Ujumbe wa Othman siku ya kwanza ofisini

Muktasari:

Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar,  Othman Masoud Sharif  ameanza kazi rasmi leo Jumatatu Machi 8, 2021  huku akiwaonya watendaji kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Unguja. Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar,  Othman Masoud Sharif  ameanza kazi rasmi leo Jumatatu Machi 8, 2021  huku akiwaonya watendaji kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

“Kikubwa zaidi ni uwajibikaji kwa watendaji na kujua majukumu yao kwani taasisi ikijua majukumu yake, pia ufanisi utapatikana,” amesema Othman.

Ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na watendaji wa ofisi yake Migombani Unguja ikiwa ni mara ya kwanza kuwasili ofisini hapo tangu alipoapishwa.

Amewataka viongozi wa idara katika ofisi hiyo kuhakikisha wanazipitia upya sheria zilizopo ili ziweze kuwa rafiki ambazo zitamsaidia mwananchi wa kawaida badala ya maslahi ya watu fulani.

"Idara zetu ziwe rafiki kwa jamii na zisiwe sababu ya kukwamisha maendeleo" amesema Othman.

Akimkaribisha makamu wa kwanza wa rais, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Saada Mkuya amesema ana matumaini makubwa na Othman kuhusu utendaji kazi wake na kwamba hataiangusha Serikali wala wananchi wa Zanzibar.

Amewataka viongozi na wakuu wa idara kuhakikisha wanawawajibisha watendaji wasiofuata misingi ya utumishi huku wakiwapongeza na kutoa motisha kwa wanaofanya vyema.