Ukaguzi magari ya wanafunzi Arusha wasuasua, Polisi waonya

Ukaguzi magari ukiwa unaendelea kituo cha usalama barabarani jijini Arusha. Picha Jenipher Mbwambo.

Muktasari:

Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani lianza ukaguzi wa magari ya kubeba wanafunzi huku ambao hawatapeleka magari kukaguliwa, hatua kali za kisheria zitachukuliwa.

Arusha. Shughuli ya ukaguzi wa magari ya shule mkoani Arusha inasuasua baada ya wamilimi wachache wa shule kujitokeza kupeleka magari yao kwa ajili ya ukaguzi huku Jeshi la Polisi mkoa huo likitoa onyo kwa ambao hawatakwenda kwenye ugauzi huo hadi Agosti 13, 2022 watafutiwa leseni.

 Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne, Agosti 9, 2022, wakati wa shughuli ya ukaguzi ikiendelea, Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani mkoa Arusha, Solomon Mwangamile amesema ni lazima magari yote yanayobeba wanafunzi yakaguliwe.

"Ukaguzi wa usalama barabarani ni jukumu letu sote na sio la mtu mmoja mmoja, kila mmoja ana wajibu wa kuangalia usalama wake na mwenzake pia," amesema

 Mwangamile amesema ukaguzi wa magari ya wanafunzi ambao umeanza jana utakamilika Agosti 13, 2022.

"Lengo kubwa la ukaguzi huu ni kuhakikisha kwamba magari haya yanayobeba wanafunzi yanakuwa katika ubora na vigezo ambavyo vinastahili kwa mujibu wa sheria," amesema

Amesema ukaguzi ni wa lazima hivyo amesisitiza kwa wamiliki wote wa magari ya wanafunzi kupeleka magari hayo kukaguliwa katika kipindi hiki ambapo wanafunzi wamefunga shule.

Mwangamile amesema gari litakapokaguliwa na kuonekana lina uwezo mzuri na lina ubora wa kubeba wanafunzi litapewa hati maalumu ya ukaguzi.

"Endapo kuna mtu yeyote hatofikisha gari lake katika ukaguzi na kulitumia kubeba wanafunzi shule zitakapofunguliwa watashirikiana na mamlaka ya usafiri wa ardhini (Latra) kumchukulia hatua kali ikiwemo kumfungia leseni yake ya usafirishaji," amesema

Tangu kuanza ukaguzi wa magari Agosti 4, 2022 magari machache yamefikishwa kukaguliwa katika Jiji la Arusha ambapo kuna idadi kubwa ya shule binafsi.

Imeandikwa na Jenipher Mbwambo