Ujenzi usiofuata mpango katika hospitali za rufaa Dar ‘kuikamua’ Serikali

Muonekano wa Hospitali ya Mwananyamala

Dar es Salaam. Kukosekana kwa mipango miji katika ujenzi wa hospitali za rufaa mkoani Dar es Salaam kutaigharimu Serikali kwa kulazimika kubomoa baadhi ya majengo na kujenga mapya.

Ukosefu wa mipango hiyo na ufinyu wa maeneo umekuwa kikwazo katika uendelezaji na upanuzi wa huduma kulingana na ongezeko la idadi ya watu na hadhi ya hospitali hizo zilizoanza kutoa huduma kama zahanati.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, idadi ya watu mkoani Dar es Salaam ni 5,383,728, ikiongezeka kutoka watu 4,364,541 mwaka 2012.

Kutokana na hilo, hospitali za rufaa za Amana, Temeke na Mwananyamala zimeanza kuandaa mipango baadhi ikihusisha ubomoaji wa majengo ili kujenga mapya.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa wiki mbili umebaini maeneo yanayomilikiwa na hospitali hizo, ama yamekwisha kutokana na upanuzi uliofanywa mara kadhaa pasipo kufuata mipango au yanakaribia kwisha.

Hospitali hizi pia zipo katika mazingira yaliyo jirani na makazi ya watu, masoko, vituo vya daladala na maeneo yenye kuhusisha shughuli zenye kelele.

Hali ilivyo Amana

Upanuzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana, umekuwa ukifanyika kwa awamu kiasi cha kumaliza eneo lote lenye ukubwa wa kilomita za mraba 26,642.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Bryceson Kiwelu anasema dira ya hospitali hiyo kwa miaka 60 ijayo ni kuwa bora zaidi nchini na nje ya mipaka, kwa kutoa huduma zenye kukidhi mahitaji ya jamii. Pia kuwa na utalii wa matibabu.

Dk Kiwelu anasema wameshaandaa eneo kulingana na mpango na kwamba, hatua za awali za maandalizi zinafanywa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (Must) na utahusisha majengo ya kisasa yatakayotumia nishati ya jua.

Hospitali hiyo itatumia maji ya ardhini kupunguza gharama za ununuzi kutoka Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa).

Anasema watakuwa na huduma za kibingwa katika fani zote za afya, hususan za uzazi na ukunga.

“Tuna mpango wa kutoa huduma zitakazovuta nchi jirani, lakini kuwa kitivo cha utafiti kuwezesha kuibua mbinu bora zaidi za matibabu, kuzuia magonjwa na kuboresha maisha ya watu,” anasema.

Dk Kiwelu anasema mpango kwa sasa ni kuwa na chuo kikuu cha sayansi ya afya ili kuzalisha wataalamu wenye sifa, weledi na utayari wa kutatua changamoto za afya.

Anasema kwa miaka zaidi ya 20, wameomba kupatiwa eneo la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kiwanja na 143 kinachopakana na hospitali chenye ukubwa wa ekari 2.9.

Kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, anasema walipeleka maombi NHC ili kupata eneo hilo, lakini walielezwa wizara ndiyo ishughulikie kwa kuwa ndiyo yenye dhamana ya kuomba eneo hilo.

Mkurugenzi wa huduma za tiba Wizara ya Afya, Profesa Paschal Ruggajo anasema eneo hilo limeombwa kwa muda mrefu tangu mwaka 2015.

Anasema kwa kuwa linahusisha sekta zaidi ya moja, limekuwa na mchakato mrefu kulipata, lakini suala hilo lipo ukingoni.

Dk Kiwelu anasema: “Amana inahudumia wakazi milioni 1.5 kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022. Kila robo ya mwaka tunahudumia wateja 45,000 ambao hupata huduma kama wagonjwa wa nje au huduma za kulazwa katika idara saba na vitengo zaidi ya 23.

“Mwaka 1956 wakati inaanzishwa hapa palikuwa na majengo madogo yaliyotumika kutoa huduma. Wakati huo ilihudumia wakazi wa Kariakoo na jirani, huku kulikuwa mwishoni mwa mji. Huko mbele Buguruni na kuendelea ilikuwa msitu,” anasema.

Hili linathibitishwa na Mwanaisha Yahaya (82), mkazi wa Ilala aishiye jirani na hospitali hiyo anayesema awali eneo hilo lilikuwa pembezoni mwa mji, lakini watu walisogea taratibu kwa kuanzisha makazi.

Miaka 69 sasa tangu ilipoanza kutoa huduma, mita chache kutoka hospitali hiyo, kuna eneo la wazi linalojulikana kama Vijana Center, likiwa na shughuli mbalimbali zenye kuhusisha kelele za muziki. Kuna soko la Ilala, maarufu kwa uuzaji wa vyakula na mavazi.

Amana kwa sasa ni kituo cha rufaa kwa hospitali na vituo vya afya 224 mkoani Dar es Salaam.

Hata hivyo, inakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa eneo la kutolea huduma na miundombinu chakavu isiyokidhi idadi kubwa ya wanaohitaji kuhudumiwa.

Hali hiyo imesababisha msongamano wa wagonjwa wodini na katika kliniki, kukosekana kwa baadhi ya huduma muhimu, kama vipimo vya MRI.

Baadhi ya idara zinakosa wodi za kulaza wagonjwa, ikiwamo ya magonjwa ya afya ya akili. Pia huduma za upasuaji hufanyika kwa uchache, kutokana na ufinyu na uchache wa vyumba vya upasuaji na wala hakuna huduma ya dawa za methadone.

Pia kuna uchache wa maegesho ya magari na changamoto ya maji kutuama wakati wa mvua.

Akizungumzia changamoto hizo, Dk Kiwelu anasema wana mpango wa kuzipatia ufumbuzi, japo kwa sasa wanahuisha miundombinu iliyopo kwa fedha za ndani wakishirikiana na wadau wa maendeleo.

Changamoto nyingine ni baadhi ya maeneo kutounganishwa na mfumo mkuu wa majitaka, hivyo hugharimika kuyanyonya.

Hata hivyo, Dk Kiwelu anasema wanashirikiana na Dawasa kuunganisha maeneo kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.

Upungufu wa watumishi ni changamoto nyingine inayosababisha ongezeko la kazi kwa waliopo, hivyo hushindwa kutoa baadhi ya huduma kwa ufasaha.

“Upungufu ulikuwepo kwa asilimia 44 na tulianza kwa kuajiri watumishi wa mkataba 121. Utatuzi mwingine ni kuajiri watumishi wa kudumu kupitia Serikali Kuu,” anasema.


Upanuzi Mwananyamala

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala ina eneo kubwa zaidi ukilinganisha na Amana na Temeke, ijapokuwa linakaribia kwisha kutokana na ujenzi unaofanyika.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Zavery Benela anasema walipokea maelekezo ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliyewataka kuandaa mpango kwa kuwa upanuzi uliofanyika awali haukuzingatia hilo.

Anasema kupitia mpango huo, baadhi ya majengo yataendelea kutumika yalivyo na utaonyesha wapi patumike kwa huduma ipi.

Dk Benela anasema kuna uhaba wa wodi, nyumba za watumishi na vyumba sita vya upasuaji, hivyo baadhi ya majengo yatabomolewa ili kujenga ghorofa.

Anasema mpango utakuwa shirikishi na utaangalia malengo ya muda mrefu ya Mwananyamala kwa kuwa wananchi wanaongezeka na hakuna ardhi nyingine.

Anasema kuna wazo la kununua eneo la ujenzi kutoka kwa wananchi wanaouza maeneo yaliyo jirani na hospitali hiyo.

Dk Benela anasema walishafanya uchunguzi uliobaini gharama za maeneo hayo ni kati ya Sh200 milioni na Sh300 milioni, hivyo wanajipanga kuona namna gani wataongeza eneo la hospitali kwa fedha za ndani.

“Bado idadi ya wagonjwa tunaowahudumia ni kubwa na watumishi wengine wako shule na wengine wanahitaji kuongezwa, ikama haitoshelezi. Wapo wanaopata huduma ya dawa za methadone, ambao ni wengi, kila siku 1,300, eneo ni dogo na wakinywa hawaondoki kwa wakati, tunahitaji eneo lao,” anasema.

Hospitali ya Temeke

Miaka 51 tangu kuanzishwa zahanati ya Temeke mwaka 1972 sasa inajulikana Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke, ikihudumia zaidi ya watu milioni mbili katika eneo lenye mita za mraba 18,861.

Licha ya idadi kubwa ya watu wanaopatiwa huduma, eneo la hospitali ni dogo katika utoaji huduma, huku ujenzi ukifanyika pasipo kuzingatia mpango.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Vicent Kimaro anasema wanaendelea kutoa huduma kwenye vituo vinavyowazunguka ili kupunguza rufaa hospitalini hapo.

Dk Kimaro anasema wanahudumia watu zaidi ya milioni mbili kutoka manispaa za Temeke, Kigamboni, Mkuranga na baadhi wanatoka Kisarawe.

“Kutokana na idadi ya watu kuongezeka na wakati mwingine Muhimbili huwa inazidiwa, ndiyo maana hospitali hizi zimeanzishwa kwa lengo la kutoa huduma za kibingwa na karibu zaidi na wananchi,” anasema.

Bila kufafanua, anasema wameandaa mpango na umewasilishwa Wizara ya Afya.

Kauli ya Wizara

Kuhusu upanuzi, Profesa Ruggajo anasema Tanzania ina mikoa 26, lakini hospitali za rufaa za mkoa zipo 28, Dar es Salaam zikiwa tatu. Anasema mipango inayoendelea ya kuzitanua ni maagizo ya Wizara ya Afya.

"Tulishaagiza hospitali zote mpya na zinazotanuka ziwe na master plan (mipango miji), pili tunazitaka zitafute nafasi nje ya mji ili ziweze kutanua huduma za tiba na vyuo kwenye mipango yao ya muda mrefu," anasema.

Akizungumzia hospitali ya Mwananyamala, anasema: "Pale pamefinywa, ni padogo. Kujenga ghorofa wameshauriwa hivyo na Waziri kwa hiyo wanaendelea na mchakato, lakini kuna suala la kuongeza eneo hivyo wanaangalia kununua hapo hapo.

"Temeke hakuna kabisa eneo kwa sasa, wanafuatilia Manispaa ya Temeke kuangalia namna gani wanaweza kutanua kutumia ule uwanja jirani au gereji, lakini nao tuliwaagiza watafute maeneo ya kutanukia na ikibidi wawe na mawazo mapana zaidi, ikiwemo kuanzisha vyuo," anasema.

Profesa Ruggajoo anasema juhudi zinaendelea na Wizara inazidi kuimarisha hospitali za wilaya, halmashauri na vituo vya afya, ili kupunguza rufaa za hospitali tatu za mkoa kwa kupeleka vifaatiba, ujuzi na kuwezesha miundombinu.

Kwa upande wake, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dar es Salaam, Shukrani Kyando anasema ujenzi wa kuongeza ghorofa unapaswa kufuata utaratibu kwa mujibu wa sheria ya mipango miji namba 8 ya mwaka 2017.

"Taratibu zote za uendelezaji miji zinamilikiwa na anayesimamia hospitali kwa maana ya mkurugenzi na zijengwe ghorofa ngapi, vyote anasimamia yeye, hakuna changamoto kubwa," anasema.

Anasema iwapo upanuzi utagusa maeneo ya watu, itabidi wananchi wajulishwe, walipwe fidia na baada ya hapo wapishe maeneo kwa ajili ya matumizi ya umma.

Arnold Mapinduzi, meneja kanda ya Mashariki Kaskazini wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), anasema upanuzi wa hospitali hizo utatakiwa kushughulikiwa na watu wa mipango miji.

Anashauri iwapo hospitali hizo hazina maeneo ya kutosha, zinaweza kutafuta mengine na kuhamishia baadhi ya shughuli kama ilivyo kwa Hosptali ya Taifa Muhimbili, ambayo imejenga Mloganzila.

“Tunawaambia wazingatie tathmini ya athari kwa mazingira. Kifungu cha 81 cha usimamizi wa mazingira mtu akitaka kujenga lazima apate kibali cha mazingira.

“Ataleta mradi kama inavyopendekezwa, mchakato utaendelea na wanaotoa vibali vya ujenzi na sisi tunaangalia mipango miji inaruhusu? Je, upanuzi unaendana na matumizi ya ardhi, kama ndivyo tunaanzia hapo,” anasema Mapinduzi.

Imeandikwa kwa udhamini wa Bill & Melinda Gates Foundation