Ukuzaji broila kwa dawa unavyotishia afya za walaji

Muktasari:

Kutokana na athari zake kwa afya ya binadamu, mazingira na mifugo yenyewe, wataalamu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wameonya kuhusu matumizi holela ya dawa za kunenepesha mifugo.

Dar es Salaam. Utafiti uliofanywa katika masoko ya Shekilango na Manzese jijini Dar es Salaam, na kuchapishwa kwenye Jarida la MDPI la Basel la nchini uswisi, umebaini kuwapo kwa kiasi kikubwa cha mabaki ya sulphonamide na tetesaklini, antibayotiki zinazotumiwa zaidi na wafugaji kwenye maini ya kuku wa kisasa.

Utafiti huo ulichapishwa Septemba 8 kwenye Jarida la MDPI la Basel nchini uswisi kwa jina la ‘Determination of Sulphonamides and Tetracycline Residues in Liver Tissues of Broiler Chicken Sold in Kinondoni and Ilala Municipalities, Dar es Salaam, Tanzania’ ulihusisha sampuli 84 za maini ya kuku wa kisasa, ukilenga kuangalia kiasi cha mabaki ya dawa hizo kama kinaendana na kinachopendekezwa na viwango vya kimataifa.

“Mazingira ya ufugaji sio salama sana ndio maana wafugaji wanalazimika kuipa mifugo dawa kiholela bila kujua kwa kufanya hivyo, wanahatarisha afya za walaji wa bidhaa za mifugo yao, mazingira na mifugo mingine,” alisema Profesa Mecky Matee, mhadhiri mwandamizi Muhas aliyeshiriki kufanya utafiti huo.

Profesa Matee alishirikiana na Dk Zuhura Kimera na Fauster Mgaya wa chuoni hapo, pamoja na Winstone Ulimo wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Matokeo ya utafiti huo yameonyesha maini yote 84 yalikuwa na mabaki ya tetesaklini huku 18 sawa na asilimia 21.4 yakiwa na mabaki ya sulphonamide na mengine 18 yakiwa na mabaki ya vyote.

Wakati mabaki ya sulphonamide yalikuwa ndani ya kiwango kinachokubalika kiafya, lakini maini 76 sawa na asilimia 90.5 yalikuwa na kiasi kikubwa kuzidi kile kinachoshauriwa kuliwa na binadamu kwa siku. Maini 13 sawa na asilimia 13.1 yalizidi kiwango cha juu cha tetesaklini kinachoshauriwa kuliwa yakiwa na mikrogramu 300 kwa kila kilo moja.

“Kuwapo kwa kiwango kikubwa cha antibayotiki kwenye maini ya kuku kunahatarisha maisha ya walaji na kunaweza kusababisha usugu katika kutibu magonjwa yanayopaswa kutibiwa na dawa hizo,” inasema ripoti hiyo.

Ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza, watafiti hao wanashauri kuongezwa kwa ufuatiliaji wa matibabu au uchanjaji wa kuku na mifugo mingine, inayotumia antibayotiki kwa kuhakikisha kunakuwa na muda wa kutosha dawa hizo kutumika mwilini, kabla bidhaa zake hazijaliwa na binadamu.

Watafiti hao wamependekeza kupigwa marufuku hamasa ya matumizi ya dawa za kukinga, kutibu na kunenepesha mifugo na hatua za kuzuia na kupambana na maambukizi zichukuliwe ikiwamo kusisitiza chanjo.

“Tunaiomba Serikali ya Tanzania kusimamia vilivyo matumizi ya dawa kwenye mifugo. Wananchi waelimishwe muda sahihi wa kuchinja au kutumia bidhaa baada ya kuipa mifugo dawa. Vilevile, tunashauri madaktari wasaidizi wa mifugo wanaowazungukia wafugaji wapewe mafunzo ya muda mafupi ili kuwajengea uwezo kudhibiti matumizi ya dawa hizi,” unasomeka ushauri wa wataalamu hao.

Kutokana na ongezeko la mahitaji ya kitoweo nchini, wafugaji wanalazimika kutafuta namna nzuri ya kukuza mifugo mingi kwa wakati mmoja.

Profesa Matee alisema “Ni muhimu kwanza kuutambua ugonjwa kabla ya kuutibu mfugo husika, kuchanja mifugo kwa wakati kuzuia magonjwa yanayoweza kutokea.

Ingawa mahitaji ya nyama, mayai na maziwa yanazidi kuongezeka nchini, watafiti hao wanaonya kuhusu matumizi ya bidhaa hizo, hasa kwa wanyama waliopewa dawa ndani ya muda mfupi.

Takwimu zinaonyesha ulaji wa nyama ya nguruwe ambao ufugaji wake unazidi kushika kasi nchini unatarajiwa kuongezeka kutoka tani 42,700 kwa mwaka 2017 mpaka tani 170,000 mwaka 2030 huku uzalishaji wa nyama ya kuku ukipanda kutoka tani 22,000 mwaka 2017 mpaka tani 37,200 mwaka huu.

Hata hivyo, wafugaji wengi wanatumia antibayotiki aina ya sulphonamides na tetesaklini (tetracyclines) kuilinda mifugo yao ambazo zikizidi sana kwenye chakula humwathiri mlaji.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Kilimo Duniani (FAO) yameweka viwango vya mwisho ambavyo mtu anashauriwa kutumia antibayotiki hizo kila siku pamoja na ukomo wa mabaki kwenye mwili wa mfugo, kabla bidhaa zake hazijatumika kama chakula.

WHO inapendekeza ulaji wa kati ya mikrogramu sifuri mpaka tatu kwa kila kilo moja.


Wadau watia neno

Mtafiti wa mradi wa Combating African Animal Trypanosomiasis - An Integrated Approach to Tackling Drug Resistance (COMBAAT) wilayani Serengeti, Dk Paul Buyugu alisema matumizi holela ya dawa hizo ni changamoto kwa kuwa usugu wa vimelea mpaka mwaka 2050 utakuwa unasababisha vifo vingi kuliko magonjwa mengine.

“Kwa mfano umeandikiwa usitumie nyama ya mfugo uliopa dawa kwa muda wa siku tano, lakini unakuta mfugaji anawapa dawa leo na kesho anauza bila kujua wanakuwa na chembechembe zinazoweza kuathiri afya ya mtumiaji,” alisema daktari huyo wa mifugo.

Shida iliyopo, Dk Buyugu alisema ni wafugaji kutoangalia au kufuata maelekezo ya ukomo wa matumizi. Alitaja vitu vinavyochangia tatizo hilo kuwa ni elimu ndogo kwa wafugaji na watumiaji wa mazao ya mifugo.

Tatizo jingine alisema ni kutozingatia maelekezo kwani mfugaji anaweza kuambiwa aweke kijiko kimoja kwenye lita tano, akaweka vijiko viwili kwenye lita mbili.

Akichangia hilo, Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST), Fadhili Hezekiah alisema wahusika wote popote walipo wapunguze matumizi ya dawa hasa katika kilimo, mifugo na usafi wa mazingira na inapokuwa lazima basi zitumike kwa viwango na njia stahiki.

“Muda uliowekwa toka matumizi ya dawa na matumizi ya bidhaa husika uzingatiwe, ili kuruhusu dawa kuisha kutoka mnyama au mmea na ikiwezekana kupungua kufika kiwango kinachokubalika na hatua kali zichukuliwe kwa wote wanaokiuka taratibu na umma uelimishwe juu ya hatari ya matumizi holela au kupindukia ya dawa ,” alisema.

Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifelo Sichwale alisema “TBS ni lazima waliona tatizo ndio maana wakafanya utafiti, hivyo wapo kwenye nafasi ya kuishauri Serikali vizuri kutokana na utafiti walioufanya.