonjwa, mama wajawazito, tulilazimika kuwavusha kwa mikono kwenda upande wa pili yalipo magari, na hata kama ni msiba ilibidi tutafute utaratibu mwingine au kuzunguka mbali kusafirisha maiti, ila kwa sasa daraja limekamilika na mambo yatakuwa vizuri kabisa."
Victory Maring'a amesema "Kwa sasa hali ni nzuri kwani daraja limejengwa, huduma za usafiri zitakuwa nzuri kwa kwani tutasafirisha hata mazao na bidhaa nyingine kuleta kijijini bila shida, tunaishukuru sana serikali kwa hatua hii muhimu ya maendeleo kwetu."
Akitoa taarifa ya ujenzi wa daraja hilo, Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) Wilaya ya Rombo, Rickson Lema amesema daraja hilo litarahisisha mawasiliano katika vijiji hivyo na kuimarisha huduma za kijamii.
"Mradi huu wa daraja la Mto Wama umegharimu Sh131.5milioni na kukamilika kwa mradi huu kumeimarisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa vijiji vya Wama, Msangai, Nanjara na maeneo jirani, tunaishukuru serikali kuongeza fedha katika bajeti ya 2022/2023 ili kuimarisha miundombinu ya barabara," amesema.
Akizindua daraja hilo, Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Abdalla Shaib Kaim amesema wameridhishwa kwa upande wa nyaraka na mradi wenyewe ambapo ubora na viwango vimezingatiwa.
"Baada ya kupokea taarifa ya kina na kuukagua mradi huu, tumejiridhisha kwa upande wa nyaraka pamoja na mradi wenyewe, ubora na viwango vimezingatiwa," amesema.