Ujerumani Magharibi yaahidi msaada kwa Tanganyika

Ujerumani Magharibi yaahidi msaada kwa Tanganyika

Muktasari:

  • Wakati siku ya uhuru ikikaribia, changamoto ilikuwa namna gani Tanganyika itatekeleza mipango yake ya maendeleo, lakini baadhi ya nchi zilijipambanua kama marafiki wa kweli


Wakati siku ya uhuru ikikaribia, changamoto ilikuwa namna gani Tanganyika itatekeleza mipango yake ya maendeleo, lakini baadhi ya nchi zilijipambanua kama marafiki wa kweli

Septemba 1961, Ujerumani Magharibi ilituma barua rasmi kwa Waziri Mkuu wa Tanganyika, Julius Nyerere ambayo ilitumwa na kiongozi wa nchi hiyo, Kansela Dk Konrad Adenauer.

Barua hiyo ilieleza kuwa nchi hiyo kwa kushirikiana na Uingereza na mataifa mengine, imekubali kuisaidia Tanganyika kifedha ili kufanikisha utekelezaji wa mpango wake maendeleo wa miaka mitatu kwa mafanikio.

Nyerere alimweleza balozi wa nchi hiyo, Herr Scholler aliyewasilisha barua hiyo kwamba Serikali pamoja na watu wa Tanganyika wamefurahishwa na kitendo hicho cha kipekee kilichofanywa na Taifa lake.

“Kwa sasa Serikali ya Tanganyika kwa kushirikiana na Uingereza, ilikuwa inaandaa mapendekezo kuhusu namna bora ya kutumia msaada huo,” alisema Nyerere.

Chanzo: Gazeti la Tanganyika Standard

Waziri Amir Jamal awataka Watanganyika kufanya kazi kwa bidii

“Kuteremsha bendera ya sasa na kupandisha ile ya Taifa jipya la Tanganyika ni kitendo rahisi sana na tukifanya hivyo bila kufanya bidii katika kazi zetu za kushirikiana kama zamani, tutakuwa tunatukana uhuru wetu,” alisema Waziri wa Njia, Umeme na Majengo, Amir Jamal alipokuwa akihutubia umati wa watu katika eneo la Usa River, Arusha.

Jamal aliendelea kusema kuwa Tanganyika imesifiwa sana na mataifa mengine ulimwenguni kwa siasa yake tulivu na ambayo imeiletea uhuru bila fujo na kumwaga damu.

“Kwa takribani miaka saba tumepigania uhuru huu ambao tunatarajia kuupata hivi karibuni tukiwa na nia ya kuwa kila binadamu aheshimiwe bila kuangalia rangi tu,” alisema Jamal.

Alisema: “Watu wa nchi jirani wanauliza kwa nini tumepata uhuru haraka hivi kuliko nchi nyingine? Jibu lake ni kwamba tumekuwa na umoja, ushirikiano kwa madhumuni ya kujipatia uhuru huu na baada ya uhuru si kukaa chini na kusema tutapata kila kitu.”

Chanzo: Gazeti la Kusare

Nyerere atia saini ilani ya ulinzi wa wanyamapori

Waziri Mkuu wa Tanganyika, Julius Nyerere ametoa ahadi ya Tanganyika kuendelea kusimamia ulinzi wa wanyamapori kwa nguvu zake zote.

Nyerere aliyasema hayo wakati wa mkutano wa kimataifa wa wanyamapori uliofanyika jijini Arusha Septemba, 1961.

Katika mkutano huo Nyerere alitia saini ilani ya ulinzi wa wanyamapori inayoweka msisitizo kwamba Tanganyika iko tayari kuilinda rasilimali hiyo muhimu.

Mbali na Nyerere, ilani hiyo pia ilitiwa saini na Waziri wa Ardhi na Utafiti, Tewa Saidi Tewa na kusomwa na Waziri wa Sheria, Chifu Abdallah Fundikira.

Mmoja wa wageni katika mkutano huo, Sir Julian Huxley aliielezea ilani hiyo kuwa ni hatua muhimu kwa Afrika na dunia katika kulinda wanyamapori na uoto wa asili.

Ilani hiyo ilisema kuwa “maisha ya wanyamapori wetu ni kitu cha kuzingatiwa sana na Waafrika wote.”

Chanzo: Gazeti la Tanganyika Standard

Serikali yatangaza maonyesho siku ya uhuru

Serikali kupitia kamati ya maandalizi ya sherehe za uhuru ilitangaza kwamba siku ya uhuru kutakuwa na maonyesho maalumu ya biashara, kilimo na kazi za viwandani ili kuonyesha historia ya shughuli hizo.

Maonyesho hayo ambayo yangekuwa ya kwanza kufanyika katika historia ya Tanganyika yatafanyika kwenye uwanja wa ndege wa Dar es Salaam kuanzia Desemba 9 mpaka 12 na yataendeshwa na Wizara ya Viwanda na Biashara.

Mazao ya wakulima yataonyeshwa na vyama vyote vya biashara na viwanda nchi nzima, ambavyo vimealikwa kushiriki maonyesho hayo.

Serikali ilisema wanaotaka kuleta vitu vyao kwenye maonyesho hayo hawatalipa ushuru, pia maji na taa vitatolewa bure.

Aidha ilisema kampuni zitakazotaka kukodisha madirisha ya kuonyesha bidhaa zao watalipa ushuru kiasi fulani.

Wanaotaka kushiriki wanatakiwa kutuma maombi yao kupitia anwani ya: Exhibition Section, Ministry of Commerce and Trade, P.O.Box 234 Dar es Salaam.

Chanzo: Gazeti la Busara